Dodoma. Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2025/26, huku mjadala kwa wabunge ukiwa kwenye gharama za vifurushi vya bima ya afya na matibabu ya ugonjwa wa figo.
Wizara ya Afya ililiomba Bunge kuwaidhinishia Sh1.61 trilioni huku Sh991.75 bilioni kati ya hizo zikienda katika miradi ya maendeleo.
Akichangia katika mjadala huo leo Jumanne Juni 3, 2025 Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko amesema kwa mujibu wa kitabu kilichotolewa na Wizara ya Afya, utafiti wa magonjwa yasiyoambukiza ulifanyika mwaka 1987.
Matiko amesema katika utafiti huo, ilibainika kuwa kati ya watu 100, mmoja alikuwa na kisukari huku watano wakiwa na shinikizo la juu la damu.
Amesema katika utafiti mwingine uliofanyika mwaka 2012, ilibainika kuwa kati ya watu 100, tisa walikuwa na kisukari na 26 shinikizo la juu la damu.
Hata hivyo, Matiko amesema tangu kufanyika kwa utafiti huo, hakuna utafiti mwingine uliowahi kufanyika nchini.
“Na uhakika mkifanya is worse (hali ni mbaya zaidi) na mmeonyesha mambo mbalimbali yanayosababisha ikiwamo vyakula, kutofanya mazoezi, sijui pombe,” amesema Matiko.
Licha ya kauli hiyo, takwimu zinaonesha kuwa, wizara hiyo imefanya utafiti mwingine wa magonjwa yasiyoambukiza kwa mwaka 2023/24 ambao matokeo yake yameanza kutumika.
Kwa upande wa mazoezi, Matiko ameshauri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kukaa na Wizara ya Afya na kuangalia jinsi ya kuweka njia na sehemu za kukimbia mitaani, ili watu wakitoka kazini wapate maeneo ya kufanyia mazoezi.
Kuhusu unywaji wa pombe, Matiko amesema vijana nchini wanateketea kwa unywaji wa pombe zinazouzwa katika maeneo holela na wakati mwingine ni feki.
“Mnasema matibabu ya figo ni gharama kama hatutazuia lazima iwe gharama, tutatumia fedha nyingi kuwatibu Watanzania. Wakati Taifa linaendelea na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, magonjwa yasiyoambukiza yatatengeneza bomu kubwa kwenye utaratibu huo,” amesema.
Matiko ameshauri wizara hiyo kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na mamlaka nyingine kudhibiti uuzaji holela na pombe feki ambazo ziko mtaani katika maduka ya vyakula pia.
“Huko mtaani tunazika sana wengine si kwa ajili ya ugonjwa wa figo, wengine wanakunywa pombe tu. Mtu ameshikilia energy drink (kinywaji cha kuongeza nguvu). Bodaboda, vijana wanakufa, wengine wanakunywa lakini hawali wanakufa,” amesema Matiko.
Amesema Serikali inatumia mitutu ya bunduki kulinda mipaka lakini vijana wa nchi wanaangamia, jambo ambalo wangefanya kupunguza vifo.
Mbunge wa Mpanda Vijijini (CCM) Moshi Kakoso ameungana na wabunge wengine kushauri Serikali kulifanyia kazi ili kuepusha Taifa kuingia katika gharama kubwa za matibabu hasa kwa vijana.
“Bodaboda wameathirika sana na matumizi mabaya ya pombe. Naomba katika maeneo haya tuyafanyie kazi bila kuyafanyia kazi Taifa litaingia katika gharama kubwa ya kutibu wagonjwa karibu nchi nzima,” amesema Kakoso ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.
Hata hivyo, Mbunge wa Bunda Vijijini, (CCM) Mwita Getere amewataka wabunge kutoangalia ukubwa wa gharama bali manufaa yake kwa kuwa, unampa mgonjwa uhakika wa matibabu, kwani dawa nyingi bei ghali.
Hata hivyo, Getere alipewa taarifa na Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Noah Lembris kuwa asilinganishe matajiri wenye uwezo wa kulipa bima ya afya na Watanzania ambao ni masikini, hivyo hawezi kumudu gharama hizo.
Akipokea taarifa hiyo, Getere amesema watu waelimishwe kuhusiana na umuhimu wa bima ya afya ili waendelee kuishi na vinginevyo watu wengi watafia nchini.
Kuhusu gharama za matibabu ya figo, Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Francis Ndulane ameshauri Serikali kupeleka vifaa vya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo hadi katika wilaya ili kuwaepusha gharama za kufuata huduma hiyo umbali mrefu.
“Kumekuwa na gharama kubwa ya kutibu huu ugonjwa, ninaomba Serikali tutengeneze programu kama ilivyokuwa katika kifua kikuu, saratani (mionzi) ambao wanapata huduma bure ili na huduma hii pia itolewe bure,” amesema.
