DC Monduli kumvaa Lukuvi Isimani, amtaka astaafu kwa heshima

Iringa. Mkuu wa Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, Festo Kiswaga amemtaka mbunge wa Isimani (CCM), William Lukuvi kustaafu kwa heshima baada ya kulitumikia jimbo hilo na Taifa kwa muda mrefu.

Kiswaga amebainisha hayo leo Jumanne Juni 3, 2025 kwenye mkutano wake na vyombo vya habari na kutoa wito huo.

Kiswaga ni miongoni mwa watu wanaotajwatajwa kutaka kuwania ubunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

‎Mkuu huyo wa wilaya amesema licha ya mchango mkubwa wa Lukuvi katika maendeleo ya sekta mbalimbali kwa miaka zaidi ya 30, ni muhimu sasa akaachana na siasa, hasa ya kugombea ubunge kupitia jimbo.

‎DC Kiswaga amesema ni wakati mwafaka kwa Lukuvi kustaafu kwa heshima na kutoa nafasi kwa kizazi kipya cha viongozi, kuendeleza mapambano ya maendeleo katika Jimbo la Isimani.

‎Ameongeza kuwa hali ya kisiasa katika Jimbo la Isimani kwa sasa si shwari kwa sababu baadhi ya watu wanaojitokeza kuwania nafasi ya ubunge wamekuwa wakikumbwa na vitisho na hofu, jambo linalodhoofisha misingi ya demokrasia.

‎“Kama tulivyokuwa tukisema, kinywa huumba na safari hii wimbo wa kustaafu uonekane kwa vitendo, si maneno tena,” amesema Kiswaga bila kutaja kama naye ni miongoni mwa wanaolitaka jimbo hilo.

‎Hata hivyo, Mwananchi limemtafuta Lukuvi azungumzie hoja hizo za Kiswaga lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

‎Mwananchi pia limemtafuta katibu wa mbunge huyo anayejulikana kwa jina la Amos Ndaso, amesema bado wanashughulikia mazishi ya mdogo wake Lukuvi, hivyo kauli za Kiswaga zitajibiwa Jumatatu Juni 10, 2025.

‎Alipotafutwa kueleza utekelezaji wa ilani ya chama katika kipindi cha uongozi wa Lukuvi katika Jimbo la Isimani, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Joseph Ryata amesema hawezi kuzungumza chochote hadi Juni 28, 2025.

Related Posts