Dar es Salaam. Mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Eugine Kabendera ametangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikiwa ni wiki moja tangu alipotangaza kujiondoa katika chama chake cha awali.
Kabendera alitangaza kukihama Chaumma, wiki iliyopita akitaja sababu za uamuzi wake huo ni kutoridhishwa na mwenendo wa kilichokuwa chama chake, akisema kimekiuka misingi yake.
Kabendera kabla ya kujiunga na Chadema, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Bara na nafasi nyingine kadhaa za kitaifa.
Mwanasiasa huyo amepokewa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa aliyesema Kabendera amekataa biashara yoyote inayoendelea nchini, kinyume na masilahi ya Taifa.
Akizungumza baada ya kupokewa, leo Jumatano, Juni 4, 2025 Kabendera amesema amegundua mwelekeo wa chama chake cha awali haukuwa unaendana na imani, maono na dhamira ya Taifa.
Kabendera amesema hakuingia kwenye siasa kwa ajili ya vyeo, badala yake aliingia kuhudumu na anapoona misingi hiyo inatikiswa na kutikisika hivyo ameona wajibu wa kuchukua hatua muafaka.
“Baada ya mashauriano ya kina na kutafakari nimeamua kujiunga na Chadema, huu sio uamuzi rahisi wala masilahi ya kisiasa. Ni uamuzi uliotokana na mshikamano wa kweli,” amesema.
Amesema ni imani yake kuwa Chadema inatoa jukwaa la mabadiliko ya kweli hasa ndoto za jamii zilizotengwa, akisisitiza uamuzi wake umekuwa kwa ajili ya wananchi.
Kabendera ni mwanasiasa na alikuwa kiongozi wa Chaumma ambapo nafasi yake ya mwisho ya uongozi kwenye chama hicho alikuwa msemaji wa chama hicho.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, aligombea ubunge katika Jimbo la Ubungo kupitia tiketi ya Chaumma, lakini lishindwa katika kinyang’anyiro hicho.