Dodoma. Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imeahirisha kusikiliza rufaa ya kupinga hukumu ya kifungo cha maisha gerezani inayowakabili aliyekuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Clinton Damas, maarufu Nyundo, na wenzake watatu.
Nyundo na wenzake watatu walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani Septemba 30, 2024, baada ya kupatikana na hatia ya kubaka kwa pamoja na kumuingilia kinyume na maumbile msichana mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam, aliyetambulishwa mahakamani kwa jina la X.
Aidha, kila mmoja aliamriwa kumlipa fidia ya Sh1 milioni kutokana na madhara waliyomsababishia.
Wakata rufaa katika kesi hiyo ni MT. 140105 Private Clinton Damas (Nyundo), aliyekuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Amin Lema (Kindamba), Nickson Jackson (Machuche) na C.1693 WDR Praygod Mushi, aliyekuwa askari Magereza.
Rufaa hiyo ilianza kusikilizwa leo, Jumanne Juni 3, 2025, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Amir Mruma. Upande wa utetezi unaongozwa na mawakili Godfrey Wasonga, Meshack Ngamando na Robert Owino, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Lucy Uisso, akiambatana na mawakili wengine watatu wa Serikali.
Wakili wa washtakiwa, Godfrey Wasonga, ameiambia Mahakama kuwa upande wa utetezi una jumla ya sababu 33 za kukata rufaa, lakini wameziweka katika makundi tisa ili kurahisisha usikilizwaji wake.
Kwa siku ya leo, upande wa utetezi umeanza kwa kuwasilisha hoja mbili kuu ikiwamo kuhusu mapungufu yaliyokuwapo katika hati ya mashitaka wakati wa usikilizwaji wa kesi ya awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, ambayo ilisababisha warufani kutiwa hatiani.
Hoja ya pili imeeleza kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria wakati wa uchukuaji wa maelezo ya warufani hao, jambo ambalo linaathiri uhalali wa ushahidi uliotumika kuwahukumu.
Baada ya kusikiliza hoja mbili za awali kutoka kwa upande wa utetezi ambazo zilichukua takriban saa sita kuwasilishwa kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri, Jaji Amir Mruma wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ameahirisha usikilizwaji wa rufaa hiyo hadi Juni 9, 2025 saa 4:00 asubuhi.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama, Wakili wa utetezi Meshack Ngamando amesema kuwa lengo la kukata rufaa ni kuhakikisha haki inatendeka na kwamba washtakiwa wanapewa nafasi ya kupata haki yao kwa mujibu wa sheria.
Amesema sababu kubwa ya kukata rufaa ni kutokana na mapungufu yaliyojitokeza katika mwenendo wa kesi ya awali, jambo ambalo linaathiri uhalali wa hukumu iliyotolewa.
“Hatuwezi kusema kuwa hukumu ile ilitokana na mihemko ya kijamii, kwa sababu Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kutoa uamuzi kutokana na ushahidi uliopo.
“Lakini kwa kuwa hatukuridhika na maamuzi yale, tumetumia haki yetu ya kikatiba kukata rufaa. Hata uamuzi utakaotolewa sasa tukiona haujaridhisha, tutakata rufaa tena,” alisema Ngamando.
Nyundo na wenzake watatu walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani Septemba 30, 2024, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume na maumbile msichana mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam, aliyetambulishwa mahakamani kwa jina la X. Pamoja na adhabu hiyo, kila mmoja alitakiwa kumlipa fidia ya Sh1 milioni.
Hadi sasa, warufani hao wametumikia adhabu yao kwa muda wa takriban miezi minane kabla ya kuanza kusikilizwa kwa rufaa yao.