Ofisa TFS Kibiti kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji

Dar es Salaam. Mtumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Idara ya Maliasili Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa, akituhumiwa kumuua Haji Mnette kwa kumgonga na gari.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo.

Katika tukio hilo, ofisa huyo wa maliasili alidaiwa kumgonga Haji Mnette kwa gari hadi kusababisha kifo chake, jambo lililoibua malalamiko na hasira kutoka kwa wananchi.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa leo Juni 1, 2025, Kamanda Msaidizi wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Rufiji, Kanuti Msaki amesema kuwa uchunguzi wa kesi hiyo umeshakamilika.

Amemtaja mtuhumiwa kwa jina la Masoud, na kusema kuwa atapandishwa kizimbani wakati wowote kuanzia sasa.

 “Masoud ambaye ni dereva wa gari la TFS, atafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa, atafikishwa mahakamani yeye peke yake miongoni mwa wengi waliokuwa ndani ya gari hilo, kwa makosa ya kusababisha kifo cha bodaboda,” amesema.

Tukio hilo la lililoacha simanzi kwa wananchi wa Kibiti, lilitokea asubuhi ya Mei 27, 2025 wakati Mnette, aliyekuwa akiendesha pikipiki alipogongwa na gari hilo kisha kupasuka kichwani na kusababisha kifo chake.

Baadaye Kanali Kalombo aliagiza Masoud awekwe ndani ili wananchi waliokuwa na taharuki baada ya tukio hilo, wawe watulivu wakati suala hilo likifanyiwa kazi.

Awali, Kabla ya Kamanda Kanuti kuzungumza, Mwananchi ilimtafuta Kanali Kalombo aliyejibu, “jambo lilifikishwa Polisi na sijafuatilia kwa leo, lakini lipo mikononi mwao wanalifanyia uchunguzi.”

Akizungumzia tukio hilo Mei 27, 2025, Rashid Mkamba, ambaye ni kaka mkubwa wa marehemu, baada ya tukio hilo askari walichukua mwili wa Mnette na kuupeleka hospitali kwa ajili ya vipimo.

“Tulipewa kibali na Serikali imekubali kugharimia gharama za mazishi na maiti imetolewa inaenda kuzikwa Kijiji cha Mtunga nyumbani kwa marehemu, ambapo magari kila kitu wanatumia ya kwao,” amesema.

Hata hivyo, Mkamba alidai baada ya kutokea kwa tukio hilo, kulitokea vurugu kutoka kwa wananchi wa Kibiti, ndipo walipochukua uamuzi wa kwenda kwa Mkuu wa Wilaya.

“Tulienda kwa mkuu wa wilaya kulalamika, tukihitaji kujua kama Serikali itahudumia gharama za msiba lakini marehemu anadaiwa madeni na ana familia yake ambayo imekuwa ikimtegemea,” alisema.

Baada ya kutoa malalamiko hayo, alisema Kanali Kolombo aliwajibu na kuagiza mwili huo ukazikwe, huku akiamuru waliosababisha wakamatwe pamoja na gari kwa ajili ya kupelekwa polisi.

Related Posts