Kama ambavyo unapambana kuwaepusha watoto wako na mihadarati, ndivyo unavyotakiwa kukomaa kuhakikisha watoto wako wa kiume, hawavutiwi na tabia za aina mpya ya wanaume mjini, yaani wanaume chawa.
Chawa ni wanaume ambao wanajipatia kipato kwa kusifia wanaume wengine, tena kwa kusifia kwa kujidhalilisha.
Kwa mfano, kuna chawa mmoja wa kiume aliwahi kusema, kama angekuwa na uwezo wa kumzalia bosi wake, angemzalia watoto watatu. Mwanaume uliyakamilika unapata wapi nguvu ya kusema maneno kama hayo?
Kuna mambo mawili yanayonikwaza yaliyonisukuma kuwaongelea wanaume chawa leo. Kwanza, ama kwa kujua au kutojua, chawa wapo kwenye jitihada za kuufanya uchawa kuwa kitu cha kawaida.
Uchawa ukiwa kitu cha kawaida uanamume wetu utashuka thamani, kwani thamani ya mwanaume ipo kwenye ukomavu, sio lelemama, sio ulegeulege wa kusifia wanaume wengine.
Watoto wetu hawana cha kujifunza kutoka kwa chawa. Watoto wetu wa kiume wanahitaji mifano bora ya kuigwa wanaume wanaojituma, wanaowajibika, wanaojenga maisha yao kwa misingi ya heshima, juhudi, na maarifa.
Hatupaswi kuwaruhusu waamini kwamba njia ya mafanikio, ni kujipendekeza au kujishusha kwa kusifia wengine kwa tamaa ya kupata maslahi.
Hata ukiangalia historia utaona dunia inawakumbuka wanaume waliokomaa na kufanya vitu vikubwa duniani sio wanaume waliokuwa wanakesha kwa kuimba kuimba mapambio ya kuwasafia wanaume wengine. Hata wafalme na machifu walikuwa na waimba mapambio wao chawa wao, lakini umewahi kuwasikia hao chawa wakitajwa kokote kwenye historia?
Hapana, kwa sababu dunia haina muda na wanaume chawa, inawadharau, inawachukulia poa, inawashusha thamani.
Kitu kingine ambacho chawa wananikwanza ni tabia yao ya kudogesha elimu. Chawa wengi ni watu ambao hawajafanikiwa kupata elimu. Na kama unavyojua, mfumo wa dunia unapotafuta ajira, historia yako ya kielimu huhitajika.
Sasa kwa bahati mbaya dunia ipo kwenye changamoto za upungufu wa ajira, watu wengi wanatoka vyuoni lakini wanapoingia mtaani hakuna ajira hivyo wanajikuta maisha yao ni magumu.
Wakati huo, upande wa pili, chawa ambaye hajafanikiwa kupata elimu rasmi ya kueleweka, unakuta anajiingizia kipato kikubwa kutoka kwa mabosi zake. Chawa ana nyumba, ana magari, ana maisha mazuri.
Kwa sababu hiyo, chawa wamekuwa na kawaida ya kuwadhihaki watu waliosoma ambao wana maisha magumu wakiamini, walipoteza muda kusoma, vingereza vingi lakini pesa hawana.
Wanachosema ni kwamba, elimu haina maana ikiwa wao wameweza kujenga maisha bila kuwa nayo kupitia uchawa.
Watu wenye mitazamo kama hii ni hatari kwa ubongo wa watoto wetu wa kiume kuliko unavyodhani. Wanaweza kumlevya mtoto na kudhani kuwa mwanaume unayesifia wanaume wengine ndiyo ‘cheat code’ ya maisha. Utasifia na kuomba hela, utajenga, utanunua chakula nyumbani, utapeleka watoto shule nzuri.
Tunatakiwa kuwakuza watoto wetu wawe wanaume wa kweli, wanaotambua thamani yao, wanaojenga ndoto zao kwa misingi imara.
Tuwafundishe kuwa thamani yao haipo kwenye maneno ya kujipendekeza, bali ipo kwenye bidii, nidhamu, na uwezo wao wa kusimama imara hata kwenye mazingira magumu. Uchawa si njia, ni mtego wa kupoteza utu.