Dar es Salaam. Wakili, Peter Kibatala ameeleza alipo Askofu Josephat Gwajima ambaye tangu usiku wa kuamkia Juni 3, 2025, Jeshi la Polisi lilipovamia kanisani kwake Ubungo, Dar es Salaam, hajaonekana.
Askofu Gwajima mara ya mwisho alionekana akiwa kanisani hapo jioni ya Juni 2, 2025 ikiwa ni siku ya kwanza ya maombi pamoja na kufunga yaliyopangwa kufanyika kwa siku saba.
Hata hivyo, maombi hayakuweza kuendelea kanisani hapo kufuatia ulinzi wa Polisi waliokuwa wamezingira eneo lote la kanisa.
Kanisa hilo mpaka sasa limezungushiwa utepe wa njano wenye maandishi meusi, likiwa chini ya ulinzi wa polisi na hakuna muumini anayeruhusiwa kusogea, tangu alfajiri ya kuamkia Juni 3, 2025.
Juni 2, 2025, Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa alitangaza kulifuta kanisa hilo kutokana na kukiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kwa kile alichokieleza ni kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.
Tangu kuzungushiwa utepe kanisa hilo na kuwa chini ya ulinzi wa polisi wenye silaha na gari ya maji ya kuwasha, waumini wanakusanyika upande wa pili wa barabara wakitaka kujua ni wapi alipo kiongozi huyo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Juni 4, 2025 wakili wa Askofu Gwajima, Peter Kibatala amesema mbunge huyo yupo mahali salama.
“Mteja wangu (Askofu Gwajima) hashikiliwi (hajakamatwa), yuko wapi ni suala ambalo siwezi kulitolea maelezo kwa sababu mbalimbali.”
“Ambacho naweza kukithibitisha hadi muda huu (saa 7:15 mchana wa Juni 4, 2025) hashikiliwi, yupo salama, hajakamatwa,” amesema Kibatala.
Amesema kuna mambo wanayoendelea kuyafanya na Askofu Gwajima kuhusiana na hatua kadhaa za kisheria baada ya hatua ya msajili.
“Kwa sasa itoshe kusema hashikiliwi, yupo salama,” amesema.
Kushughulika na Polisi wanaolinda kanisa
Akizungumzia ulinzi unaoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi, makao makuu ya kanisa hilo eneo la Ubungo Kibo jijini Dar es Salaam, Kibatala amesema tayari wameanza taratibu za kisheria juu ya suala hilo.
“Hayo wanayoyafanya, wanafanya kwa misingi gani ya kisheria? kama polisi wanatekeleza kinachoitwa kufutwa kwa kanisa, hakuna kitu hicho,” amesema wakili huyo.

Kibatala amesema kama taarifa ya kufungiwa kwa kanisa ni ile inayosambaa kwenye mtandao, basi kuna upungufu kisheria.
“Wao wamefuta kanisa linaitwa Glory of Christ Church, kanisa la mteja wangu (Askofu Gwajima) linaitwa Glory of Christ Tanzania Church, kuna changamoto za kisheria na kimantiki,” amesema.
Amedai mteja wake, hajaambiwa chochote, wala hawajapewa barua na mtu yeyote kuhusu kufutwa kwa kanisa akidai utaratibu wa kisheria ni mteja wake kupewa barua, utaratibu ambao anadai haujafanyika huku akihoji polisi wanaolinda kanisa hilo wanafanya nini pale.
“Suala la Polisi kuwa pale tunalishughulikia kisheria, walioko pale wako pale kwa hicho kinachoitwa kufutiwa usajili, lakini ni kifaa kazi gani kilitumika kufuta usajili? ni hiyo barua inayosambaa kwenye mitandao au kitu kingine? Amehoji.
Amesema utaratibu wa kisheria kuhusu Polisi kulinda kanisa hilo umeshaanza kufanyika Dar es Salaam na Dodoma.
Kibatala amegusia pia baadhi ya waumini waliokamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi Oysterbay wakati wa purukushani kati yao na polisi zilizotokea Juni 2, 2025 wakiwa kwenye maombi kanisani hapo.
“Ilibidi tugawane majukumu, wengine kushughulikia mambo ya huko Oysterbay, wakili Ikoti Lissu na viongozi wengine wa kanisa wapo pale ili hao watu (waumini waliokamatwa) wapate dhamana na mambo mengine ya kisheria,” amesema.
Hata hivyo, amesema idadi kamili ya waliokamatwa bado hajathibitishwa, japo alimbiwa na kanisa ni watu 80.
“Hata hivyo saa 10 jioni tutatoa taarifa rasmi ya watu wangapi walikamatwa, wangapi wameachiwa,” amesema.
Katika eneo la kanisa hilo hadi kufikia leo Juni 4, 2025 saa 5:14 asubuhi, utepe uliokuwa umezungushwa ulikuwa umesogezwa.
Jana utepe huo ulikuwa umezungushwa hadi kwenye eneo la barabara (service road) ya upande wa kanisa, kabla ya leo Mwananchi kushuhudia ukiwa umeondoshwa barabarani na kuishia kwenye nguzo iliyo jirani na lango kuu la kuingilia kanisani.
Gari la maji ya kuwasha ambalo jana Jumanne lilikuwa limeegeshwa mwanzoni, limesogezwa hadi kwenye parking ya kanisa hilo ambako kuna magari mengine binafsi, ambayo yamekumbwa na kadhia ya kuzungushiwa utepe wakati wa purukushani.
Hata hivyo waumini wamepungua, wakisalia wachache kulinganisha na wale waliokuwepo jana, huku wachache waliopo ambao hutambuana kwa kusalimiana salamu ya…majeshi… majeshi wakiwa na matumaini ya kurudi kuendelea na maombi, licha ya ulinzi unaoendelea kuimarishwa na Polisi wenye silaha kanisani hapo.