Mwanaharakati mbaroni akihamaisha kupingwa muswada wa fedha

Nairobi. Wanaharakati nchini Kenya na Chama cha Mawakili Kenya (LSK) wamelitaka jeshi la polisi kumwachilia kwa dhamana mwanaharakati Rose Njeri ambaye alikamatwa na anaendelea kuwekwa kizuizini.

Rose anashikiliwa kwa tuhuma za kutengeneza mtandao wa maoni na kuwashawishi Wakenya wenzake kushiriki katika hatua ya kupinga muswada wa fedha 2025.

Njeri ambaye ni mfanyabiashara na mtaalamu wa masuala ya fedha anadaiwa kutumia ukurasa wake wa mtandao wa X kutoa mafunzo kwa Wakenya kuhusu yaliyomo kwenye muswada huo wa fedha 2025

Muswada huo unatarajiwa kujadiliwa bungeni mwezi huu baada ya Waziri wa Fedha, John Mbadi kusoma bajeti ya taifa Juni 12, 2025.

Kwa mujibu wa mwanaharakati Boniface Mwangi, wanaharakati wamepanga kuandamana hadi katika Kituo cha Polisi Pangani jijini Nairobi kuishinikiza polisi kumuachilia huru, kwa dhamana Njeri.

Hiyo ni kutokana na kile walichodai Njeri ana matatizo ya upungufu wa damu mwilini na anapaswa kupata lishe bora na matibabu.

Jumamosi, familia yake ilishinda katika kituo hicho cha polisi huku wakidai kwamba Ofisa mkuu anayesimamia kituo hicho (OCS) aliwaeleza kuwa kesi hiyo inachunguzwa na idara ya uchunguzi wa jinai (DCI).

Aliyekuwa Jaji Mkuu wa pili chini ya katiba mpya nchini Kenya, David Maraga amesema:“Vijana nchini Kenya hawana cha kusherehekea katika siku kuu hii ya Madaraka kwa kuwa Uhuru wao unabanwa.”

Taarifa za kuwafahamisha Wakenya kuhusu yanayopendekezwa katika muswada wa fedha 2025, zimeanza kuchapishwa katika mitandao ya kijamii huku wengi wakitumia X kueleza kero zao na mapendekezo yaliyomo kama vile madai kwamba kodi ya ongezeko la thamani (VAT) itapanda kutoka asilimia 16 hadi 18.

Hiyo itafanya baadhi ya bidhaa ambazo zilikuwa hazitozwi ushuru kama vile maziwa na mikate zingepanda bei katika hali ambayo wengi hawangeweza kumudu gharama yake.

Kufuatia hilo watu wengi wanaitaka Serikali kumuachia huru mwanaharakati huyo ambaye pia ni mtalaamu wa teknolojia ya kompyuta, huku wakidai kuwa kukamatwa kwakwe kunakiuka haki zake za kimsingi na ni shambulizi dhidi ya wanaojieleza kupitia mfumo wa kidijitali.

Mwaka mmoja uliopita, vijana nchini Kenya waliandamana kupinga muswada wa fedha 2024 ambao walihisi ulikuwa unambana Mkenya zaidi na ungepandisha hali ya maisha na kufanya wengi wasiweze kumudu mahitaji yao ya kila siku.

Maandamano yaliendelea kwa wiki kadhaa hadi Juni 25, 2024  ambapo mambo yaligeuka kuwa magumu vijana walipolivamia Bunge la Kenya huku polisi wakiwafyatulia risasi.

Baada ya ghasia za saa kadhaa vijana kadhaa walifariki, huku wengine wengi wakiripotiwa kukamatwa.

Rais WIllliam Ruto alikanusha madai kwamba polisi wanawakamata raia, lakini wiki chache zilizopita alisema kwamba wote walioripotiwa kupotea walirejeshwa makwao lakini baadhi ya familia bado zinasema kwamba watoto wao hadi sasa hawajulikani walipo.

Akimzungumzia Rose Njeri, Rais wa LSK, Faith Odhiambo amesema mawakili watafika mahakamani leo Juni 3, 2025 kuishinikiza serikali kumfikisha kortini au kumuacha huru mwanaharakati huyo.

Faith pia alilalamikia alivyowahi kuzuiliwa bila ya mawakili wake kupata fursa ya kumuona au kupata dhamana ya polisi.

Related Posts