Majaliwa aonya dhidi ya chokochoko za kisiasa

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa vijana wa Tanzania kutojiingiza katika ajenda za watu wachache wanaolenga kuvuruga amani ya nchi, hususan kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Amesisitiza umuhimu wa vijana kuwa makini na kujiuliza kwa nini chokochoko huibuka mara kwa mara kila unapokaribia mwaka wa uchaguzi.

Akizungumza leo, Juni 3, 2025 katika kongamano la vijana na mazingira, Majaliwa amesema kumekuwa na mtindo unaojirudia wa baadhi ya watu kujitokeza nyakati za uchaguzi kwa lengo la kuvuruga amani.

Ametoa rai kwa vijana kuitambua mbinu hiyo mapema na kujiepusha kushiriki katika harakati zozote zinazoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

“Wale wote wanaotaka kuvuruga amani katika nchi hii hasa kipindi cha uchaguzi wanatumia nafasi zao kuharibu utulivu, taswira na usalama nchi. Tuwe makini sana na watu hawa ambao kwa namna moja au nyingine wana nguvu na wanaitumia kutaka kuharibu amani ya nchi.”

“Nitumie fursa hii kuwasihi vijana tumieni maarifa yenu kuchanganua mambo, hebu jiulizeni kwa nini haya yanaibuka kipindi cha uchaguzi tu. Hii sio mara ya kwanza kuona vituko vya aina hii vilikuwepo mwaka 2015, 2020 na sasa 2025. Hebu tujiulize tunaelekea wapi na wanaofanya wana  lengo gani,” amesema na kuongeza

“Tanzania imejengewa misingi imara ya amani na utulivu, naamini vijana mnapaswa kuiendeleza, sisi tulioko madarakani tukitoka nyie ndiyo mtashika hatamu ni muhimu kuhakikisha amani inaendelea kudumishwa nchini.”

Katika kongamano hilo Majaliwa amezindua Mkakati wa Taifa wa Usimamizi Taka (2025-2030) ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya siku ya mazingira duniani itakayoadhimishwa kitaifa Juni 5, 2025 jijini Dodoma.

Mkakati huo unalenga kutoa mwongozo wa kuhamasisha udhibiti na usimamizi wa taka kupitia uchumi rejeshi, ukitoa fursa ya kuzitazama taka kama rasilimali inayoweza kuzalisha bidhaa na kutengeza ajira.

Waziri Mkuu ametumia nafasi hiyo kuwasihi vijana hasa wasomi na wabunifu katika sekta ya mazingira kuisaidia Serikali mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto kwenye sekta hiyo, ikiwemo namna ya kupunguza kiwango kikubwa cha taka zinazozalishwa.

Kwa sasa Tanzania inazalisha taka ngumu kati ya tani milioni 14.4 hadi tani 20.7 kwa mwaka ambazo ni sawa na wastani wa kilo 241 hadi 347 kwa mtu mmoja kwa mwaka.

Maeneo makubwa yanayokadiriwa kuwa na uzalishaji mkubwa wa taka hizo ni mijini ambapo tafiti zinaonesha asilimia 70 ya taka zinazozalishwa zinaweza kurejelezwa, lakini ni asilimia tano hadi 10 ya taka hizo ndizo hurejelezwa.

Kufuatia hilo Majaliwa amewataka vijana kutumia maarifa waliyonayo kushauri Serikali na mamlaka husika mbinu bora zinazoweza kusaidia taka kurejelezwa na kukusanywa tofauti na hali ilivyo sasa.

“Sasa hivi taka tunazofanikiwa kuzikusanya ni asilimia 50 ya zote zinazozalishwa, hivyo kuna nyingi zinazosambaa nyie bado vijana mna maarifa, mbinu na mnaendelea kufanya bunifu mbalimbali tusaidieni nini kifanyike kukabiliana na hili.

Majaliwa pia ameziagiza halmashauri zote nchini kuweka vituo vya kutenganisha taka ili kuhakikisha zote zinazozalishwa zinashughulikiwa kwa njia salama na kupunguza kiwango cha zinazosambaa majalalani.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amewataka vijana kuzichangamkia fursa zinazotokana na takataka.

“Zamani tulikuwa tunaona taka kama uchafu usiohitajika tena, sasa hivi mambo yamebadilika taka ni fursa, ni utajiri unaweza kujiajiri kupitia kurejeleza takataka ukapata kipato huku ukiweka mazingira katika hali ya usafi.

“Niwahimize vijana kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuweza kutumia ubunifu na ujuzi wao wa kuzibadili changamoto mbalimbali ziwe fursa. Wachangamkie fursa za mazingira zilizopo kama biashara ya kaboni na urejelezaji wa taka za plastiki,” amesema Khamis.

Related Posts