Unguja. Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imewateua mabalozi wanne wa utalii, wakiwemo raia wa ndani na wa kigeni zikiwa ni juhudi za kukuza na kutangaza utalii wa Zanzibar.
Miongoni mwa mabalozi hao ni Alois Inninger, raia wa Ujerumani, ambaye anatarajiwa kusaidia kuvutia watalii kutoka nchi mbalimbali za Ulaya. Wengine walioteuliwa ni Ruqaiya Karanja, mshindi wa taji la Miss Utalii mwaka 2020, Dk Lisa Wana na Abdurahim Abduhhamid Numa, wote wakiwa na uzoefu wa muda mrefu katika sekta ya utalii.
Akizungumza wakati wa kuwatambulisha na kuwakabidhi vyeti mabalozi hao leo Juni 3, 2025, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amesema kwa muda mrefu walikuwa wakiteua wasanii kuwa mabalozi wa utalii, lakini mwaka huu wameamua kubadili mkakati kwa kuwateua watu wenye ushawishi na uzoefu wa moja kwa moja katika sekta hiyo.
“Mabalozi wa heshima wa utalii wamesema kuwa, ingawa hapo awali tuliwahi kuteua wasanii, kwa sasa jambo la msingi ni kuitangaza vyema chapa ya Zanzibar. Lengo ni kuwafanya watu, ndani na nje ya nchi, watambue vivutio vya kipekee vya Zanzibar pamoja na fursa zilizopo kitaifa na kimataifa. Tumejitathmini na kujiridhisha kwamba hawa watakuwa na mchango mkubwa katika nembo yetu ya Zanzibar — kila mmoja anakuja na haiba, kipaji, na uhamasishaji wake,” amesema Soraga.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Aboud Suleiman Jumbe, amesema wizara inatarajia mabalozi hao kutumia utaalamu na uzoefu wao kuitangaza Zanzibar na vivutio vyake kupitia mifumo mbalimbali ya habari, taarifa na matangazo ya kibiashara.
Amesema pia wanatarajia mabalozi hao kutoa simulizi nzuri kuhusu Zanzibar, jambo litakalowavutia zaidi watalii kutembelea kisiwa hicho.
Naye Inninger, mwekezaji katika sekta ya utalii kwa zaidi ya miaka 13, amesema anajivunia kupewa heshima ya kuiwakilisha Zanzibar kimataifa.
“Maana ya kuwa balozi ni kuiwakilisha nchi katika njia bora na kuleta watalii wengi zaidi Zanzibar kutoka sio tu kwenye nchi yangu bali pia mataifa mbalimbali ya Ulaya,” alisema.
Amesema kazi yake haitakuwa tu kutafuta watalii, bali pia kuwahamasisha kuwa wawekezaji wa baadaye katika kisiwa hicho. Ameongeza kuwa atajielekeza kutafuta masoko mapya kutoka maeneo ambayo bado hayajafikiwa ipasavyo, kama vile Amerika Kusini, Asia na Australia.
Amesema ukuaji wa sekta ya utalii Zanzibar umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya Serikali, hali inayowezesha kuboresha ustawi wa jamii na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla.
“Nitafanya kila ninachoweza kuiwakilisha Zanzibar katika mazingira bora zaidi, ndani na nje ya nchi, kuongeza idadi ya watalii na kuvutia wawekezaji zaidi kuwekeza Zanzibar,” amesema.
Kwa upande wake, Ruqaiya Karanja, aliyekuwa Miss Utalii mwaka 2020 na mbunifu mwenye uzoefu katika sekta ya utalii, amesema atatumia ujuzi wake kuhamasisha vijana na wanafunzi kutembelea fukwe na misitu ya kipekee ya Zanzibar.