Sababu mkwamo biashara saa 24 Kariakoo huu hapa…

Dar es Salaam. Ruhusa ya Serikali kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa saa 24 Dar es Salaam imefanikiwa kwa biashara chache pekee, huku nyingi zikiendelea na utaratibu wa zamani, Mwananchi imebaini.

Dhamira ya Serikali kuruhusu hilo, imelenga kuimarisha uchumi wa mkoa, kuongeza mapato ya Serikali, kutoa fursa za ajira kwa wananchi, lakini kuifanya Dar es Salaam iwe na mfanano na majiji mengine yaliyoendelea na kuchangamka kibiashara.

Februari 25, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alizindua mpango huo katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wakuu wa wilaya zote na wakurugenzi wa halmashauri za jiji hilo.

Uchunguzi wa Mwananchi, maduka ya dawa, taasisi za fedha, baadhi ya hoteli, baa na ushushaji wa mizigo kutoka kwenye malori, ndizo shughuli pekee zinazofanywa kwa saa 24 sokoni Kariakoo.

Lakini, idadi kubwa ya maduka ya nguo, viatu, vifaa vya nyumbani, umeme na vitu vingine hufungwa kuanzia saa 12 jioni na mengine yakichelewa hadi saa tatu usiku, ikiwa ni tofauti na iliyotarajiwa.

Pia, katika baadhi ya mitaa hata taa zinazimwa kwa kile kinachoelezwa na wafanyabiashara kuwa, wanahofu kuibiwa na vibaka wanaozurura saa zote kuwachanganya walinzi.

Baadhi ya wafanyabiashara wamekosa imani ya kuwaachia wasaidizi wao droo za fedha waendelee kuuza usiku, ndio sababu wanalazimika kufunga, kama anavyoeleza Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Renatus Mlelwa.

Amesema jamii ilikuwa na matarajio makubwa maduka ya Kariakoo yangefunguliwa saa zote, jambo ambalo halitekelezeki kirahisi hasa kwa biashara za jumla.

“Wapo wafanyabiashara wanaofanya kazi na wake zao ni watu wanaoaminiana. Huwezi kumkuta mtu huyo anabadilisha droo au kumwachia mtu mwingine aendelee kuuza wakati wao wamepumzika hilo haliwezekani,” amesema Mlelwa.

Biashara nyingine za Kariakoo zinaendeshwa na ndugu na jamaa, hivyo mfumo wake hauendani na saa 24, isipokuwa baa na nyingine zinazohitajika kwa saa zote.

“Hata ukienda nje ya nchi, maduka makubwa ya jumla hufungwa usiku saa 12 jioni baada ya hapo kuna wafanyabiashara wadogo wanaingia mitaani kuuza hadi usiku,” amesema.

Amesema sehemu kama viwanja vya ndege pekee ndizo huduma hupatikana saa 24 kwa sababu ya mzunguko wa wasafiri tofauti na kwenye masoko yanayohusika na bidhaa za jumla.

“Kama ilivyo kwa wenzetu ikifika jioni maduka yanafungwa na kuruhusu wafanyabiashara wadogo, kwa hiyo tunaotaka huduma za jumla inabidi kulala na kusubiri asubuhi,” amesema.

Pia, amesema hata taarifa iliyokuwa imesambaa kwa nchi jirani ni biashara zitakuwa za saa 24 lakini wanapofika kwenye hoteli wanazofikia za Kariakoo hali ni tofauti, hivyo kusubiri hadi asubuhi.

“Wageni wanaokuja walitarajia kuona maduka yote yako wazi hadi saa nane usiku, lakini hali halisi ni tofauti. Hatuwezi kusukuma jambo hili kwa nguvu bila maandalizi na uhalisia wa mazingira ya biashara,” amesema.

Mlelwa amesema ingawa dhamira ya Serikali ni njema ya kupanua biashara, bado kuna haja ya kuzingatia mazingira halisi ya uendeshaji wa biashara katika maeneo kama Kariakoo.

Mmoja wa wafanyabiashara wa maduka ya nguo Kariakoo, James Mwakipesile amesema hawezi kufikiria kufanya kazi usiku kwa sababu ya umbali wa makazi yake pia kutokuwa na mtu wa kuaminika wa kumuachia maduka yake.

“Naishi Kibamba kutoka hapa hadi nyumbani ni safari ndefu, hivyo siwezi kumuachia mtu droo ya pesa wakati wa zamu ya usiku. Biashara ni fedha na huwezi kumpa mtu mzigo wa namna hiyo bila kuwa na uhakika naye kabisa hata kama ni ndugu yangu,” amesema Mwakipesile.

Amesema biashara ya saa 24 pia inahitaji kuajiri watu wengi kwa ajili ya kupeana zamu, hivyo wanapaswa kuwa na mtaji mkubwa utakaoendana na biashara anayoifanya.

