Heshima ndiyo msingi wa chama imara

Wiki hii nilipata fursa ya kuhudhuria Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika Dodoma.

Katika mkutano huo, ilipitishwa rasmi ilani mpya ya CCM kwa kipindi cha Mwaka 2025–2030. Kati ya mambo makubwa yaliyomo kwenye ilani hiyo, lililonigusa zaidi ni azma ya chama kuendelea na mchakato wa kupata Katiba mpya.

Jambo hilo limekuwa gumzo kubwa kwenye vyombo vya habari kwa muda mrefu sasa. Hata hivyo, leo sitazungumzia kuhusu ilani hiyo; badala yake, napenda kugusia jambo jingine muhimu nililoliona, ambalo kwa mtazamo wangu, halina tija kwa chama wala taifa.

CCM ni chama kinachoongozwa na misingi na imani thabiti. Moja ya imani kuu za CCM ni kwamba binadamu wote ni sawa.

Kila mtu bila kujali nafasi yake, anastahili heshima, utambuzi na kuthaminiwa utu wake. Hii ina maana kwamba, ndani ya chama, viongozi na wanachama wa kawaida wanapaswa kuhesabika sawa , wote wakiwa na heshima ya kipekee.

Hata hivyo, kwa siku za karibuni, kumekuwa na dalili za kuibuka kwa kauli za kudhalilisha watu, kuwaita majina mabaya na kupuuzia utu wa wengine.

Hili si jambo zuri kwa chama chenye historia ndefu kama CCM na siyo afya kwa mustakabali wa taifa letu.

Makala hii inalenga kuikumbusha jamii kuwa heshima si bidhaa ya kununua, ni zawadi ya bure inayojengwa katika mawasiliano na uhusiano wa kila siku.

Mkubwa amheshimu mdogo na mdogo naye amheshimu mkubwa. Viongozi wa ngazi za juu wawaheshimu viongozi wa ngazi za chini na wanachama wa kawaida, vivyo hivyo wanachama waheshimu viongozi wao. Hata pale inapotokea kuna tofauti za hoja au ukosoaji, heshima ibaki mstari wa mbele.

Nguvu ya CCM ipo kwa watu wake. Wanachama wa CCM ndio msingi wa chama hicho; hawa ndio wenye mamlaka ya mwisho kupitia vikao kama Mkutano Mkuu.

Mwananchi yeyote wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi anayeikubali imani, malengo na madhumuni ya CCM, anaweza kuwa mwanachama. Lakini kuwa mwanachama si kuwa na kadi tu, bali ni pamoja na kutimiza masharti muhimu.

Na masharti hayo ni pamoja na kuwa mtu anayeheshimu watu, anayeielewa, kuieleza na kuitekeleza itikadi na siasa ya CCM, anayeamini kazi kama kipimo cha utu.

Lakini pia awe mtu anayeshirikiana na wenzake na kuwajibika katika utekelezaji wa masuala ya umma sambamba na kuwa mfano wa tabia njema na uaminifu na awe na shughuli halali ya kujiingizia kipato.

Kwa maana hiyo, mwanachama yeyote anayo haki ya kushiriki katika shughuli za chama, kutoa maoni kwenye vikao, kuomba uongozi, kujitetea pale inapohitajika na hata kumuona kiongozi yeyote wa CCM kwa kufuata utaratibu.

Lakini hakuna haki bila wajibu. Kila mwanachama ana wajibu wa kulinda umoja wa chama, kukemea chuki na dhuluma, kushiriki katika kuondoa umasikini, ujinga na maradhi, kujielimisha na kuwa tayari kukosolewa na kujikosoa muda wowote ule.

Moja ya nguzo muhimu ndani ya CCM ni haki ya kukosoa na kukosolewa. Hata hivyo, ukosoaji huo unapaswa kufanywa kwa staha, lugha ya heshima na siyo matusi au dhihaka.

Vivyo hivyo, viongozi wa chama wanapaswa kujibu hoja kwa hoja, si kumshambulia mkosoaji au kumvunjia heshima.

Tumeona mara nyingi mwanachama akikosoa hadharani, anaitwa kwenye kikao cha maadili na kupewa onyo au hata kufukuzwa uanachama.

Hivyo ni muhimu kukumbuka kwamba kiongozi ni mwanachama tu aliyepewa dhamana; hana ubora wa asili kuliko wengine. Kwa maana hiyo, anastahili kuheshimiwa lakini pia ana wajibu wa kuheshimu wenzake, hasa wanapotoa hoja.

Viongozi wanapaswa kuwa na “ngozi ngumu,” kama mzazi anavyovumilia makosa ya mtoto wake. Wakati mwingine watoto ni watundu, wasumbufu, au wachokozi, lakini mzazi humrekebisha mtoto wake kwa upendo, si kwa kumvunjia utu.

Vivyo hivyo kwa wanachama wanaopitiliza kwa lugha au matendo, wanapaswa kurekebishwa si kudhalilishwa. Kuwaita majina mabaya hakujengi, bali kunavunja.

Tukumbuke kuwa nguvu ya CCM na hatma ya taifa hili zipo mikononi mwa watu wake. Tunapolinda heshima, tunalinda msingi wa umoja, mshikamano, na maendeleo. Tufanye ukosoaji kwa staha, tuendelee kujenga chama imara na taifa lenye mshikamano.

Kwa sababu mwishowe, taifa hili ni la Watanzania wote na mustakabali wa Tanzania unamtegemea kila mmoja wao kuheshimiana, kusikilizana na kushirikiana kwa ujenzi wa kesho iliyo bora zaidi ya leo.

Related Posts