Wachumi wapinga wananchi kukatwa Sh100 kwenye simu

Dar es Salaam. Wataalamu wa uchumi nchini wamesema iwapo kodi na tozo zitaendelea kuongezwa kwa wananchi ambao ndiyo wazalishaji wa mali, uchumi wa nchi hauwezi kukua.

Wameeleza kuwa msingi wa uchumi ni kuwaachia wananchi fedha ili wazitumie katika kufanya biashara, miamala na uwekezaji, “badala ya kuzipeleka serikalini kwa njia ya tozo nyingi zisizo na tija”.

Kauli hiyo imekuja kufuatia pendekezo la Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga, alilolitoa bungeni jana Jumatatu, Juni 2, 2025, akishauri wananchi wakatwe Sh100 kila wanaponunua vocha ya Sh1, 000, kwa ajili ya kuchangia bima ya afya kwa wote.

Mtinga alisema Tanzania ikiwa na laini hai za simu takriban milioni 90.4, hatua hiyo inaweza kuingiza Sh9.4 bilioni kwa siku, Sh271.2 bilioni kwa mwezi na Sh3.2 trilioni kwa mwaka, ambazo zitasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo kupata huduma ya afya.

Hata hivyo, Mwanazuoni wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo, amesema wazo hilo linawezekana kiutekelezaji, lakini halina mantiki ya kiuchumi na haliwezi kusaidia katika kukuza uchumi wa nchi.

“Unapoongeza kodi na tozo, unazitoa fedha kwa wananchi ambao ndio wanapaswa kuzalisha mali na kuzipeleka serikalini. Uchumi haujawahi kukua namna hiyo,” amesema Profesa Kinyondo.

Ameongeza kuwa wananchi tayari wanalipia huduma za afya na baadhi yao wana bima ya afya, hivyo kuwatoza tena kupitia vocha za simu ni sawa na kuwabebesha mzigo mara mbili.

“Leo tukate tozo ya vocha, kesho ya kupokea simu, keshokutwa maongezi – hii si hulka ya kiuchumi. Ni lazima fedha zionekane mikononi mwa watu ili wafanye biashara na kuwekeza kwenye shughuli za maendeleo,” amesema.

Hata hivyo, Profesa Haji Semboje, mwanazuoni mwinmgine wa uchumi amesema pendekezo hilo ni wazo binafsi la mbunge lakini halitekelezeki na halina mashiko katika mazingira ya nchi yenye wananchi wengi masikini.

“Hili ni wazo la mtu, lakini kiuchumi halitekelezeki. Suala la afya halihusiani na fedha pekee bali sera, sheria, mifumo ya kitaasisi na utekelezaji wake,” amesema Profesa Semboje.

Mbali na wanazuoni hao, baadhi ya wananchi waliotoa maoni kuhusu hoja hiyo wamesema badala ya kuwabebesha wananchi, Serikali itumie ipasavyo mapato kutoka sekta za madini na rasilimali nyingine nyingi ilizonazo.

“Kwa nini kila wakati mzigo uwe kwa wananchi? Madini tuliyonayo yakitumika vizuri hakuna ambaye atakosa huduma za afya,” ameandika Krystalice25 kwenye mtandao wa kijamii.

Akichangia hoja hiyo, Mchungaji Mwamakimbula ameongeza kuwa “Mtu anaweka Sh1,000 ili anunue bando, sasa anapokatwa Sh100 inabidi aongeze Sh500. Kama hana hiyo Sh500 inamaanisha atakosa mawasiliano.”

Profesa Semboja ameshauri ili kufanikisha mpango wa bima ya afya kwa wote, kunapaswa kuwepo na sera madhubuti, sheria sahihi na taasisi zenye uwezo wa kusimamia vizuri huduma hizo.

“Wananchi wapewe elimu na taarifa sahihi. Jamii ichukuliwe kama rasilimali ya nguvu kazi na ishirikishwe kikamilifu,” amesema.

Kwa upande wake Profesa Kinyondo amependekeza mfuko wa bima ya afya uboreshwe kabla ya kupanua wigo wake. Ametolea mfano wa NHIF ambao alisema ulikuwa ukitumia fedha vibaya, hivyo unahitaji marekebisho makubwa.

“NHIF lazima ijiendeshe vizuri. Pili, ili kuwa na bima kwa wote, inapaswa kuwa nafuu. Tusipoangalia tutaendelea kuongeza tozo hadi kwenye mafuta na umeme (luku). Twende taratibu, tukijipanga hadi 2035 tuwe tumeifikia bima kwa wote,” amesema.

Kwa ujumla, wachumi na wananchi wengi wameeleza kuwa hatua ya kuongeza tozo kwa wananchi maskini si suluhisho la kudumu katika kufanikisha mpango wa bima ya afya kwa wote.

Badala yake, wamesema inahitajika mikakati jumuishi inayozingatia sera bora, usimamizi wa rasilimali, na utekelezaji unaozingatia hali halisi ya uchumi wa nchi.

Related Posts