Njombe. Watumishi wa halmashauri ya Mji Njombe wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa ili kuleta matokeo chanya kwa halmashauri na wananchi wanaohudumiwa.
Wito huo umetolewa leo Mei 31, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Kuruthum Sadick wakati wa dua ya kuwaombea watumishi wa halmashauri hiyo iliyofanyika huko wilayani Njombe.
Amesema wanapoelekea mwishoni mwa mwaka wa fedha na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, Mungu awape afya njema na akili ili wafanye kazi zao kwa juhudi na usalama kwa kuzingatia sheria na kanuni.
“Tunaelekea mwishoni mwa mwaka wa fedha, katika kumshukuru Mungu tumeamua kuwaita watumishi wa Mungu ili kutuombea afya njema na tuweze kufanya kazi zetu vizuri,” amesema Sadick.

Amesema maombi na dua kutoka kwa viongozi wa dini mkoani humo yatawasaidia watumishi kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili, weledi, haki na sheria zilizopo katika halmashauri na nchi kwa ujumla.
Amesema baada ya kutimiza majukumu ya ofisi mtumishi ana haki ya kujishughulisha na vitu vingine ambavyo vitamwingizia kipato ili kuweza kustawi kwani wapo kwa ajili ya kutumikia nchi na kuangalia masilahi yao pia.
Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu, Samson Meda amesema mafanikio, mshikamano na upendo uliopo ndani ya halmashauri hiyo vinatokana na uwepo wa Mungu.
“Ndiyo maana leo tumeona tuwe na siku maalumu ya dua kwa ajili ya kuendelea kuiombea halmashauri kuendelea kudumisha upendo, amani, mshikamano, usalama na ustawi wa halmashauri kwa ujumla wake,” amesema Meda.
Baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo, Datius Bitanuzile amesema maombi hayo yanakwenda kuwabadilisha na kuwa na roho za nyama na si jiwe kama ambavyo mafundisho ya Mungu yanavyosema.
“Kwa hiyo Mungu anakwenda kutubadilisha katika utendaji wetu wa kazi katika ushirikiano najua tunategemeana kati ya idara na idara , mfanyakazi mmoja na mwingine” amesema Bitanuzile.
Naye Elizabeth Kayani ameomba halmashauri hiyo kuendelea kutenga muda kwa ajili ya maombi ya mara kwa mara, ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na ustawi wa jamii kwa ujumla.
“Kwa kweli tumepokea haya maombi vizuri sana kwani ni jambo jema na la baraka kwetu sisi watumishi wa halmashauri ya mji tunamshukuru Mungu na hili jambo liendelee siku zote kwa sababu ni baraka na kumtukuza Mungu,” amesema Kayani.
Shekhe wa Mkoa wa Njombe, Rajabu Msigwa ameupongeza uongozi wa halmashauri hiyo kwa kubuni jambo hilo kwani ili kufanikiwa katika nyanja yoyote ni vizuri kumtanguliza Mungu.
“Mungu anasema ukinishukuru nitakupa zaidi hivyo ni muda wa kutengeneza nyoyo zetu kwa kupendana, kushirikiana katika kazi au majukumu yoyote kwakuwa tunategemeana,” amesema Msigwa.