Ndulane ameitaka Serikali kutafuta chanzo cha fedha cha kugharamia matibabu ya bure ya ugonjwa huo.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Regina Qwaray amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu na vifaa vya afya na sasa kinachotakiwa ni kufanya utafiti wa kina kufahamu sababu za ongezeko la magonjwa hayo.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Regina Qwaray.
Amesema wananchi wapewe elimu ya kutosha kuhusu magonjwa yasiyoambukizwa ikiwamo saratani na figo ambayo zamani ilikuwa ikiwatokea wazee na si watoto wadogo kama ilivyo sasa, akishauri uchunguzi zaidi kwenye mazao.
Regina amesema na hilo linaweza kufanyika kwa kuwa na vifaa vya kupima mboga na mazao katika masoko nchini ili kuona ubora na kama kuna sumu, hivyo kuzuia kutumika.
Mbunge wa Singida Magharibi Elibariki Kingu, ameshauri kutokana na umuhimu wa nafasi ya Mganga Mkuu wa Serikali (CMO) iwe chini ya wizara lakini ijitegemee yenyewe.
“Majukumu ya CMO ni nyeti sana, wakati mwingine zinaweza kutokea rasharasha za kisiasa zinazoweza kumfanya kushindwa kufanya majukumu ambayo yatalinda ‘interest’ ya Taifa letu na kuhakikisha professionalism (taaluma) inafuatwa,” amesema.
Kwa upande wa huduma za kujifungua, Mbunge wa Ilemela (CCM), Dk Angelina Mabula amesema kutokana na kuongezeka kwa huduma za kujifungua kwa upasuaji, vijana wengi kwa sasa wanashawishika kujifungua kwa njia hiyo na kuogopa kujifungua kwa kawaida.
Ameomba ushauri zaidi utolewe kwa mabinti ni namna gani anaweza kubeba ujauzito na kufanya mazoezi yapi ili wakati wa kujifungua wajifungue kawaida na kuwaepusha na uzazi wa upasuaji.
Kuhusu P2, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Dk Thea Ntara ameshauri Serikali kuangalia ni namna gani watatoa elimu ya matumizi bora ya dawa za P2 kwa sababu inaonekana kuna madhara zaidi kuliko faida.
Akihitimisha hoja hiyo, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema katika mwaka 2025/26, Serikali itaanza utaratibu wa bima ya afya kwa wote ili kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na uwekezaji uliofanywa kwenye sekta ya afya.
“Vifurushi tulivyonavyo vya bima ya afya, sivyo vifurushi vya bima ya afya kwa wote, Waheshimiwa wabunge kaeni sawasawa tutakuja na bima ya afya kwa wote ili uweze kuwasaidia wananchi wote na lengo letu ni kupunguza vifo na kuwafanya wananchi wetu wawe salama,” amesema.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama akizungumza bungeni leo Jumanne Juni 3, 2025 wakati wa kupitisha makadirio ya Mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026.
Kuhusu magonjwa yanayoambukiza ikiwamo homa ya ini, aliwahakikishia wabunge kuwa, kwa sasa Serikali imefanyia kazi kwa kuingiza kwenye mkakati wa kitaifa wa kupambana na magonjwa yanayoambukiza.
Kuhusu madeni ya Bohari ya Dawa (MSD), Mhagama amesema wamekuwa na vikao na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kwa ajili ya kuyafanyia kazi madeni ya MSD ili iweze kufanya kazi vizuri.
“MSD iliwasilisha maombi ya Sh561 bilioni, waheshimiwa wabunge toka MSD hii imeanza ni kwa mara ya kwanza mwaka jana wamepewa Sh100 bilioni,” amesema.
Amesema hadi sasa MSD wameongezewa Sh50 bilioni na hivyo hadi leo wana Sh150 bilioni, mbali na juhudi zao wanazozifanya za kuwekeza ndani.
Mhagama amesema ukiachia mtaji na deni, imeendelea kutoa Sh42 bilioni kwa ajili ya kujenga maghala ya kuhifadhia bidhaa za afya.
“Lakini Serikali kwa mwaka huu wa fedha, taarifa ya kamati ilizungumza madeni ya bidhaa msonge ambayo yamezidi kuifanya MSD iendelee kunyong’onyea katika utendaji wake, Serikali imetenga tena Sh48.2 bilioni kwa ajili ya ugomboaji wa bidhaa za miradi msonge ili kuifanya MSD iendelee kuwa salama,”amesema.
Pia Mhagama amesema Serikali inatarajia kupata fedha kutoka China kama ruzuku ya Sh119 bilioni na zitasaidia kuongeza nguvu kwa MSD.
Kuhusu deni la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Waziri Mhagama amesema wamekubaliana na Waziri Mwigulu kutoa hati fungani ambayo itasaidia kubeba mzigo huo na taratibu zote zimekamilika.