Fedha zavuruga vigogo serikalini | Mwananchi

Dar es Salaam. Kuna nini bungeni? Ni swali linaloakisi hisia za watu wengi wanaoshangazwa na wimbi la Watanzania wanaojitokeza kuwania ubunge katika chaguzi za miaka ya karibuni.

Ugumu wa swali hilo, unatokana na kwamba, ubunge umekuwa ndoto sio tu za wasio na ajira, bali hata viongozi wakiwamo wakuu wa mikoa, wilaya na wakuu wa taasisi za umma na binafsi.

Fikiria wadhifa wa mkuu wa mkoa anayepewa usafiri, makazi, ulinzi na mamlaka nyingine lukuki, kadhalika eneo lake la utawala linaweza kumeza wabunge takribani watatu, lakini anakuwa tayari kuiacha nafasi hiyo na kwenda kugombea ubunge.

Mathalan, kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pekee, jumla ya makada 10,367 walijitokeza kuwania nafasi 358 za ubunge wa majimbo na viti maalumu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Wimbi la Watanzania kuzisaka nafasi hizo, linahusishwa na ukubwa wa masilahi kwa maana mshahara, marupurupu, posho za vikao na kiinua mgongo wanavyopata wabunge, kama inavyofafanuliwa na wataalamu wa uongozi na wadau wa wanasiasa.

Ukiacha wenye mtazamo huo, wapo wanaosema watu wanaacha nafasi na taaluma zao kwenda kugombea ubunge, wakitarajia wateuliwe kuwa mawaziri, huku wengine wanaona ubunge ni kazi huru inayokupa nafasi ya kuamua nini cha kufanya na muda wa kufanya bila kusimamiwa na kushurutishwa.

Ndani ya vyama tayari kumekuwa na wimbi la watu kujitokeza kuwania ubunge huku CCM ikitangaza kuanzia Juni 28 dirisha la kuchukua fomu litafunguliwa.

Rais Samia Suluhu Hassan alisema tayari watumishi serikalini wamekwisha wasilisha majina yao.

Wakati wa mkutano mkuu wa CCM uliofanyika Mei 29 na 30, 2025 Rais Samia alimwagiza katibu mkuu wa chama hicho ifikapo leo Juni mosi, 2025 apate majina ya wale wote wanaotaka kuwaia upande wa CCM ili wanaobaki wapate mafunzo.

“Ili tuwe na uchujaji wenye haki na uadilifu, wale walioko kwenye vikao vya uchujaji, ambao wenye nia ya kugombea watoe taarifa mapema watupishe, upande wa Serikali tulikwisha kupata majina mapema bado CCM,” amesema Rais Samia.

Mmoja wa kigogo serikalini aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutokutajwa jina amesema: “Kuna kundi kubwa la watumishi serikalini wanakwenda kugombea ubunge. Subiri utaona wakati ukifika hasa kule CCM utawaoa. Lakini ni fursa kwa wengine kwani wakitoka, wanaingia wengine kwenye nafasi zao.”

Akizungumzia hilo, aliyekuwa Waziri Mkuu (1995-2005), Frederick Sumaye amesema masilahi makubwa yanayotokana na nafasi ya ubunge ukilinganisha na nyingine, ndiyo sababu ya watu wengi kukimbilia wadhifa huo.

“Uwe Profesa wa chuo kikuu au uwe mkurugenzi wa taasisi ya umma au nafasi yoyote ambayo ni nje ya hizo, masilahi ya wabunge ni makubwa. Kwa hiyo watu wanaona kwamba inalipa kwenda bungeni ndiyo maana mtu anakuwa tayari kuacha kazi ya uteuzi anakwenda bungeni,” amesema.

Sumaye ametolea mfano ukuu wa mkoa na wilaya, akisema ni nafasi kubwa kiutawala kuliko ubunge, lakini watu wako tayari kuziacha kwa ajili ya kuwa wabunge.

Ukiacha masilahi makubwa, mwanasiasa huyo wa zamani amesema wimbi lingine la watu kuutaka ubunge, linachochewa na dhana kuwa watakapochaguliwa, wanakuwa karibu kuteuliwa kuwa mawaziri.

Amesema hilo linatokea zaidi kwa wataalamu na wanazuoni, ndiyo maana wengi wanatoka vyuo vikuu wanakwenda kugombea, wakitarajia kushinda na baadaye wateuliwe kuwa mawaziri.

