Waumini kanisa la Askofu Gwajima walivyokaa kwa saa 11 katika vumbi, jua

Dar es Salaam. Ni huzuni! ndivyo ilivyokuwa kwa waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima ambao kwa zaidi ya saa 10 wamepiga kambi mita chache kutoka lilipo kanisa lao wakisubiri hatima ya kiongozi na kanisa lao.

Kanisa hii limezungushiwa utepe, liko chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi, waumini wakizuiwa kuendelea na maombi ya siku saba yaliyoanza jana Jumatatu, Juni 2, 2025 kabla ya kutawanywa na polisi katika purukushani zilizoanza saa 5 usiku wa kuamkia leo.

Leo Jumanne, Juni 3, 2025 tangu asubuhi hadi sasa (saa 11:00 jioni) polisi wameendelea kuimarisha ulinzi kanisani hapo, huku waumini wakikaa juani  na kupigwa vumbi wakihaha kujua hatima ya kanisa lao huku wakilazimika kufanya maombi barabarani.

Kanisa hilo lililopo Ubungo, Dar es Salaam limezungushiwa utepe wa njano, hakuna anayeruhusiwa kusogea wala kuchukua chochote, huku baadhi ya magari binafsi nayo yakiwa yamekumbwa na kadhia ya kuzungushiwa utepe, kwa kile ambacho polisi inadai inatekeleza maagizo kufuatia kanisa hilo kufutwa na msajili.

Mwananchi iliyopo eneo la tukio muda wote imeshuhudia baadhi ya waumini wakitiana moyo vikundi vikundi, wakiamini kazi ya kanisa itaendelea licha ya changamoto ambayo kanisa lao linapitia kwa sasa.

Hawakuishia hapo, wakiwa upande wa pili wa barabara, wakilitazama kwa mbali kanisa lao ambalo liko chini ya ulinzi wa Polisi, waumini hao walikusanyika vikundi vikundi na baadhi yao kusali wakiwa kwenye vibanda vilivyo pembezoni mwa barabara upande wa pili wa kanisa.

Licha ya nyuso za huzuni, waumini hao wanaamini siku saba za kufunga na kuomba zilizoanza jioni ya Juni 2, 2025 kabla ya kanisa kuvamiwa na polisi na kuzungushiwa utepe zitaendelea na kufanyika kwa mafanikio.

Wakiwa na imani hiyo, wameendelea kutazama gari la maji ya kuwasha likiwa limeegeshwa kwa saa kadhaa kwenye lango kuu la kanisa lao likiwekwa tayari kwa lolote huku askari wa kutuliza ghasia wenye silaha wakipishana kuimarisha doria.

Upande wa pili ambako wapo waumini hao, mmoja wa watu aliyekuwa amevaa kiraia aliwaonya waandishi wa habari kuwahoji waumini wa kanisa hilo kwa kile alichodai si wasemaji wa kanisa, akitaka kila kinachohusu kanisa hilo ahojiwe muhusika ambaye ni Askofu Gwajima.

Hata hivyo, Askofu Gwajima ambaye pia ni mbunge wa Kawe, hayupo eneo hilo huku waumini wake wakidai moja ya kutoondoka eneo hilo ni kutaka kufahamu alipo kiongozi wao huyo wa kiroho.

“Baba (Askofu Gwajima) wakati vurugu na polisi zinatokea (usiku wa kuamkia Juni 3) alikuwepo kanisani, lakini katika vurugu zile hatujui yupo wapi,” amesema mchungaji Christian Laisubira wa kanisa hilo akiainisha waumini hawataondoka hadi watakapofahamu ni wapi alipo.

Jana Jumatatu, Juni 2, 2025, Serikali ilitagaza kulifuta kanisa hilo linalomilikiwa na Askofu Josephat Gwajima ni kile kilichoelezwa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ni ukiukwaji wa Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Msingi wa hayo ni mkutano wa Askofu Gwajima na waandishi wa habari, alioutumia kueleza anavyochukizwa na matukio ya kutoweka na kutekwa kwa watu huku akitoa mfano wa hali ingekuwaje iwapo matukio hayo yangewakuta watoto wa viongozi akiwemo yeye mwenyewe.

Kihampa alichukua uamuzi huo kwa kumwandikia barua Askofu Gwajima juu ya kufutwa kwa kanisa hilo na nakala kuituma kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura ili kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.

“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 17(b) cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 2019 kilichoifanyia marekebisho kifungu cha 2 cha Sheria ya Jumuiya.

Related Posts