ZECO yazidai Sh73 bilioni taasisi za Serikali, binafsi, wawakilishi waingilia kati

Unguja. Wakati Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) likidai deni la Sh73.7 bilioni kutoka kwa wateja wake, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameonesha mshangao wao kutokana na deni hilo kubwa kudaiwa na mashirika yenye uwezo kifedha, huku wananchi wakikumbwa na adhabu ya kukatiwa huduma za umeme wanaposhindwa kulipa.

Wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji, Nishati na Madini leo  Juni 3, 2025, baadhi ya wawakilishi wameitaka Serikali kuandaa mpango madhubuti wa kukabiliana na changamoto ya madeni makubwa, wakisisitiza kuwa kiasi hicho kikubwa cha fedha kingetumika kuboresha miundombinu ya umeme.

Awali, wakati akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri Shaibu Hassan Kaduara hakutaja kwa undani deni hilo, ila alifafanua kuwa ni  la hadi Machi mwaka huu.

Kati ya deni hilo, Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa), taasisi ya Serikali, inadaiwa Sh52.684 bilioni; taasisi nyingine za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano (SMT) zinadaiwa Sh13.107 bilioni, huku wateja binafsi wakidaiwa Sh7.980 bilioni.

Kati ya fedha hizo, Zawa ambayo ni taasisi ya Serikali wanadaiwa Sh52.684 bilioni, taasisi nyingine za SMZ na SMT,  zinadaiwa Sh13.107 bilioni huku wateja binafsi wakidaiwa Sh7.980 bilioni.

Amesema hali hiyo inatokana na utaratibu usioepukika wa kutumia umeme kabla ya malipo.

“Wateja wengine hushindwa kulipa ankara zao za matumizi ya umeme kikamilifu na kwa wakati, jambo linalosababisha mkusanyiko wa madeni kwa shirika la umeme,” amesema  Kaduara.

Akichangia bajeti hiyo, Mwakilishi wa Kiwani, Mussa Foum Mussa amesema kiwango hicho ni kikubwa na kinashoshangaza zinadaiwa taasisi za Serikali na binafsi ambao wana uwezo wa kifedha ikilinganishwa na wananchi wanyonge.

“Kwa masikitiko makubwa wanaodaiwa ni mashirika makubwa yenye uwezo, lakini wananchi wanyonge hawadaiwi hii inakuwaje kwa nini ikitokea kwa wananchi asipolipa hapati huduma na huku madeni yanaendelea kulimbikizwa,” amehoji.

Ameitaka Wizara ya Maji, Nishati na Madini kueleza mikakati itakayotumika kukusanya madeni hayo, pamoja na mpango maalumu wa kuhakikisha madeni hayaendelei kukusanywa, kwani wananchi wana haki katika malalamiko yao.

Hoja kama hiyo imetolewa na mwakilishi wa Ziwani, Suleiman Makame Ali ambaye amesema inawezekena vipi mwananchi wa hali ya chini alipe, lakini taasisi kubwa zinashindwa kulipa.

Amesema jambo hilo haliingia akilini, “Kwa hiyo ufike wakati sasa hizi taasisi ziondolewe kwenye malipo zipewe bure umeme kuliko kuendelea kama hivi ilivyo maana tatizo hili sio la leo wala jana.”

Mwakilishi wa Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu amesema shirika la umeme haliwezi kuendelea kwa kiwango hicho cha madeni  maana kimekuwa kikubwa zaidi huku akiishauri wizara kuweka mita za kulipia kabla ya kutumia kwa wateja hao ili kuepusha changamoto hiyo.

Mwakilishi wa Uzini, Haji Shaaban Waziri ameitaka wizara kuzisisitiza taassi hizo zilipe madeni yake huku mwakilishi wa Tunguu, Simai Said akisema licha ya madeni hayo bado kuna changamoto kubwa ya umeme na kuumiza wananchi.

“Tuje na mawazo na utaratibu tofauti maana hali itaendelea kuwa mbaya zaidi,” amesema.

Katika ushauri wake Simai ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, amesema ifike wakati wawekezaji wa hoteli wanapokuja kuwekeza kila mmoja aje na mpango wake wa kuzalisha umeme mbadala badala ya kuendelea kutegemea umeme wa Serikali.

“Hoteli unakuta ina vyumba 300 bado iendelee kutegemea umeme wa Serikali, hapa tutakwama, kwa hiyo wizara ijipange, shirika liajiri watu wenye uwezo ambao watakuwa na mawazo mapya badala ya kuendelea kuwa na mawazo yaleyale,” amesema.

Related Posts