Pia, amesema ni vigumu kufunga biashara mchana kwa ajili ya kufungua usiku ambako hakuna uhakika wa wateja kwani baadhi ya wateja wao kutoka nje ya nchi huwapigia simu na kuomba kufungiwa mzigo.

Kwa upande wa mama lishe, anayefanya biashara ya chakula Mtaa wa Uhuru na Sikukuu, Zena Mwenda amesema wanaokula chakula usiku kwao ni wale wanaolinda, wabeba mizigo ya usiku na wanaolala kwenye maduka.

 “Ukifika saa nne usiku, hata wateja wa kawaida hawapo. Huwezi kuandaa chakula saa saba usiku maana hakuna wateja wa kuamini, hivyo inabidi kupika chakula ambacho hakitazidi muda huo ili kisibaki,” amesema Zena.

Mfanyabiashara wa kigeni kutoka Zambia, Sasha Chanda amesema walipoona taarifa ya biashara ya muda wote waliona kuna unafuu kwa kuwa, sasa usafiri ni wa saa 24 lakini hali imekuwa tofauti.

“Tuliaminishwa kuna biashara muda wote, hata usiku lakini tulipofika tumekuta maduka yamefungwa,  hivyo inabidi kulala asubuhi tunaamkia kwenye maduka kabla ya kuwekwa tangazo la saa 24,” amesema Chanda.

Wamachinga nao wanalalamikia hali hiyo, wakieleza kuwa kuanzia saa nne usiku, mazingira ya biashara hubadilika na kuwa kimya kabisa.

Andrew Maganga, mfanyabiashara ndogondogo (machinga) amesema katika uhalisia biashara ya saa 24 ni ngumu kufanyika kwani wateja ndani ya mitaa hiyo hakuna na wanaopita ni wachache.

“Ukiangalia maduka na wamachinga wote wamefunga na mimi nafanya hivyo pia kwa kuwa hakuna wateja na hata sehemu tunayosimama tunategemea taa za kwenye maduka ambazo huzimwa na kuachwa za ndani,” amesema Maganga.

Omary Mtemvu, anayefanya biashara ya simu za mkononi Mtaa wa Msimbazi amesema hakujawahi kuwa na mabadiliko ya ufungaji wa maduka na ikiwa hivyo muhusika anakuwa kwenye miadi na mteja.

“Ukifika saa tano usiku, wateja ni wachache wanaokuwepo ni wapiti njia ambao wametoka kwenye shughuli zao za kila siku na muda huo ni wa watu wa usafi na magari yao wanasafisha mitaa,” amesema Mtemvu.

Mei 28, 2025 akijibu swali la mwandishi wa Mwananchi kuhusu saa 24 za Kariakoo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema biashara ya saa 24 inayotarajiwa kuimarika katika soko hilo na maeneo mengine ya jiji siyo utani, bali ni mnyororo wa kiuchumi unaotegemea teknolojia na mabadiliko ya fikra za Watanzania.

Alisema Bandari ya Dar es Salaam inapokea na kushusha mizigo usiku na mchana kutoka kwenye meli kupitia mitambo mikubwa ya kisasa, hivyo mnyororo wa usafirishaji na upokeaji wa mizigo unalazimika kufanya kazi saa zote.

“Meli zinakuja saa nane usiku, zinashusha mizigo. Je, nani atapokea mzigo huo? Tunahitaji madereva wa malori, wenye malori, wafanyakazi wa bandari, walinzi, waendeshaji wa ICD (maghala ya nje ya bandari), wote hawa wafanye kazi saa 24,” alisema Chalamila.

Akiweka wazi kuwa biashara ya saa 24 si ulevi wala fujo, bali ni mfumo mpya wa maisha ya kisasa, Chalamila alitoa wito kwa wananchi kuondoa dhana kuwa kufanya biashara usiku ni haramu au hatari, akisema huduma nyingi za afya na taasisi muhimu tayari zinafanya kazi saa 24.

Aidha, alisema Serikali haianzishi utaratibu mpya, bali inafungua fursa zilizopo kwa kutumia rasilimali zilizopo kama barabara, taa za barabarani, mitandao ya usafiri na usalama, huku akisisitiza kuwa hakuna maendeleo yatakayopatikana kwa kufunga maduka saa kumi na mbili jioni kila siku.

“Hatuanzishi kitu kipya, tunachofanya ni kutumia hali ya kimaumbile tuliyonayo mji unakuwa, watu wanaongezeka, fursa zinafunguka. Watanzania tunapaswa kujifunza kufanya kazi bila kujifungia kwenye mazoea,” alisema.

Chalamila alisema mfumo wa kufanya kazi saa 24 unahitaji ushirikiano wa sekta zote, ikiwamo polisi, mamlaka za usalama barabarani, mamlaka za afya, usafi wa mazingira na huduma za jamii, ili kuweka mazingira salama kwa wafanyabiashara na wateja.

Related Posts