Kingine kinachosababisha wengi waukimbilie ubunge, Sumaye aliyekuwa mbunge wa Hanang mkoani Manyara amesema ni kukosekana udhibiti katika kazi ya ubunge, akifafanua hayupo anayekusimamia muda wa kuingia na kutoka kazini.

“Kazi ya mbunge haina udhibiti mwingi, hayupo anayekwambia saa mbili uwe ofisini au asubuhi ukichelewa mstari utapigwa. Ni kazi unayoweza kwenda ofisini saa nne, unaweza usiende ukaenda kwenye shughuli zako binafsi. Ni kazi ambayo watu wanaona ina masilahi mazuri lakini haina pressure,” amesema.

Sumaye amesema si jambo la kufurahia kama Taifa inapoonekana watu wengi wakiwamo viongozi wa taasisi za umma, wanataaluma wanakimbilia ubunge.

Hoja yake hiyo, inatokana na kile alichofafanua kuwa, kama wataalamu wengi waliobobea katika fani mbalimbali watakimbilia bungeni nchi itatengeneza mapengo na hasara katika sekta muhimu.

Kwa mtazamo wa Sumaye, iwapo masilahi ya mbunge yatalingana na kada nyingine, hakutakuwa na wimbi kubwa la wanaokimbilia nafasi hizo kama inavyoshuhudiwa sasa.

“Naamini kwamba kama masilahi yatalingana na kada nyingine zinazofanana, hiyo itapunguza wimbi la kila mtu kutaka kuwa mbunge. Mimi naamini hicho ndicho kipengele muhimu,” amesema.

Uwaziri usitokane na ubunge

Sambamba na hilo, amependekeza uwekwe utaratibu utakaofanya mawaziri wasitokane na wabunge kama ilivyowahi kupendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

“Ukiwa mbunge unakuwa chini ya muhimili wa Bunge na majukumu yako, kiukweli mawaziri wako kwenye nguzo ya utendaji, lakini akiwa waziri yuko serikalini, akiwa upande wa ubunge yuko kwenye Bunge au legislature sasa hizi ni nguzo dola ina nguzo tatu,” amesema.

“Serikali, Bunge na Mahakama ni mihimili ambayo kila mmoja unajitegemea. Unaporuhusu mbunge kuwa waziri maana yake unaruhusu mtu mmoja atumikie mihimili miwili kwa sababu waziri anaitumikia Serikali.

“Bunge kazi yake ni kuishauri na kuisimamia Serikali, unaporuhusu mbunge awe waziri inakuwa vigumu wewe mwenyewe ujisimamie na kujishauri, kwa hiyo kunakuwa na mgongano mkubwa,” amesema.

Kwa mujibu wa Sumaye, eneo hilo lina utata ndiyo maana ni muhimu kutenganisha uwaziri na ubunge na kuwepo utaratibu utakaofanya anayeteuliwa kuwa waziri asiwe mbunge.

“Najua hili eneo halipendwi. Tume ya Jaji Warioba ililiweka sawa lakini lilipigwa chini kwa sababu wanaojadili ndio hao wanaofaidika kwa kuwa kwenye nafasi hizo,” amesema.

Mkurugenzi wa Mikakati na Mafunzo wa Twaweza East Afrika, Dk Baruani Mshale amesema inawalazimu wengi kuutaka ubunge, kwa sababu ndiyo wadhifa unaoonekana kuwa miongoni mwa fursa kubwa za kujikwamua kimaisha.

Mshale ambaye pia ni mkufunzi wa masuala ya uongozi, amesema kwa uhalisia ubunge haikupaswa kuwa nafasi ya mtu kujineemesha, badala yake iwe ya kujitolea.

“Haikupaswa kuwa nafasi ya mtu kujitengeneza ukwasi, kupata fedha, kuwa tajiri, ilitakiwa iwe nafasi ambayo unajitolea kwa niaba ya wananchi wenzako,” amesema.

Kadri siku zinavyokwenda, Dk Baruani amesema watu wanazidi kuona ubunge ni njia fupi ya kujinufaisha kutokana na utitiri wa marupurupu, kiinua mgongo, posho za vikao, bima za madaraja ya juu, mishahara na udhamini wa mikopo mikubwa.

Amesema mazingira hayo yamewafanya watu wavutiwe na nafasi hiyo, ukizingatia si rahisi kupata kiasi kama hicho cha fedha kwa haraka kama utaamua kukitafuta kupitia shughuli nyingine.

Dk Baruani amesema wimbi lingine la wanaoutaka ubunge, linatokana na kujiweka karibu na mamlaka ili ipatikane nafuu ya tozo, kodi zinazohusiana na shughuli zao na aghalabu hii huwa kwa wafanyabiashara.

