Mtwara. Bei ya samaki katika soko la feli lililopo ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani imepanda kwa kasi, huku wauzaji wakieleza kuwa hali hiyo imesababishwa na upatikanaji mdogo wa samaki kutokana na hali mbaya ya hewa, hususan upepo mkali unaovuma baharini.
Wakizungumza leo Mei 31, 2025, baadhi ya wafanyabiashara wa samaki wameeleza kuwa kutokana na uhaba huo, wanalazimika kununua samaki kwa bei ya juu na hivyo kuuza kwa gharama kubwa zaidi ili kuokoa mitaji yao na kuendeleza biashara.
Wafanyabiashara hao wameiomba Serikali kuwasaidia wavuvi kwa kuwapatia vifaa vya kisasa vitakavyowawezesha kuvua samaki kwa ufanisi nyakati zote za mwaka wakiamini kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama na kuongeza upatikanaji wa samaki sokoni.

Shufaa Mohamedi, mmoja wa wachuuzi wa samaki katika feli hiyo, amesema upatikanaji wa samaki kwa sasa ni mdogo mno, kiasi kwamba ndoo moja inauzwa hadi Sh100,000.
“Awali, tulikuwa tunanunua ndoo moja kwa Sh25,000 hadi Sh30,000, lakini sasa bei imepanda hadi Sh80,000 au Sh100,000. Sisi wenye mitaji midogo hatuwezi kumudu kuendesha biashara. Tunaomba Serikali iwasaidie wavuvi kwa vifaa vya kisasa ili waweze kuvua kwa ufanisi, maana walaji ni wengi kuliko samaki waliopo sokoni,” amesema Shufaa.
Zainabu Dadi, mfanyabiashara mwingine wa samaki katika soko hiyo, amesema hali hiyo imekuwa ngumu kwao kwani dagaa ambao awali waliweza kununua kwa Sh30,000 kwa ndoo ndogo, sasa wanauziwa hadi Sh60,000.
“Samaki wamepanda bei sana, tunateseka kama wafanyabiashara. Hali hii inatokana na vifaa duni vya kuvulia samaki. Hatuna sehemu nyingine ya kutegemea; hapa ndipo tunapata fedha za kulipia ada za watoto na gharama nyingine za maisha. Tunaomba Serikali iwasaidie wavuvi vifaa bora ili tupate samaki kwa wingi,” amesema Zainabu.
Kwa upande wake, Mwamvita Mkwaya ambaye pia ni muuza samaki katika eneo hilo, amesema hali ya sasa ya upatikanaji wa samaki si nzuri na hivyo kuathiri bei sokoni.
“Kwa sasa samaki hawapatikani kabisa, na bei imekuwa juu sana. Samaki tuliokuwa tunanunua kwa Sh15,000 na kuuza kwa Sh20,000, sasa tunanunua kwa Sh25,000 na kuuza kwa Sh30,000. Wale wa Sh12,000 sasa wanauzwa hadi Sh25,000. Hii inaathiri sana biashara yetu,” amesema Mwamvita.
Baadhi ya wavuvi wameeleza kuwa upepo mkali baharini ndio chanzo kikuu cha upungufu wa samaki kwani wengi wao hawawezi kwenda kuvua kutokana na vifaa duni na hali hatarishi ya bahari.
Nassoro Ally Salimu, mkazi wa Zanzibar ambaye kwa sasa yupo Mtwara kwa ajili ya shughuli za uvuvi, amesema upepo mkali unawafanya samaki kujificha, hivyo kuathiri upatikanaji wake.
“Samaki kwa sasa hawaonekani kabisa kutokana na upepo. Wanaojaribu kwenda kuvua ni wavuvi wadogo wenye uwezo mdogo, hivyo wanarudi na samaki wachache sana. Hali hii inafanya bei kupanda na watu wenye kipato kidogo kushindwa kumudu,” amesema Nassoro.
Ameongeza kuwa hali hiyo inawaathiri moja kwa moja kimaisha kwa kuwa hutegemea uvuvi kujipatia kipato.
“Kama hatuwezi kwenda baharini, basi hatupati kabisa fedha za matumizi wala kutimiza malengo tuliyojiwekea. Tunateseka sana,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wavuvi Manispaa ya Mtwara, Sheha Shamte, amesema kupanda kwa bei ya samaki kunatokana na upatikanaji mdogo wa bidhaa hiyo.
“Bei huwa juu samaki wanapopatikana kwa uchache. Tunapowapata kwa wingi, bei hushuka. Kipindi kama hiki samaki aina ya damudamu walipaswa kupatikana kwa wingi, lakini hali sivyo. Tunashindwa hata kupeleka chombo baharini maana gharama ni kubwa chombo kinahitaji kama Sh100,000 ili kwenda kuvua, lakini ukirudi bila chochote, unapata hasara kubwa,” amesema Shamte.

Ameongeza kuwa wavuvi hawana sehemu ya kukimbilia wanapopatwa na changamoto za kifedha au vifaa kuharibika.
“Tunaomba Serikali ituone kama sehemu muhimu ya uchumi. Tuwekewe mazingira ya kupata mikopo ya dharura au vifaa kama mashine na nyavu tunapopatwa na dharura,” amesema.