Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, ameongoza Misa ya Shukurani kwa mara ya kwanza tangu aruhusiwe kutoka hospitali alikokuwa akipatiwa matibabu kwa takriban mwezi mmoja, kufuatia tukio la kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Ibada hiyo imefanyika leo Juni 3, 2024 katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, lililopo katika makao makuu ya TEC, Kurasini jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na mapadri, watawa na wafanyakazi wa Sekretarieti ya TEC waliokusanyika kwa pamoja kumshukuru Mungu kwa uponyaji wa Padri Kitima.
Akizungumza wakati wa mahubiri, Padri Kitima amesema, anamshukuru Mungu kwa uponyaji kwa sababu shambulio lake lilikuwa na lengo la kukatisha maisha.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles akiongoza adhimisho la Misa Takatifu ya shukrani katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili lililopo TEC-Kurasini jijini Dar es Salaam.
“Tunamshukuru Mungu kwa wema wake. Pia nawapongeza na kuwashukuru wote waliokuwa nami kwa sala, upendo na matashi mema wakati wote wa matibabu yangu. Shambulio lile lilikuwa na lengo la kukatisha maisha yangu, lakini rehema za Mungu zimeonekana.”
Amesisitiza kuwa Kanisa Katoliki linapaswa kuendelea kuwa nguzo ya matumaini kwa jamii, hasa kwa wanyonge wasio na sauti.
“Kanisa ni sauti ya watu wasio na sauti, ni msindikizaji wa wanyonge. Ni jukumu letu kuhakikisha linaendelea kuwa mwanga wa Watanzania wote,” amesema.

Padri Kitima pia aliwataka wafanyakazi wa Sekretarieti ya TEC kuyatazama yaliyotokea kwa jicho la kiimani na kuendelea kusimama imara licha ya changamoto.
“Mungu hasahau, hatakaa kimya. Tutambue kuwa hata mitume walikumbana na mateso, lakini waliendelea mbele kwa imani. Tusirudi nyuma,” alihimiza.
Itakumbukwa Padri Kitima alishambuliwa na watu wasiojulikana eneo la Kurasini, Temeke jijini Dar es Salaam zilipo ofisi za TEC makao makuu.