“Wapo wanaoingia kwenye ubunge ili mambo yao yawanyookee, kama biashara yake imwendee vizuri asisumbuliwe, asibughudhiwe na tozo mbalimbali na vyombo vingine,” alisema.

Ameeleza kuwa, wapo wanaoingia wakiwa na nia ya dhati ya kwenda kufanya mabadiliko, lakini wapo wale wanaofanya hivyo wakiamini kuwa karibu na Serikali, kutawanyooshea mambo yao.

Pamoja na kuwepo kwa makundi hayo, Dk Baruani amesema  iwapo wanaoutaka ubunge wakawe sehemu ya mabadiliko ya sheria zinazoonekana kukwaza shughuli fulani na hiyo aghalafu hufanywa na wafanyabiashara.

“Mtu anaweza akasema kwa kuwa yeye ana uzoefu wa kufanya biashara na hapendezeshwi na uamuzi ambayo mara nyingi unafanywa, anaamua kuingia katika vyombo vya maamuzi ili ashawishi uamuzi utakaolinda maslahi kama yeye,” amesema.

Hoja ya ukubwa wa masilahi katika ubunge, inapingwa na mbunge wa zamani wa Kibakwe, Isack Kamwelwe anayesema watu wanadhani kuna fedha nyingi unapokuwa Mbunge, lakini uhalisia ni kinyume chake.

Alisema imebaki ikiaminiwa hivyo, kwa sababu hata wanaoingia kwenye ubunge, hawakuwahi kuweka wazi uhalisia wa maslahi yaliyopo, wanaumia kimyakimya.

“Wanadhani kwenye ubunge kuna hela kwa sababu hata wanaoingia kwenye ubunge wakikutana na shida hawasemi kwa hiyo haijulikani kukoje.

“Mtu anakuja anaacha kazi anaingia kwenye ubunge, sisi huwa tunawahoji umeacha kazi umekuja kwenye ubunge hali ikoje, anakuonyesha kujutia,” amesema.

Ili kuthibitisha hilo, amesema ni vema kuangalia maisha ya wanasiasa waliostaafu ubunge wanaishije.

Kwa upande wa vijana, amesema wengi wanajikuta katika rada za kuutaka ubunge kutokana na changamoto ya ajira na kwamba wanaona moja ya ajira ni ubunge.

Lakini wengine, amesema wanaingia kwenye vyama kwa malengo ya baadaye ikiwamo kuwa wabunge.

Kiu ya kubadilisha maisha ya nyumbani

Mbunge wa Masasi Mjini (CCM), Geoffrey Mwambe ni miongoni mwa waliowahi kuwa watumishi wa umma, akitoka kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na baadaye akaondoka na kwenda kugombea ubunge.

Katika hoja yake kuhusu kwa nini watu wengi wanaukimbilia ubunge, amesema nafasi hiyo ni uwakilishi wa wananchi, wakati utumishi wa umma ni ajira kwa ajili ya aliyekuajiri.

Amesema wengi wanalazimika kugombea ubunge baada ya kuguswa na jamii ya nyumbani kwao, wakiona ili kuwe na mabadiliko na matokeo chanya, atalazimika akawe sehemu ya uongozi.

“Kwa sababu anajua anapokuwa mkurugenzi wa taasisi ya umma, pengine hawi na mchango wa moja kwa moja wa kubadilisha jamii ya kwao. Wengi tumekulia vijijini tunatamani maisha ya kijijini kwetu yabadilike na tunatamani tungetumia uzoefu wetu kuhakikisha angalau maisha ya kwetu yanabadilika,” amesema.

Sambamba na hilo, amesema anaona uongozi ni wito na karama ya kutaka kuwatumikia watu, unapoiongoza taasisi au mkoa unajikuta unatamani kufanya zaidi ndipo mtu anapogombea ubunge.

Sababu nyingine, amesema unapokuwa mkuu wa taasisi umma unakuwa na kiu ya kuchangia na kushiriki kuboresha sera au sheria zinazoigusa taasisi yako, hakuna nafasi nyingine itakayokupa fursa hiyo zaidi ya ubunge.

“Unapokuwa mkurugenzi unakuwa na mamlaka ya kushauri na sio kutunga na kupitisha. Unawiwa badala ya kusimamia taasisi, sasa unatanua wigo na kupata nafasi ya kutunga sheria na sera,” amesema.

Related Posts