Serikali yalifuta Kanisa la Askofu Gwajima, yeye asema…

Dar es Salaam. Serikali imetangaza kulifuta Kanisa la Ufufuo na Uzima, linalomilikiwa na Askofu Josephat Gwajima, ikiwa ni siku moja tangu kiongozi huyo wa kiroho atangaze msimamo wake wa kuendelea kukemea vitendo vya utekaji na watu kupotea.

Sababu ya uamuzi huo wa Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ni kile kilichoelezwa kanisa hilo limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Mzizi wa hayo ni mkutano wa Askofu Gwajima na waandishi wa habari, alioutumia kueleza anavyochukizwa na matukio ya kutoweka na kutekwa kwa watu, huku akitoa mfano wa hali ingekuwaje iwapo matukio hayo yangewakuta watoto wa viongozi akiwemo yeye mwenyewe.

Ingawa alichokieleza kilipata pongezi kutoka kwa wanaharakati, kwa upande mwingine alipingwa na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) ambacho naye ni kada pia, kwa kile walichoeleza ameshindwa kuwawakilisha wananchi jimboni kwake Kawe, ameamua kuichafua Serikali.

Haikuishia hapo, Askofu Gwajima aliibuka tena jana Juni 1, 2025 katika Ibada ya Jumapili kanisani kwake, akisema ataendelea kukemea pasi na kurudi nyuma matukio ya utekaji na kutoweka kwa watu katika mazingira ya kutatanisha.

Sambamba na hilo, alitangaza siku saba za maombi ya kufunga na kuomba kuanzia leo Jumatatu, Juni 2, 2025 ili haki itawale nchini na kwa viongozi mbalimbali wa kisiasa akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.

Barua ya kufutwa kwa kanisa hilo imetumwa leo, Jumatatu Juni 2, 2025 na kusainiwa na Kihampa kwenda kwa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Gwajima, ikieleza kitendo kilichofanywa na Askofu huyo kinaweza kuhatarisha amani na utulivu nchini.

Kwa mujibu wa barua hiyo inaeleza, katika siku za karibuni, Askofu Gwajima alionekana katika mimbari ya kanisa hilo, akitoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Barua hiyo inaeleza vitendo hivyo ni kinyume cha Kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, ikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 2019, kwa kuwa vinahatarisha amani na utulivu nchini.

“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 17(b) cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 2019 kilichoifanyia marekebisho kifungu cha 2 cha Sheria ya Jumuiya.

“Nakujulisha kuwa nimefuta usajili wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, kuanzia leo Juni 02, 2025. Unatakiwa kusitisha shughuli za kanisa lako mara moja,” anaeleza Msajili kupitia barua hiyo.

Hata hivyo, barua hiyo iliweka wazi kifungu cha 19(1) cha sheria hiyo kinalipa kanisa hilo haki ya kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia kwa Katibu Mkuu kupinga uamuzi huo.

“Rufaa dhidi ya uamuzi wa kufuta usajili wa Kanisa la Ufufuo na Uzima inapaswa kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ndani ya siku 21 kuanzia tarehe ya barua hii,” imeeleza barua hiyo.

Alichokisema Askofu Gwajima

Baada ya uamuzi huo wa Serikali, Mwananchi limefika kanisani hapo Ubungo ambapo imekuta maombi ya kufunga na kuomba yakiwa yanaendelea.

Mmoja wa wachungaji ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema hakuna kitakachowazuia kuendelea na ibada.

“Tupo kama unavyotuona, hatuna hofu na chochote, ratiba za kanisa zinaendelea kama kawaida,” amesema mchungaji huyo.

Hata hivyo amekataa kutaja jina akimtaka mwandishi kuandika kile anachokiona kinaendelea kanisani.

Mbali na ibada, nje ya kanisa hilo baadhi ya watu waliovaa kiraia wakiwa na radio call walionekana kuimarisha usalama katika eneo hilo huku watenda kazi wengine wakiwaongoza waumini kukaa kwa mpangilio, ili kuendelea na ibada.

Saa 12 jioni, Askofu Gwajima alipanda jukwaani na akasema:“Leo ni siku ya kwanza ya maombi yetu ya kuombea Taifa la Tanzania. Kubwa ni haki izuke katika nchi, tukae kwa amani na katika maombi haya hatuwaombei Wakristo tu, Waislamu tu bali tunaombea wote.”

