Arusha. Jaji Modibo Sacko wa Jamhuri ya Mali amefanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) akirithi mikoba ya Mtanzania Jaji Imani Daud Aboud aliyemaliza muda wake.
Jaji Sacko alikuwa Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo mwaka 2023, akiwa chini ya jaji Aboud, aliyehudumu kwa miaka minne katika chombo hicho kikuu cha haki barani Afrika.
Jaji Sacko ametangazwa baada ya uchaguzi ulifanyika leo Juni 2, 2025 jijini Arusha, Tanzania, katika kikao cha 77 cha kawaida cha Mahakama hiyo, ambapo majaji 11 walipiga kura ya siri kuchagua viongozi wapya.
Katika uchaguzi huo, Jaji Bensaoula Chafika wa Algeria amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Mahakama hiyo iliyokuwa inashikiliwa na Jaji Sacko.
Akizunguza nje ya Mahakama hiyo, jaji Aboud amesema kuwa anajivunia kwa kiasi kikubwa kuongoza mahakama hiyo kwa misimu miwili akiacha mafanikio mengi ikiwemo kuanzisha siku maalumu ya Mahakama.
“Changamoto kubwa ni nchi zetu za Afrika kutekeleza azimio la uanzishwaji wa Mahakama hii kubwa ya haki ikiwemo hukumu zinazotolewa,” amesema.
Katika hilo amezitaka nchi za Afrika kuhakikisha zinatekeleza hukumu hizo ili kuleta thamani halisi ya uanzishwaji wa taasisi hiyo ya juu ya haki za binadamu.
Naye jaji Sacko amesema kuwa amepokea kijiti hicho huku kukiwa na ukiukwaji mkubwa wa hali za binadamu na watu katika baadhi ya nchi za Afrika.
“Nitahakikisha nawasiliana na viongozi wa juu wa nchi hizo na mamlaka za haki Ili kupunguza ukiukwaji huu wa hali za binadamu katika nchi zetu, na kuongeza thamani ya taasisi hii ya haki” amesema.