Dar es Salaam. Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2025/26 inawaslishwa leo Jumatatu, Juni 2, 2025 bungeni, huku macho ya Watanzania yakisubiri kuona Serikali inakuja na mikakati gani kuhakikisha inapambana na kuondoka kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) nchini ambayo imefadhili sekta hiyo kwa miaka mingi.
Ufadhili wa USAID ulisaidia maeneo mengi, ikiwamo kuajiri watumishi wa afya, afua mbalimbali za afya zilizotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya na Tamisemi lakini pia wadau wa asasi za kiraia na mashirika.
Mei 13, 2024 Bunge la Tanzania liliidhinisha Sh1.31 trilioni huku ikianisha vipaumbele 10 vitakavyotekelezwa kwa mwaka 2024/25 kupitia bajeti hiyo, bajeti iliyoongezeka kutoka Sh1.235 trilioni kwa mwaka 2023/24.
Hoja zinazosubiriwa na Watanzania ni utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote (UHC), upungufu wa watumishi katika sekta ya afya baada ya kuondoka kwa USAID, afya ya akili na suluhu ya malalamiko ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).
Tamko la Sera ya Afya ya Mwaka 2007, linataka uwepo kwa watumishi wa kutosha wenye ujuzi katika taaluma mbalimbali katika ngazi zote za kutolea huduma nchini.
Katika malalamiko ya NHIF, kumekuwa na mvutano unaokabili uendeshaji wa mfuko huo na sekta binafsi ya afya pamoja na vituo vya umma.
Hoja nyingine inayosubiriwa katika bajeti hiyo, ni uhakika wa upatikanaji wa dawa za miradi misonge ikiwamo zile za wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), kwa kuwa kumekuwa na tetesi nyingi za upatikanaji wake kwa sasa.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema kujua hatma ya afya za afya, watumishi, uhakika wa dawa ndiyo kubwa zaidi, hasa katika wakati huu ambao ufadhili wa USAID umeondoka.
“Sote tunasubiri kwa hamu kusikia mipango. Tunadhani bajeti itaziba nakisi ya bajeti baada ya Marekani kupunguza misaada, wengi wanatarajia kuona mipango itakayofanya waone mustakabali wa afya zao,” amesema Dk Mugisha.
Amesema Watanzania wanataka waone mikakati ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko, yasiyoyakuambukizwa na ya ajali.
Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige amesema hana uhakika kama bajeti ya Wizara ya Afya imefikia asilimia 15 ya matumizi ya Serikali, kwa maana hiyo ilikuwepo tangu makubaliano ya Abuja kwamba angalau nchi itumie asilimilia 15 ya mapato yake kwa ajili ya afya.
Pili amesema maendeleo yanayofanywa siku zote, lazima yalenge kule kwenye fungu la idadi ya watu wanaoathirika zaidi kuliko wengine.
“Kwa mfano watoto wadogo chini ya miaka mitano na wajawazito, bado kuna tatizo katika maeneo ambayo yanalima vyakula kwa wingi, lakini bado yana watoto wenye udumavu. Ukichukua maeneo kama Katavi, Njombe, Iringa, vyakula vinavyolimwa vingi vinauzwa lakini udumavu ni mkubwa, ilipaswa lielekezwe kwenye jamii,”amesema Dk Mzige.
Dk Mzige amesema ni muhimu kuwaambia kinamama au kinababa kuhusu afya za watoto. Umuhimu wa ulaji wa mboga za majani na matunda.
Amesema muhimu kuikumbusha jamii kusafisha kinywa mara mbili kwa siku kuepuka uvutaji wa sigara, na kwmaba elimu hiyo ianzie mashuleni.
Mdau mwingine wa masuala ya afya ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema bima ya afya haikuwa imepangwa vizuri tangu imeanza kwani ilijikita zaidi kutibu na si kukinga.
“Kama kuna ugonjwa una gharama kubwa ni usafishaji wa figo kisukari na presha, wanufaika hawaelimishwi nini cha kufanya wanakuja wakiwa wameugua,” amesema mmoja wa watumishi waliopo katika hospitali za umma.
“Bajeti haijawahi kutenga uwepo wa wataalamu hawa maeneo ya wilayani, hakuna uwiano kati ya Tamisemi na Wizara ya Afya, mgonjwa atoke kilomita 90 kwenda mkoani na kama amezidiwa anakufa njiani kabla hajafika hospitalini.
“Ambulensi zinabeba wagonjwa wengi zinatumia mafuta na zinanunuliwa ghali, ukitazama mshahara wa dereva na gharama ya ghali namafuta, fedha zinazidi angeajiriwa daktari bingwa wilayani.”
Mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, Hafidh Omary amesema Serikali imefanya ununuzi wa vifaa ambavyo ni vingi visivyo na idadi na mwelekeo mzuri.
“MRI inauzwa bilioni mbili waweza ajiri madaktari 199 kwa mwaka na ukawalipa vizuri, kifaa na mtu ni vitu viwili tofauti huwezi kutoa gari bila dereva,” amesema.
Mfanyabiashara wa soko la samaki Feri jijini Dar es Salaam, Hawa Mwinjuma amesema tatizo la ajali hapa nchini ni kubwa hivyo lazima bajeti iangalie namna ya kuzipunguza, huku akichochea nchi kulima zaidi tumbaku ambayo ina athari.
“Tanzania tunaongozwa kwa kulima tumbaku, nadhani wakati wizara zingine zinaihesabu kama inaingiza kipato, tuangalie wagonjwa wanavyoongezeka. Pia kinamama tuwekewe huduma muhimu kule kijijini kwetu Mtwara huko hali si nzuri hatuna hata daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama lazima umfuate mbali,” amesema Hawa.