Othman: Haijalishi tumeumizwa kiasi gani, tutaingia kwenye uchaguzi

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud amesema haijalishi wamepitia magumu kwa kiasi gani kipindi kilichopita, lakini kamwe hawatasusia uchaguzi licha ya kuwapo dalili za kutaka kuwakatisha tamaa.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema kwa namna yoyote itakavyokuwa watahakikisha wanapigania mifumo kabla ya uchaguzi lakini wasitarajie kwamba chama hicho kitasusia katika visiwa hivyo, huku akiomba wananchi kuunga mkono chama hicho.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa jimbo la Mpendae Mkoa wa Mjini Magharibi Juni mosi, 2025 ambapo amekumbushia madhila ambayo yametokea katika chaguzi zilizopita, huku akiwataka wananchi kukiunga mkono chama hicho ili kuleta mabadiliko ya kweli katika visiwa hivyo.

“Tuna maumivu ya kupoteza ndugu zetu 21, tumebaki na vizuka (wajane) 18, watu zaidi ya 48 wamepata ulemavu na tumewauguza kwa kipindi kirefu na watu wengine zaidi ya 1,000 wamejeruhiwa kwa sababu ya uchaguzi,” amedai Othman na kuongeza.

“Haijalishi madhila tuliyopitia lakini niwaambie ndugu zangu tunakwenda kwenye uchaguzi kama itakavyokuwa, lakini tutahakikisha tunapigania mabadiliko ya mifumo kabla ya kuingia kwenye uchaguzi,” amesema.

Amesema lengo la chama hicho ni kutaka kuleta mabadiliko ya mifumo, watendaji kuwajibika na kubadilisha maisha ya wananchi kwani kwa rasilimali zilizopo, Zanzibar haipaswi kuwa maskini, “lazima tufike pahala rasilimali zilizopo ziwanufaishe wananchi wenyewe na sio masilahi binafsi

“Kwa maendeleo yaliyopo Zanzibar kwa karne nyingi nyuma, ni ajabu kuona bado vijana wanateseka na ugumu wa maisha na badala yake hata taasisi zinategemewa ziwaajiri, Serikali inazikodisha kwa watu binafsi tena kutoka nje ya Zanzibar kwa kutumia kivuli cha uwekezaji,” amesema.

Pia, amewataka wananchi kuamka na kutumia haki yao ya kuchagua viongozi bora katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ili kupata uongozi utakaowajali katika maisha yao.

Naye Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo upande wa Zanzibar, Ismail Jussa, amesema imebaki miezi michache kufikia uchaguzi mkuu na wakati huu watahakikisha wanapigania haki zao kwa namna yoyote ile.

Amesema iwapo wakiingia madarakani watahakikisha wanafumua mikataba yote iliyoingiwa na Serikali iliyopo madarakani, kwani mingi haina dhamira njema kwa nchi.

“Kuna fedha nyingi zinazoweza kuleta maendeleo hapa Zanzibar lakini mifumo haipo sawa,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho upande wa Zanzibar, Omar Ali Shehe amesema uchaguzi mkuu ni mchakato ambao unaanzia kwenye uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu ka wapigakura, na kuitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuzingatia haki kwa wote.

Amesema licha ya ZEC kuweka kiwango kikubwa cha pingamizi kwa wananchi wasio na sifa kuwa kwenye daftari ili kuwakatisha tamaa washindwe kuwapinga mapandikizi, lakini jambo hilo halitawarejesha nyuma.

ZEC imeweka Sh50,000 ya pingamizi kwa wananchi ambao hawana sifa za kuwa kwenye daftari, awali ilikuwa Sh5,000.

Hata hivyo Mkurugenzi wa ZEC, Thabit Idarous Faina amewahi kulitolea ufafanuzi kwamba wameweka kiwango hicho kwa sababu ya kuepusha pingamizi ambazo hazina sababu kutokana na kiwango kidogo cha fedha.

Related Posts