BARAZA LA MZEE SALIM: Dharau ni miongoni mwa sumu mbaya ya uchaguzi

Miongoni mwa mambo ambayo athari zake ni kubwa kwa maisha ya mtu binafsi, jamii na taifa kwa ujumla ni dharau, au kwa maneno mengine, kupuuza mambo ya msingi, hasa yale yanayohatarisha maisha na usalama wa watu.
Siku hizi, imekuwa jambo la kawaida kwa baadhi ya madereva wa magari, waendesha pikipiki na baiskeli kupuuza taa nyekundu za barabarani, wakikiuka sheria kwa makusudi hata mbele ya watembea kwa miguu.
Wengine huzidisha hatari kwa kutokuzima injini wanapoweka mafuta, kutumia simu au hata kuvuta sigara katika vituo vya mafuta, licha ya maonyo yaliyowazi kuhusu hatari za tabia hizo.
Wako pia wanaochoma mahindi, kukaanga viazi au chipsi kwa karibu mno na vituo vya mafuta, hili pia ni jambo la hatari linalodhihirisha dharau isiyosahaulika.
Si kwamba watu hawa hawafahamu hatari hizo, bali ni uamuzi wa kupuuza kwa makusudi.
Kwa kutambua madhara ya dharau, wahenga walituasa kwa busara: “Mdharau mwiba mguu huota tende” au “Asiyesikia la mkuu huvunjika mguu.”
Kwa maneno hayo, walituonya kuhusu kupuuza maonyo au dalili za hatari, jambo linaloweza kuzaa majuto makubwa.
Mtunzi maarufu wa fasihi, Said Mohamed, aliwahi kuwaelezea watu wa aina hii kuwa ni “Mti mkavu”, yaani watu walioishiwa fikra sahihi na mantiki.
Kwa masikitiko makubwa, hali kama hii ya dharau inaonekana pia katika mazingira ya kisiasa ya Zanzibar, hasa tunapoelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.
Ni kawaida kwa kipindi hiki kuwa wakati wa hofu kwa watu wengi wa Zanzibar, kutokana na historia ya machafuko, vipigo, ulemavu na hata vifo vinavyotokea wakati wa chaguzi.
Tunasonga mbele huku kumbukumbu za yaliyopita bado zikiwa hai kwa wengi wetu.
Cha kushangaza, hakuna dalili madhubuti zinazoonyesha kuwa juhudi za makusudi zimechukuliwa ili kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa huru, wa haki na wa amani.
Dhihaka hii ya wazi kwa hali halisi iliyopo ni kama kudharau si tu mwiba, bali misumari na vigae na badala ya kuota tende, huenda tukashuhudia watu wakipoteza miguu au maisha yao kabisa.
Kila uchao, viongozi wa upinzani hasa wa chama cha ACT-Wazalendo, wanalalamikia hali ya kutokuwa na mazingira huru ya uchaguzi, wakidai njama zinazolenga kuvuruga uchaguzi wa haki.
Wamesisitiza kuwa hawatakubali sauti ya wananchi ipuuzwe au kudhalilishwa katika visanduku vya kura.
Malamiko hayo yanajumuisha tuhuma dhidi ya polisi kwa kutengeneza mazingira ya kuwatisha watu katika vituo vya kuhakiki majina yao.
Wengine wanasema walizuiwa kuangalia majina ya wapiga kura wengine, jambo ambalo ni kinyume na sheria za uchaguzi, kwa sababu kila Mzanzibari ana haki ya kuweka pingamizi dhidi ya mtu asiye na sifa za kupiga kura.
Iwapo uhuru wa kuchambua daftari la wapiga kura unazuiwa, inawezekanaje kuweka pingamizi kwa wanaodaiwa si Wazanzibari halali au waliojiandikisha zaidi ya mara moja?
Zaidi ya hapo, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), bado haijatoa maelezo ya wazi juu ya kwa nini uchaguzi umepangwa kufanyika kwa siku mbili, ilhali katiba inatamka wazi kuwa ni uchaguzi wa siku moja. Ukimya wao ni kama dharau kwa malalamiko halali ya wananchi.
Taasisi za kiraia zilialikwa kuomba vibali vya kutoa elimu kwa wapiga kura, lakini hali ya mchakato huo haijulikani na kuna madai ya upendeleo katika utoaji wa vibali hivyo, pamoja na vile vya waandishi wa habari.
Dharau hizi hazina mwisho mwema kwa uchaguzi huu wala kwa mustakabali wa Zanzibar.
Viongozi wa Tume, serikali na vyama vya siasa wanapaswa kutambua kuwa wananchi wamechoka na machafuko, manyanyaso na dhuluma ya maisha inayorudiwa kila baada ya miaka mitano.
Ikiwa mataifa mengine, ambayo zamani yalikuwa na migogoro ya kisiasa, sasa yamepiga hatua na kuwa na chaguzi zenye heshima na amani, ni nini kinachoshindikana kwa Zanzibar?
Narudia kwa msisitizo: dharau inayoonyeshwa sasa inaweza kuzaa majuto makubwa kama ilivyotokea katika chaguzi zilizopita.
Njia ya pekee ya kulinda amani na haki ni kuchukua tahadhari mapema, kuondoa kila aina ya mizengwe, na kuhakikisha kila hatua ya uchaguzi inaaminika na inaheshimiwa na pande zote.
Tuache dharau, tusimame na haki, ili tuweze kuvuka salama kipindi hiki kigumu na kuijenga Zanzibar yenye amani, heshima na matumaini kwa wote.
Kama Wazanzibari wote watakubaliana na haya niyasemayo, ni wazi tutavuka salama katika kipindi hiki kizito.

Related Posts