Dar es Salaam. Serikali kwa kushirikiana na wadau imeanzisha mfumo wa kuimarisha ukusanyaji wa takwimu za vizazi na vifo, zitakazounganishwa na mifumo mingine ya Serikali ili isomane.
Akizungumza leo Jumatatu, Juni 2, 2025 katika ufunguzi wa mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Serikali inachokikusudia katika mfumo huo ni kutambua idadi ya wanaofariki dunia na kwanini wanafariki.
“Tutakapojua kwanini maana yake itatusaidia kuweza kuchukua hatua za kitabibu na kuwekeza nguvu nyingi kwenye kitu kinachosababisha vifo,” amesema.
Amesema katika jamii ya Tanzania bado hakujawa na teknolojia nzuri inayosaidia kupata takwimu za kila kifo kutoka ngazi ya chini.
“Ni muhimu kupata takwimu hizi zitakazosaidia Taifa kuwekeza ili mwisho wa siku kitu kinachoitwa umadhubuti wa rasilimali za Taifa katika kukuza, kustawisha maendeleo,”amesema Chalamila.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk Honorati Masanja amesema Ifakara wanashirikiana na Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Wizara ya Afya.
Amesema wamekuwa wakitekeleza mpango wa SRS, afua ambayo inalenga kuimarisha ukusanyaji wa takwimu za vizazi na vifo, zinazounganishwa na mifumo mingine ya serikali ikiwamo Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).
Amesema wanatafiti namna gani wanaweza kuboresha huo upungufu.
“Kama kizazi lazima kisajiliwe na akifariki taarifa zake zisajiliwe na tujue amefariki kwa sababu gani hiyo itatusaidia, ni namna gani tuweze kuelekeza nguvu kwenye magonjwa yapi katika kukinga.”
Dk Masanja amesema kuna changamoto ya mifumo kutosomana, “Unakuta hata ndani ya wizara tu wana taarifa zao na kwingine mifumo haijasomana, taarifa za vifo kutoka polisi zinaenda wapi? Zinawafikiaje wizara na mifumo hiyohiyo tunaiboresha iweze kusomana.”
Amesema katika utekelezaji wa mfumo huo, wanakwenda katika jamii ili kujua kwa nini watu wanakufa na kuja na takwimu sahihi.
“Mkutano huu umewaleta wadau mbalimbali wa nchi nane wanaofanya kitu kinachofanana na sisi ni mpango unaofadhiliwa na Gates Foundation, leo tunaangalia tumefikia wapi katika hatua ya kwanza ya kufanya tathmini ya mifumo yetu ya ukusanyaji wa taarifa za vifo katika ngazi ya jamii na sehemu zingine kama hospitali,” amesema.
Amesema wataangalia namna takwimu zinavyoweza kuwa zinaunganishwa na taarifa zingine kwa kufuata maagizo ya Serikali ya mifumo kusomana kwani kuna maeneo taarifa za vizazi na vifo hazifiki inavyotakiwa na kwa wakati.
Makamu wa Rais kutoka CVRS Improvement, Profesa Phillip Setel amesema jinsi ya kugundua ni sababu gani halisi ya vifo kutoka kwa jamii yenyewe ni jambo gumu kidogo, hivyo wapo katika hatua za kuchunguza na kudhibitisha na kuleta habari halisi kwa watunga sera za afya na jamii kuboresha afya ya wote.
“Watu wengi wanaumwa magonjwa tofauti hasa ya kuambukiza malaria, VVU, Kifua Kikuu na sasa tuna magonjwa yasiyoambukiza, tunataka kwenda katika jamii na kujua kwanini watu wanakufa na kuja na takwimu sahihi,” amesema Profesa Setel.