Kibaha. Zaidi ya wafanyabiashara 1,000 katika mnada maarufu wa Loliondo Kibaha, Mkoa wa Pwani, wameanza kugawiwa maeneo mapya ya kufanyia biashara kila Jumamosi baada ya kuhamishwa kutoka eneo lao la awali.
Hatua hii imekuja kufuatia uamuzi wa mamlaka husika kulipangia eneo hilo la zamani wauzaji wa matunda na mbogamboga, kwa lengo la kuimarisha mpangilio wa biashara na kuhakikisha kila kundi linapata mazingira bora ya kufanyia shughuli zake.
Ugawaji wa maeneo hayo, ambayo kwa sasa ni barabara zilizoainishwa kwa matumizi ya muda maalumu wa mnada, unasimamiwa na viongozi wa wafanyabiashara hao, kwa ushirikiano na uongozi wa Serikali ya mtaa.
Wafanyabiashara hao wameeleza kuridhishwa kwao na hatua hiyo, wakisema Serikali imeonesha kuwajali na kutambua mchango wao katika kukuza uchumi wa eneo hilo.
Wakizungumzia hatua hiyo wakiwa eneo la tukio leo Jumatatu Juni 2, 2025 wamesema wanashukuru kwa kitendo kilichofanywa na serikali kwani kinaonesha kuwajali.
“Tunashukuru Serikali kwa kutupangia eneo hili jipya. Imekuwa ni faraja kubwa kuona tunazingatiwa na kupangiwa utaratibu rasmi wa kuendeleza biashara zetu bila kubughudhiwa,” amesema mmoja wa wafanyabiashara, Christina Tenda
Wamesema pamoja na changamoto za hapa na pale, wanatumaini mazingira hayo mapya yataongeza ufanisi wa biashara na kuimarisha uhusiano baina yao na mamlaka husika.
Hatua hii inaonekana kama sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kupanga upya shughuli za biashara ndogondogo katika Manispaa ya Kibaha, kwa kuzingatia usalama, usafi na uratibu mzuri wa maeneo ya umma.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Eliah Matinya amesema mpango wa halmashauri hiyo kuwahamishia kwenye eneo hilo umefanyika kwa njia shirikishi kuanzia hatua za awali.
“Tuliitwa na uongozi wa Serikali tukaeleweshwa sababu ya kutuhamisha tukaona zina maana kubwa sana kwakuwa kule ambako sasa hivi kunatumika na wauza matunda na nyanya kutabomolewa na kujengwa soko la kisasa, hivyo wanapisha na kuja kufanyia biashara ambako awali tulikuwepo sisi,” amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Aidan Mchiwa amewashukuru wafanyabiashara hao kwa kuitika agizo la Serikali na kukubali kuhamia maeneo mapya waliyopangiwa.