Kigaila ataja sababu tatu Chaumma kushiriki uchaguzi

Mwanza. Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma, Benson Kigaila ametaja sababu tatu za chama hicho kuamua kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu, ikiwamo kukikabili Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza leo Jumanne Juni 3, 2025, Kigaila ametaja sababu ya kwanza kuwa ni kushinda uchaguzi na kuongoza Serikali, akisema hilo ndilo lengo la chama chochote cha siasa.

Sababu ya pili, amesema ni kupata fursa ya kushiriki vikao vya kisheria na kikatiba ikiwamo Bunge ambako watapata mwanya wa kupambania mabadiliko ya katiba, sheria na mifumo ya kiuongozi.

“Mabadiliko ya katiba na sheria hayapatikani mitaani kwenye vijiwe vya kahawa; mabadiliko yote ya kisheria yanapatikana kupitia bungeni. Sisi Chaumma tumeamua kushiriki uchaguzi tupate jukwaa la kupigania na kupata mabadiliko,” amesema Kigaila.

Amesema sababu ya tatu ni kukabiliana na CCM katika uwanja wa siasa ili kuzuia wagombea wa chama hicho kupita bila kupingwa karibu katika kila uchaguzi.

Amesema kuhusu, Chaumma inajipigania haki zake bila kusubiri mtu.

Amejenga hoja hiyo akisema iwapo itatokea mgombea wao amenyimwa fomu katika mchakato wa uchaguzi mkuu ujao, watachimba mkwara kusimamisha mchakato hadi apewe fomu.

Kuhusu Watanzania kupata mateso amesema wameshuhudia mateso mengi tangu kupata uhuru miaka 60 iliyopita, hivyo Chaumma inataka kwenda kubadilisha hali hiyo.

“Chaumma tunaenda kwenye uchaguzi kupigana kwenye sanduku la kura, kuwaokoa Watanzania tunataka wakulima, Watanzania waache kuteseka, wafanyabiashara wasiteseke,” amesema.

Kuhusu mabadiliko, Kigaila amesema Chaumma inataka mabadiliko ya sheria ya muundo wa Tume  Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Katiba mpya na mahitaji hayo yanapatikana kwa kupaza sauti bungeni.

“Kususa haiwezi kuwa dawa, huwezi kumuachia nyani shamba la mahindi, anaweza kumaliza shamba lote, Chaumma hatukubali hali hiyo tunaenda kupambana na CCM kwa kula nao sahani moja,” amesema.

Amesisitiza kuwa, chama hicho kinajisimamia chenyewe na hakina mtu anayeweka msukumo kama inavyosemwa huko mitaani.

Kigaila amesema: “Chaumma kinajisimamia chenyewe, ni chama huru na hakisubiri kupatiwa maelekezo.”

Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chaumma, Devotha Minja amewaomba Watanzania kukiunga mkono chama hicho ili kufanikisha lengo kushinda uchaguzi na kuingia kwenye mabaraza ya madiwani ya halmashauri na bungeni kupigania mabadiliko.

Amewasihi wanawake na vijana kukiunga mkono ili kishike dola, akiahidi kitabadilisha mfumo wa mikopo inayotolewa na halmashauri kuwezesha wengi kunufaika bila upendeleo.

Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu amewaomba Watanzania kupuuza tuhuma za waliotoka Chadema kujiunga Chaumma kununuliwa akisema ni propaganda za kisiasa zinazolenga kuwadhoofisha.

“Mimi nilimpoteza baba nikiwa umri wa miaka mitatu….nimelelewa na kukuzwa kwa msaada wa mama yangu, ndugu, jamaa na marafiki…sijawahi kununuliwa, nije ninunuliwe leo. Hebu waulizeni Salum amenunuliwa shilingi ngapi?” amesema Mwalimu.

Kwa upande wake, mgeni rasmi wa shughuli hiyo, Mwenyekiti wa Chaumma, Hashimu Rungwe amesema dhamira ya chama hicho ni kutaka kuwakomboa Watanzania na si jambo lingine.

“Tunataka sera ya ubwabwa iwafikie Watanzania wote, kwani waliowengi kupata lishe na milo mitatu ni changamoto, naamini dhamira yetu inaweza kutimia kwa watu kupata ubwabwa shuleni na hospitali bure iwapo tutaungwa mkono,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Wanawake wa Chaumma, Vellena Marwa amesema nchi imekaa vibaya kuna uonevu wa wananchi wa hali ya chini jambo ambalo chama hicho kikichukua dola kitalifanyia kazi.

“Tunahitaji kuwakomboa wananchi, wanawake, wazee na watoto, Wananchi muiunge mkono Chaumma ili tuwapeleke kwenye ukombozi kwani wote tumepigika,” amesema.

Mwanachama mwingine, Moza Ally amesema mpango wao ni kumtoa mkoloni mweusi pangoni ili kuhakikisha wananchi wanapata ukombozi na kuwa na maisha mzuri.

“Kina mama tunatabu nyingi, niwaombe kina mama tuungane na Chaumma tuingie kwenye sanduku la kura kuingiza wengi kwenye nafasi za uamuzi ili kwenda kubadilisha sera na mifumo,” amesema.

Mwalimu ametumia mkutano huo kuueleza umma kwanini chopa haijaruka, akisema imetokana na sababu za kisheria zinazohusiana na helkopta zenye usajili wa Kitanzania

“Tarehe mwezi wa tano, nilifanya mawasiliano na kampuni moja kwa ajili ya kupata chopa, lakini baadaye wakatueleza kuwa hawataweza kutuhudumia kutokana na katazo kutoka mamlaka ya kutoruka kwa ndege zote za helkopta zenye usajili wa Tanzania,” amesema Mwalimu.

Amesema baadaye Mei 14, 2025 walifanya mpango wa kupata chopa kutoka nchini Afrika Kusini, mpango ambao haukufanikiwa.

Mwalimu amesema baadaye walipata chopa kutoka nchini Kenya na kuanza kuomba kibali kutoka Mamlaka ya Anga Tanzania, na kufanikiwa kupata kibali leo asubuhi.

“Tulitarajia ndege ingeingia jiji Mwanza leo kabla ya saa 11:00 jioni lakini imeshindikana. Hivyo tunatarajia chopa yetu itaingia Mwanza kesho asubuhi na tutaendelea na ziara yetu ya chopa kama tulivyopanga,” amesema Mwalimu.

Related Posts