Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiwa mbioni kuandaa mwongozo na sheria ya mtandao mmoja wa laini za simu ‘National Roaming’, Afrika imeweka makubaliano ya kuwa na matumizi ya mtandao mmoja ili kuingia kirahisi katika uchumi wa kidijitali.
Mtandao mmoja wa laini za simu, utamwezesha mtumiaji kupata mtandao eneo lolote atakalokuwa hata kama hakuna mnara wa laini anayotumia karibu.
Akizungumza wakati wa kufungwa kwa kongamano la 14 la Jukwaa la Utawala wa Mtandao Afrika (AfIGF), jana Jumamosi, Mei 31, 2025 Katibu Mkuu wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla amesema Tanzania imeanza kujiandaa.
” Tunaweka National Roaming ili mtumiaji aweze kupata mawasiliano popote alipo, hata kama mnara wa kampuni ya simu anayoitumia haupo. Tayari tunalifanyia kazi kwenye miongozo na sheria zetu.”
“Mtumiaji wa Vodacom akifika kijiji chenye mnara wa Halotel, ataendelea kupata huduma, kinyume na hali ya sasa ambapo mawasiliano hukatika iwapo hakuna mnara wa kampuni husika.
Mpango huo, ambao tayari umeanza kutekelezwa katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki, utawezesha pia kutumia laini hiyohiyo ya simu nchi jirani kama Uganda na Kenya,” amesema Abdullah.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akifunga kongamano la 14 la Jukwaa la Utawala wa Mtandao Afrika (AfIGF) Jana Jumamosi, Mei 31 katika ukumbi wa JNICC. Mkutano huo ulihudhuriwa na mawaziri wa wizara hizo barabla Afrika na wadau zaidi ya 1000 kutoka nchi hizo.
Amesema walichokubaliana kwenye kongamano hilo, kwa sababu Afrika imegawanyika kuna Kusini, Mashariki, Magharibi na Kaskazini na kwa kuwa Kanda nyingi zilishaanza kuungana.
“Kilichobaki ni kuungana ili kama mtu umetoka Tanzania, ukienda Afrika Kusini laini yako iwe ileile na asilimia kubwa tayari hilo linafanyika,” amesema Katibu Mkuu huyo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Usimamizi wa Internet kwa Tanzania, Dk Nazar Kilama amesema ili kuwezesha uchumi wa kidijiti kwa nchi za Afrika ni vizuri sasa kuwe na mwingiliano wa mawasiliano akitolea mfano mtumiaji akitoka Tanzania akaenda Benin atumie laini moja.
“Tukiwa na mtandao mmoja, hata kama uko Benin unafanya shughuli zako za kiuchumi, haina haja tena kuanza kuhangaika na kuanza kubadilisha fedha ndipo ununue Simcard nyingine.
“Inatakiwa ukiingia nchi yoyote ya Afrika uwe unatumia laini moja, kinachotakiwa ukiwa na visa card yako au debit card unaweza kununua mtandao ukaweka kwenye simu hiyo hiyo moja na ikafanya kazi ukiwa nchini humo na ukawasiliana popote,” amesema.
Amesema maazimio kama hayo yanaweza kusukuma uchumi binafsi wa Afrika na binafsi.
Washiriki wa jukwaa hilo kwa umoja wao wamesema, wanathamini mkataba wa kuasisiwa kwa Umoja wa Afrika na malengo ya Ajenda 2063, na kutoa maazimio yao.
Kwa pamoja wametoa tamko wanatambua Mkataba wa Kidijitali wa Afrika (ADC) unaoendana na Mkataba wa Kidijitali wa Dunia (GDC), umejikita katika kujenga Afrika yenye uwezo wa kidijitali, ambapo teknolojia inachochea ukuaji wa uchumi, ustawi wa kijamii na mustakabali wenye mafanikio kwa wote.
Wametangaza kwa pamoja dhamira yao ya kuimarisha mustakabali wa kidijitali wa Afrika kupitia utawala wa mtandao wa kidemokrasia, unaozingatia haki na kushirikisha wadau mbalimbali.
Wamesema ili kufanikisha hilo, wanajitolea kuandaa mpango kazi madhubuti unaoshughulikia changamoto kuu na kufungua fursa kwa ajili ya ukuaji endelevu wa kidijitali.
Katika hatua nyingine, wamesema wanatambua mafanikio yaliyopatikana kupitia mchakato wa WSIS huku pia, wakitambua changamoto zinazoendelea kuzuia ushiriki kamili wa Afrika katika uchumi wa kidijitali wa dunia.
Jukwaa limewezesha kujenga ushirikiano wa pamoja katika kuunda sera na mifumo ya kidijitali inayohudumia masilahi ya wote barani Afrika kwa ustawi bora wa huduma za intaneti.
Katika jukwaa hilo wataalamu wa masuala ya mtandao wamejadili kwa kina mada mbalimbali ikiwemo Akili Unde (AI) na teknolojia zinazoibuka, miundombinu ya umma ya kidijitali na usimamizi wa taarifa.
Kupitia majadiliano yao, walibainisha changamoto mbalimbali ikiwemo upande wa miundombinu na uunganishaji wa mtandao.
Wamesema, sehemu kubwa ya watu barani Afrika bado wameachwa nyuma kutokana na ukosefu wa mtandao mpana wa intaneti, gharama kubwa za data na upatikanaji mdogo wa njia fanisi za upitishaji mawasiliano kwa kasi.

Vilevile, wamesema kuna changamoto upande wa usimamizi wa rasilimali za mtandao huku wakibainisha kuwa, Kituo cha Taarifa cha Mtandao cha Afrika (AFRINIC) kinakumbwa na changamoto kubwa za kiutendaji na kiutawala.
Hali hiyo inachagizwa na kutokuwepo kwa uthabiti wa kifedha, migogoro ya uongozi na ukosefu wa uhakika wa kisheria, hali inayotishia usimamizi bora wa rasilimali za mtandao.
Wametaja changamoto zingine ni mifumo ya elimu kukosa ujumuishaji wa maarifa ya juu ya kidijitali kama vile akili unde (AI), taarifa kubwa na usalama wa mtandao na kwamba mitaala mingi ya shule haijajumuisha elimu ya Tehama katika ngazi ya msingi, jambo linalozuia watoto kupata ujuzi wa kidijitali mapema.
Wamesema uwepo wa mifumo dhaifu ya ulinzi wa taarifa na uwezo mdogo wa kiusalama mtandaoni, unaziweka nchi hatarini kwa uhalifu wa kimtandao, uvunjaji wa faragha ya taarifa na mashambulizi kwa miundombinu muhimu.
Aidha, wamesema kuna upungufu wa maudhui ya kidijitali yaliyo katika lugha za asili na yanayozingatia muktadha wa kitamaduni, ambapo unadhoofisha ujumuishaji wa kidijitali na uhifadhi wa urithi wa kitamaduni.
Katika eneo la utekelezaji, wameazimia
Kwa pamoja, kuanzisha mfumo wa Bara la Afrika wa kufuatilia na kutathmini maendeleo, wenye ripoti kila baada ya miaka miwili kwa Afrika IGF, ili kuhakikisha uwazi na maamuzi yanayotegemea ushahidi kamili.
Pia, wamekubali kuondoa pengo la kijinsia katika matumizi ya teknolojia, kukuza uongozi wa wanawake katika utawala wa mtandao, na kuwawezesha vijana wa Afrika kushiriki katika uundaji wa sera na suluhisho za kidijitali.