Askofu Gwajima amesema katika maombi hayo watawaombea viongozi wa kisiasa akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na vyama vya siasa: “Ili jua la haki liweze kuzuka.”

Katikati ya maelezo yake, Askofu Gwajima baada ya nyimbo za kusifu akasema: “Nafikiri mmeona kwenye mtandao watu wanapitisha karatasi kwamba Kanisa la Ufufuo na Uzima limefungwa, hakuna wa kufunga kanisa la Mungu duniani, si kweli ni uongo ni wahuni hao wahuni…barua hiyo siyo ya Serikali, serikali yetu haiwezi kufanya hivyo.” Ameongeza: “Serikali yetu ni nzuri haifanyagi mambo kama hayo. Tunaendelea na maombi katika makanisa yetu zaidi ya 2,000 yako mtandaoni leo tutaendelea, kesho mpaka siku saba tutafunga mchana tu, tunakunywa maji tu na tunamlilia Mungu kuwa jua la haki lizuke, amani itawale Tanzania na ushindi utawale.”

Akiwa kanisani hapo, jana Jumapili Juni 1, 2025, Askofu Gwajima aliwataka waumini wake wafanye maombi hayo maalumu kwa ajili ya watu wanaotekwa, kutoweka bila kupatikana, huku baadhi wakikutwa wakiwa wameuawa au wamejeruhiwa vibaya.

Awali, katika ibada hiyo alianza kwa kuwaambia waumini waimbe wimbo wa ‘Tanzania Nakupenda’ kwa pamoja.

“Mwambie mwenzako Tanzania kwanza yeyote na lolote linafuata baadaye,” alisema Askofu Gwajima.

Pia, Askofu huyo alieleza kushangazwa na wingi wa watu waliofika katika kanisa hilo akisema: “Naona leo mmefurika sana, inaonekana mnajambo lenu sawasawa eeh sababu leo mmejaa mpaka nje kule.”

Baada ya wimbo huo, alianza kuelezea kuhusu mkutano wake na waandishi wa habari uliohusu utekaji wa watu na wasiojulikana.

Askofu huyo alisema ametafakari kuhusu taarifa za kupotea kwa watu nchini na kuona ni wakati sasa viongozi wa kiroho, kisiasa na kijamii kusimama kidete kulaani na kutaka hatua madhubuti zichukuliwe.

Baadhi ya matukio aliyotaja ni lile la kupotea kwa Sheikh Jabir Al-Farsy visiwani Zanzibari, aliyeripotiwa kuondoka nyumbani kwake Mei 28, mwaka huu majira ya usiku, kabla ya mwili wake kupatikana ukiwa umetupwa eneo la Bumbwisudi.

Askofu Gwajima alimtaja pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu wa CCM jijini Mwanza, Daniel Chonchorio aliyeondoka tangu Mei 23 na hajapatikana hadi sasa.

“Kwa hiyo watekaji wanateka mwana CCM na kiongozi wa dini unapomchukua Sheikh nyumbani kwake na anakutwa ameuawa hatujui kesho nani anafuata kwa baadaye,” alisema Askofu Gwajima.

Alisema CCM ambayo waasisi wake ni Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Abeid Aman Karume: “Chama hiki hakikubali utekaji na mimi mpaka sasa ni mwanachama wa CCM, naungana na Nyerere na Abeid Karume na viongozi wengine wote hawajaasisi chama cha kuteka watu.”

“CCM siyo watekaji na siyo chama cha kuteka watu na kama kuna mtu anateka,  anateka kwa masilahi yake mwenyewe. Mmenisikia ndugu zangu mimi hadi leo ni mwanachama wa CCM ambaye hataki utekaji na narudia tena sitaki utekaji na watu kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha,” alisema Askofu Gwajima.

Askofu Gwajima alisisitiza vitendo vya utekaji si sera ya CCM, bali vinafanywa na watu binafsi kwa maslahi yao na kwamba anayeteka kwa kisingizio cha chama hicho anatenda dhuluma.

Hata hivyo, gazeti hili halikuchapisha taarifa hiyo ya awali ya Askofu Gwajima, baada ya kugonga mwamba kwa juhudi za kuzipata mamlaka kujibu kile alichokieleza.

Ukiacha upinzani kutoka kwa makada hao, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mkutano mkuu maalumu wa CCM jijini Dodoma, alitaka vikao vya chama hicho, viteue wagombea ubunge watakaostahili ili kuwaepuka wale aliosema watakigwajimanize chama.

Related Posts