Arusha. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, amewataka mawakili wa Serikali kuzingatia maadili ya kazi zao na kuepuka rushwa, akisisitiza kuwa rushwa haina siri na hatimaye hufichuliwa.
Pia, amewahimiza kutambua changamoto na ugumu wa kazi zao, kwa kuwa ni jukumu la kuleta haki katika jamii.
Amesisitiza wazingatie kutenda haki ili kuimarisha usawa na amani katika jamii.
Dk Ndumbaro amesema hayo leo Jumanne, Juni 3, 2025, wakati akihutubia mafunzo ya siku tatu yanayofanyika Arusha, yaliyoandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Mafunzo hayo yanajumuisha masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ujuzi wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dk Ndumbaro amesema kuwa kazi ya sheria inataka mtu mwenye maadili na kuwa licha ya kazi hiyo kuwa na majaribu mengi wanapaswa kuzingatia maadili yao.
“Kuna wakati majaribu yanakuwa ni mengi, usipofuata maadili utajiingiza kwenye mtego wa kupokea rushwa au kuungana na adui yako wa upande wa pili na ukifanya hivyo ujue umejiharibia mwenyewe. Hakuna rushwa inayotolewa kwa siri itajulikana tu.
“Wakati mwingine kabla haijakufikia watu wanajua hii rushwa inakwenda kwa fulani na ukiungana na adui wa upande wa pili itajulikana tu, baadaye utaanza kutafuta mchawi umekaa hupati uteuzi hupandishwi cheo kumbe mchawi ni wewe mwenyewe,” amesema.
Amesema hakuna kazi inayoleta haki katika jamii ikawa nyepesi hivyo wanapaswa kuhakikisha wamenyooka, mikono yao na dhamira za nafsi zao ziseme haki ipo kwani wakitenda jamii itakuwa na usawa.
“Kwenda kumshtaki mhalifu mwenye misuli yake ya kiuchumi si jambo dogo, lakini ni jambo ambalo linaleta amani katika jamii, usawa katika jamii na haki kwani hayo ndiyo yanafanya wananchi waiamini Serikali na kuheshimu sheria,” amesema.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, Dk Ndumbaro amewataka mawakili hao kutoa elimu kwa jamii zaidi juu ya utii wa sheria.
“Katika kipindi cha kampeni nimekuwa nikijiuliza sana kwamba kipindi hicho, sheria zinakwenda likizo?
“Kwa uelewa wangu mdogo wa sheria kipindi cha kampeni sheria haziendi likizo, sheria zipo zinafanya kazi wanasheria wapo wanafanya kazi, mahakama zipo zinafanya kazi. Kama wanasheria tuelimishe jamii na wanasiasa ili wasivunje sheria wakadhani wataachwa kwa sababu ni wanasiasa,” amesema.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, ofisi yao imeendesha mashauri ya madai 9,031 na kati ya hayo mashauri 8,347 ni ya madai ya kitaifa, 33 ni madai ya kimataifa na 633 ni ya kikatiba na haki za binadamu.
Amesema katika kuendesha mashauri hayo, mashauri 966 yamemalizika na wameweza kuokoa zaidi ya Sh51.02 bilioni kiasi ambacho Serikali ingelipa endapo ingeshindwa mashauri hayo.
Dk Possi amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025 wameendesha mashauri 70 yaliyotokana na uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba mwaka jana ambapo kati ya hayo matano yalifunguliwa kabla ya uchaguzi, yakipinga kanuni za uchaguzi huo.
“Katika kuendesha mashauri hayo yote 70, Serikali imeshinda 69 ambayo ni sawa na asilimia 98.2 huku tukishindwa shauri moja ambalo tumekata rufaa,” amesema.
Kuhusu mashauri ya usuluhishi, amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, wameendesha mashauri 205 na kati ya hayo 180 ni ya kitaifa na 29 ni ya kimataifa ambapo 21 yalimalizika na kushinda mashauri 16.
Dk Possi amesema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wamepanga kutoa mafunzo maalumu kwa mawakili kuhusu sheria za uchaguzi zitakazowezesha utendaji kazi wao.
Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA), Bavoo Yunusi amesema kutokana na mabadiliko mbalimbali ya sheria za uchaguzi, moja ya majukumu yao ni kuhakikisha wananchi wanaelewa mambo ya msingi yanayohusiana na uchaguzi mkuu.
Amesema wameandaa kongamano la kitaifa lenye dhima ya kujenga uelewa wa pamoja kwa mawakili na wananchi kuhusu masuala ya uchaguzi mkuu.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Alice Mtulo amesema mafunzo hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo, ‘ubobezi wa kisheria kwa ajili ya kesho, teknolojia, mikakati na mizania binafsi kwa mawakili wa Serikali katika kutekeleza dira ya maendeleo ya taifa 2050’.
Amesema mafunzo hayo yamehusisha mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Joseph Mhagama amesema miongoni mwa changamoto zilizokuwa zinajitokeza ni pale Taifa linapotakiwa kusimamia shauri la madai au usuluhishi nje ya nchi, ambapo zipo nyakati limekuwa likipoteza na kupata hasara kubwa.