Nairobi. Ukistaajabu ya Mussa, utayaona ya Firauni, methali hii yaonekana kudhihirika katika kisa cha kusikitisha cha Rosanna Kathure kutoka Meru, Kenya, ambaye alikumbwa na kadhia ya kupigwa vibaya na mumewe hadi kufikishwa chumba cha kuhifadhia maiti kwa kudhaniwa amefariki dunia.
Akihojiwa na Tuko News ya nchini Kenya leo, Juni 4, 2025, mwanamama huyo amesimulia kuwa alimfumania mumewe akiwa kitandani kwao (yeye na mumewe) na mwanamke mwingine, jambo lililozua hasira na kusababisha mwanamume huyo kumshambulia kwa kipigo katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.
“Alinipiga hadi nikazimia kabisa na kupelekwa hospitali nikiwa hoi. Baadaye, nilipelekwa mochwari ambako niliandikishwa jina kwenye paji la uso na kuwekwa pamba puani, kwa kuwa walidhani tayari nimefariki dunia,” amesimulia kwa uchungu.
“Nilimfuma mume wangu akiwa na mwanamke mwingine kitandani kwetu, nilipowakamata, mwanamke huyo alikimbia huku mume wangu akiwa anavaa nguo bila mpangilio, sikumpandishia sauti nilikuwa nikimueleza kwa upole.
“Baadaye nilidhani ameondoka kumbe alikuwa amejificha nyuma ya nyumba akasubiri muda nimelala na watoto akaingia akamulika na tochi nikamuuliza nani wewe akasema mimi mume wako,” amesimulia.
Amesema baada ya majibizano mafupi alianza kumshambulia kwa kitu chenye ncha kali: “Alinikata usoni, kichwani, tumboni na mguuni, majirani wakaja baada ya kipigo kuzidi na kelele,” amesimulia.
Rosanna amesema alijeruhiwa na kuvuja damu na alipelekwa hospitalini akiwa hajitambui ambapo alidaiwa amefariki tayari na alipelekwa mochwari kama maiti.
“Kwanza walinipeleka katika Hospitali ya Maua, lakini madaktari walipoona sitikisiki, wakanihamishia Hospitali ya Meru Level 5. Huko mara moja walinipeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ambako nilikaa kwa siku tatu kabla ya kuokolewa siku ya nne.
“Wazazi wangu walikuwa tayari wamepewa taarifa ya kuja kuwachukua watoto wangu kwa sababu nilikuwa nimekufa. Hata hivyo, walitaka kufika hospitali kuthibitisha habari hizo,” amesimulia Rosanna.
Rosanna amedai walikuwa wamemuwekea pamba mwilini, wakiamini kuwa hana uhai. Jina la Rosanna na jina la baba yake lilikuwa limeandikwa kwenye paji la uso wake alipokuwa amelala kwenye chumba baridi kati ya wafu.
Kwa mujibu wa Rosanna, alinusurika kwa miujiza baada ya mama mmoja, aliyekuwa akitafuta mwili wa binti yake katika mochwari hiyo, kugundua kuwa bado alikuwa hai.
“Kulikuwa na mwanamke mmoja wa Kikuyu kutoka Nanyuki aliyekuja kuchukua mwili wa binti yake. Baada ya kuutoa, aliniona nikiwa nimelala sakafuni.
“Aliposogea karibu, aligundua kuwa moyo wangu bado unadunda, ndipo akatambua kuwa kuna mtu ambaye bado yu hai ndani ya chumba cha maiti.
“”Mama huyo, pamoja na wengine waliokuwepo, walimjulisha daktari kuhusu hali yangu. Ingawa awali alikuwa na shaka, alikuja kuniangalia na kuthibitisha kuwa kweli bado nilikuwa hai.
“Baada ya hapo, walinitoa kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti na kunipeleka wodini kwa ajili ya matibabu,” amesema.