Heche: Tanga inafaa kwa fursa za  kiuchumi

Korogwe. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche amesema Tanga inafaa siyo tu kuwa mji wa bandari na viwanda kama ulivyo Guangzhou nchini China, bali maisha na maendeleo ya wakazi wake yanatakiwa kuakisi fursa za kiuchumi zinazopatikana mkoani humo.

Kiongozi huyo ambaye yuko kwenye ziara ya kampeni ya chama hicho ya kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi kupitia kauli mbiu ya ‘No reforms, no election’ amesema hayo leo Jumapili Juni mosi, 2025  alipohutubia mkutano wa hadhara mjini Korogwe.

Amesema Chadema ikipata dhamana ya kuunda na kuongoza Serikali, itaufanya mji na Mkoa wa Tanga kuwa wa bandari na viwanda hasa vile vya kuchakata na kuongeza thamani za bidhaa zinazotokana na mkonge.

Amesema Serikali ya awamu ya kwanza chini ya hayati Mwalimu Julius Nyerere iliendeleza kilimo cha mkonge na ujenzi wa viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani bidhaa zinazotokana na zao hilo ili kukuza uchumi wa wakazi wa Tanga na Taifa kwa jumla.

Amedai kuwa, malengo ya Mwalimu Nyerere kuhusu maendeleo ya Tanga na Taifa kupitia mkonge, yamekufa baada ya kilimo cha zao hilo na viwanda vilivyojengwa kufa kutokana na sera na usimamizi mbovu.

Amedai kuwa, Taifa limekuwa likitumia zaidi ya Sh70 bilioni kuagiza bidhaa zinazotokana na mkonge ikiwamo magunia na vifungashia vingine.

“Tungekuwa na sera nzuri ya kuendeleza kilimo cha mkonge na viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani zao hilo, fedha zote tunazotumia kuagiza bidhaa ya mkonge kutoka nje zingebaki nchini kutekeleza miradi ya maendeleo na kukuza uchumi wetu,” amesema Heche.

Amesema maendeleo yaliyopo katika miji ya Guangzhou nchini China na Dubai ni mifano hai namna uwekezaji kwenye ujenzi wa bandari na viwanda unavyokuza uchumi wa watu na Taifa kwa jumla.

Madai ya kukimbia uchaguzi

Akizungunzia madai ya chama hicho kukimbia uchaguzi, Heche amesema: “Chadema hatuogopi kushiriki wala hatuwezi kuukimbia uchaguzi; tunachokidai ni mabadiliko ya sheria na mfumo itakayofanya chaguzi zetu kuwa siyo tu huru na haki, bali pia kura za wananchi ziheshimiwe kwa anayepata kura nyingi kutangazwa kuwa mshindi.”

Amesema kuheshimu kura za wananchi siyo tu inarejesha mamlaka ya umma kuwawajibisha viongozi wao, bali pia itaongeza uwajibikaji kwa wote wanaokasimiwa madaraka kwenye ofisi za umma, kwa sababu watahofia kuwajibishwa kwa kuondolewa madarakani kupitia sanduku la kura.

Amedai kuwa, sheria na mfumo uliopo, siyo rahisi kwa viongozi wakuchaguliwa kuwaogopa na kuwajibika kwa wapigakura kwa sababu wengi wanapata nafasi hizo bila kushinda.

 Katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema wakazi wa Tanga mjini wanarekodi nzuri ya kukikataa chama tawala, ingawa wana kumbukumbu mbaya ya uchaguzi wa mwaka 2020 na 2024.

“Chadema tumechukua msimamo wa No reforms no election, tunataka uchaguzi uwe huru lakini Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ikawaita makatibu wa vyama kwenda kusaini kanuni, mimi sikwenda hadi mifumo ibadilishwe kwanza,” amesema.

Wakati huohuo, Heche amehamasisha na kupokea michango ya fedha kutoka kwa wananchi wanaohudhuria kupitia kampeni ya chama hicho ya ‘Tone Tone’ inayolenga kuushirikisha umma kuchangia gharama za shughuli za siasa zikiwamo ziara za viongozi na mikutano ya hadhara.

Kampeni ya ‘Tone Tone’ imezidi kushika kasi katika kipindi ambacho Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetangaza kusitisha ruzuku ya kila mwezi ya zaidi ya Sh100 milioni kwa Chadema.

Uamuzi huo umetokana na kile kinachodaiwa ni ukaidi wa chama hicho kuhusu msimamo wa kutowatambua viongozi na wajumbe wanane wa kamati kuu walioteuliwa na kupitishwa na Baraza Kuu Januari 22, 2025.

Katika maagizo na maelekezo yake, Ofisi ya Msajili iliuagiza uongozi wa Chadema kuitisha kikao cha Baraza Kuu kuwapitisha viongozi hao ikidai, akidi ya kikao cha Januari 22, 2025 hakikutimia.

Chadema kupitia ilitangaza kupinga maagizo na uamuzi wa Ofisi ya Msajili kwa madai kuwa, yako nje ya mamlaka ya msajili kwa mujibu wa sheria na imepanga kukutana Jumanne Juni 3, 2025 katika kikao cha dharura cha kamati kuu.

Related Posts