Othman: Wazanzibari msifanye makosa Oktoba, chagueni  ACT-Wazalendo ikasimamie rasilimali

Unguja. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud amewataka Wazanzibari kutofanya makosa katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba kwa kuhakikisha wanakichagua chama hicho ili kikasimamie rasilimali zitakazowanufaisha watu wote.

Masoud ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema licha ya kisiwa hicho kubarikiwa rasilimali za kutosha bado baadhi ya wananchi wanakabiliwa na umaskini, hata wale waliomaliza vyuo wanakosa ajira, hivyo ACT imedhamiria kukomesha hali hiyo.

Ameeleza hayo leo Jumapili Juni Mosi,2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja Zantex, Jimbo la Mpendae, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

“Msifanye makosa Oktoba huu ni mwaka wa kuinusuru Zanzibar. ACT Wazalendo tutakwenda kuisafisha Zanzibar, tutapambana na vitendo vya ufisadi na rushwa, tunataka watu washiriki katika uchumi na kunufaika na rasilimali zilizopo.”

“Wazanzibari amkeni na tumieni wananchi  haki yenu ya msingi ya kuchagua viongozi bora katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu, chagueni watu sahihi watakaojali masilahi ya nchi na wananchi,” amesema Othman.

Katika mkutano huo, Othman amesema Jimbo la Mpendae, kama yalivyo majimbo mengi ya visiwa vya Zanzibar yana  vijana wengi wenye  ujuzi na fani  mbalimbali, ikiwemo ufundi magari na useremala lakini wanashindwa kuendelea au kubadilisha maisha yao kwa sababu ya kutowezeshwa.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo (Zanzibar), Ismail Jussa amedai kuwa ufisadi katika miradi ya Serikali unaonesha wazi kutokuwepo kwa uadilifu na misingi kwa watu waliopewa dhamana ya kuisimamia.

 “Hii inasababisha kila kukicha tunashuhudia ongezeko la kodi kwa wananchi wanyonge na matumizi holela yasiyokuwa na utaratibu mzuri wa kifedha,” amedai Jussa.

Related Posts