Serikali yawatoa hofu Watanzania mataifa makubwa kukata misaada

Dodoma. Serikali imesema ilishajiandaa kikamilifu kwa ajili ya kujiimarisha kimapato ili kukabiliana na hali ya namna yoyote iwapo  misaada kutoka kwa nchi wahisani itapungua.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatatu Juni 2, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ambaye ameeleza umuhimu wa mikakati hata kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa masharti kutoka kwa Rais wa Marekani, Donald Trump

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Profesa Aloyce Ndakidemi ameuliza ni nini mkakati wa Serikali katika kukabiliana na masharti magumu ya kuondoa misaada kwa nchi maskini kulikofanywa na Rais Donald Trump.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo ameuliza Serikali imejiandaa vipi kukabiliana na mabadiliko ya sera za baadhi ya nchi tajiri kulisaidia Taifa kukuza uchumi.

Waziri Nchemba amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza mapato ya ndani ili kuhakikisha kuwa sehemu kubwa ya bajeti inagharamiwa kwa kutumia mapato ya ndani.

“Aidha, kwa kutambua umuhimu wa mahitaji ya kibajeti, Serikali itaendelea kuvutia ushiriki wa sekta binafsi katika ugharamiaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia njia mbadala ikiwemo ubia kati ya sekta ya umma na binafsi,” amesema Dk Nchemba.

Waziri amesema mkakati huo utakwenda kusaidia kuipunguzia Serikali mzigo wa kukopa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa kibajeti, kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

Related Posts