Dar es Salaam. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limetangaza kuanza ujenzi wa kituo kipya cha watoto wenye usonji katika eneo la Kitopeni Bagamoyo mkoani Pwani.
Usonji, au Autism Spectrum Disorder (ASD) ni hali ya ukuaji wa ubongo inayojumuisha changamoto katika maeneo ya mwingiliano wa kijamii, mawasiliano na tabia zinazojirudia. Hali hii inahitaji uangalizi maalumu na msaada kutoka kwa wataalamu ili kusaidia watu wenye ugonjwa huu kufikia uwezo wao kamili.
Dalili za ugonjwa huo mara nyingi huanza kujitokeza katika umri wa miaka miwili hadi mitatu.
Akizungumza leo Jumatatu, Juni 2, 2025 Naibu Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Wilbroad Mastai katika Kanisa la Azania Front lililopo Posta jijini Dar es Salaam, amesema watoto wenye changamoto hiyo wanahitaji kuwa katika uangalizi maalumu.
Hivyo Kanisa limeamua kuja na mradi wa ujenzi wa kituo hicho kitakachogharimu jumla ya Sh6 bilioni ambacho kitaanza ujenzi kwa awamu ya kwanza utakaotumia miezi 10 ambapo kikikamilika kitahudumia watoto kati ya 700 hadi 1,000 wakiwamo 100 wa elimu ya ufundi.
Akinukuu twakimu za Wizara ya Afya, Mchungaji Mastai amesema takriban watoto 22,000 kila mwaka wanazaliwa wakiwa na usonji. Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002 watoto 1,700,000 walikuwa na ulemavu wa aina mbalimbali huku asilimia 19 wakiwa na ulemavu wa akili.
“Kutokana na mabadiliko ya tabianchi na uchakavu wa miundombinu uongozi wa kanisa umelazimika kuja na mpango wa ujenzi wa kituo kipya kitakachozingatia viwango vya kimataifa eneo la Kitopeni Bagamoyo,” amesema.
Hadi sasa michakato ya kuelekea utekelezaji wa mpango kama vile usanifu wa majengo hitajika hatua ya kushirikiana na wanasaikolojia imekamilika kwa sehemu na vingine vinaendelea.
Kutokana na hilo, Kanisa linatoa wito kwa wahisani kukutana katika siku ya kilele cha harambee itakayofanyika Alhamisi ya Juni 5, 2025 ukumbi wa Diamond Jubilee ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Hata hivyo amesema michango imeanza tayari kutolewa tangu Februari mwaka huu kwa ufanisi kutoka kwa kanisa na wadau wengine.
“unawakaribisha wahisani tuliowaalika shughuli hili ni endelevu na siyo ya kidini wananchi wote wanakaribishwa kuchangia ujenzi wa kituo hiki,” amesema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya changizo na itifaki ya ujenzi, Mchungaji Eliona Kimaro amepongeza wazo la ujenzi wa kituo hicho kwa kuona umuhimu wa kuwahudumia watoto hao wenye uhitaji maalumu.
Mchungaji Kimaro ametoa wito kwa wazazi kutowaficha ndani watoto wenye matatizo hayo, kwani wana uwezo wa ujuzi ambao utawasaidia maishani.
“Baadhi ya wazazi wanawaficha ndani watoto hawa, wanapaswa kutambua wana uwezo binafsi ikiwemo ujuzi utakaowasaidia kwenye maisha yao kitaaluma wajitegemee,” amesema.
Ameongeza kwamba kituo hicho chenye eneo la hekari 30 kitatumika kuwalea watoto wakati ambao wazazi wao wanaendelea na majukumu mengine ya kujenga Taifa.