Sababu daraja la Tanzanite kutumiwa bure

Dodoma. Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Dk Oscar Kikoyo ameitaka Serikali kuanza kutoza fedha kwa watumiaji wa daraja la Tanzanite kama ilivyo kwa la Mwalimu Julius Nyerere.

Dk Kikoyo amesema hayo bungeni leo Jumatatu Juni 2,2025 alipouliza swali la nyongeza ambapo amehoji kwa nini watumiaji wa daraja la Tanzanite wana uwezo lakini hawalipi, wakati daraja la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni jijini humo wanalipa ingawa watumiaji wengine ni watu wa kipato chini.

Katika swali la msingi, mbunge huyo ameuliza kwa nini watumiaji wa Daraja la Mwalimu Julius Nyerere wanalipia kila wanapopita huku watumiaji wa Daraja la Tanzanite hawalipi.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema watumiaji wa Daraja la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wanalipia kila wanapopita kwa sababu limejengwa kwa utaratibu wa ubia, yaani Public Private Partnership (PPP) ambapo mwekezaji hurudisha fedha alizowekeza.

Naibu Waziri amesema kwa upande wa Daraja la Tanzanite watumiaji hawalipi kwa sababu limejengwa kwa utaratibu wa kawaida kama uliotumika kujenga madaraja mengine nchini.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesema wanayafanyia kazi maoni ya wadau na wabunge ili ikibidi baadhi ya madaraja makubwa yote yaanze kutozwa malipo.

Related Posts