Kilio cha wanawake wasakao uongozi Zanzibar, ZEC yajibu

Unguja. Oktoba mwaka huu, Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu wake ambao utawachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Hata hivyo, kuna changamoto kubwa inayojitokeza kila uchaguzi unapowadia ya ushiriki mdogo wa wanawake, hasa visiwani Zanzibar, ukilinganisha na wanaume.

Sababu moja kubwa inayotajwa mara kwa mara ni hali duni ya uchumi. Mchakato wa uchaguzi kuanzia kuchukua fomu, kufanya kampeni hadi kufanikisha ushindi, inahitaji fedha nyingi.

Kwa wanawake wengi ambao kiuchumi hali yao ni duni ukilinganisha na wanaume, hukwama na kimekuwa kizuizi kikubwa kinachowakwamisha kushiriki kikamilifu kwenye kuomba nafasi za kugombea.

Ripoti ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya mwaka 2020 inaeleza kwa undani hali hiyo. Kati ya wagombea 601 waliochukua fomu kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo, wanawake walikuwa 135 tu, sawa na asilimia 22.4 pekee ya wagombea wote.

ZEC imeandika, wanawake walioweza kushinda katika ushindani wa moja kwa moja walikuwa ni 37 pekee kati ya nafasi 160 za udiwani na uwakilishi zilizokuwa zinagombewa.

Hii ni idadi ndogo sana, ikizingatiwa wanawake wako zaidi ya nusu ya idadi ya watu wa Zanzibar.

Inaelezwa kuwa changamoto hiyo haiwezi kupuuzwa. Ni wazi kuwa kuna haja ya kuweka mikakati mahsusi ya kuwawezesha wanawake kiuchumi ili waweze kushiriki kwa usawa kwenye siasa na uongozi.

Akizungumzia hilo, Naima Salum Hamad kutoka chama cha UDP alipozungumza na Mwananchi, amesema kama mwenendo huo utaendelea, ni wazi itaendelea kushuhudiwa wanawake wachache wakijitokeza kugombea hai inayopoteza nguvu kubwa ya uongozi na maono ambayo yangelisaidia kulijenga Taifa.

Anasema kadiri uchaguzi wa Oktoba unavyokaribia, ni muhimu wadau mbalimbali, serikali, mashirika ya kiraia na vyama vya siasa, kuangalia kwa jicho la huruma na nia ya dhati jinsi ya kuondoa vikwazo vinavyowafanya wanawake waendelee kubaki nyuma katika mchakato huo wa kidemokrasia.

“Kwa sababu taifa imara linajengwa na ushiriki wa wananchi wake wote, wanaume kwa wanawake, basi lizingatiwe,” anasema Naiman.

Kwa mujibu ZEC, gharama zilizokuwepo katika uchaguzi wa mwaka 2020, mgombea wa nafasi ya udiwani alitakiwa kulipa ada ya Sh10,000 pamoja na dhamana ya Sh50,000.

Kwa upande wa nafasi ya uwakilishi, ada ilikuwa Sh50,000 na dhamana Sh300,000, huku nafasi ya urais ada ilikuwa Sh100,000 na dhamana ya Sh2 milioni.

Baadhi ya wanawake ambao wamewahi kukutana na changamoto hiyo, wanasema sio tu inakwamisha usawa wa kijinsia, lakini inawafanya wajione wanyonge.

Naima anasema asilimia kubwa ya wanawake hawana rasilimali fedha, hivyo hutegemea huruma, jambo ambalo linakuwa gumu katika ushindani wa kisiasa.

Hata hivyo, anasema pamoja na kukosa fedha lakini ni vyema wanawake kushiriki katika nafasi hizo bila kukata tamaa na wanapaswa kuungana mkono.

“Unapokosa fedha, unapata woga na hii ndio changamoto kubwa kwetu sisi wanawake, kwa hiyo unatakiwa ujiamini kwa sababu kuna misukosuko inayotokea kama ya kudharaulika lakini unasonga mbele,” amesema.

Amesema licha ya kwamba hana fedha, ameshawahi kugombea zaidi ya mihula mitatu katika majimbo tofauti bila kukata tamaa. Miongoni mwa majimbo aliyorusha karata ni pamoja na Donge, Mfenesini na anasema safari hii anatarajia kuomba kugombea urais wa Zanzibar, mchakato wa chama utakapoanza.

Ametoa rai kwa ZEC kuwapigia chapuo wanawake wenye nia ya kusaka uongozi hata kwa kuwapatia nafasi za upendeleo kutokana na mazingira na uwezo wao.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ADC Zanzibar, Mtumwa Faiz Sadiki amesema licha ya kukiri changamoto ya ukata wa fedha kwa wanawake, anakwenda mbali zaidi akisema changamoto hiyo inawakuta zaidi wanawake wanaotoka kwenye vyama vichanga ambavyo pia vinakosa hata fedha za kuwadhamini.

Mtumwa anasema wanawake ni jeshi kubwa na wanatamani siku zote wapeperushe bendera za vyama vyao kupitia nafasi mbalimbali ikiwemo ya urais.

“Lakini ndiyo hivyo, changamoto zinatukwamisha, fedha nyingi zinazowekwa na Tume ya uchaguzi, hata mimi kama nina milioni mbili nitaenda kununua kabati sitaweza kuipeleka huko kwa sababu sina uhakika wa kuireejsha,” amesema Mtumwa.

Anasema mwaka 2015 aligombea ubunge jimbo la Mfenesini, alipoenda kugonga muhuri fomu yake Mahakama ya Kwerekwe, alikutana na mwanamke (hakumtaja) ambaye alitia nia ya kugombea nafasi ya Urais lakini hakuwa na fedha, akashindwa.

“Wapo (wanawake) wanaoweza kugombea, lakini wanashindwa kwenye ada, lakini kama viwango vinapungua watakuwa na nafasi kubwa ya kugombea katika nafasi hizo,” amesema.

Hata hivyo kutokana na kelele nyingi za wadau, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imeingilia kati na kupunguza asilimia 50 ya kwa wanawake wanaotaka kugombea Urais, uwakilishi na udiwani watakaosimamishwa na vyama vyao.

Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi amesema punguzo hilo halitahusisha nafasi ya viti maalum kwa nafasi ya uwakilishi na udiwani, bali ni kwa wagombea wanawake majimboni na urais wa Zanzibar.

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Thabit Idarous Faina amesema ZEC imetoa punguzo hilo baada ya malalamiko ya wanawake kuhusu kiwango cha fedha kilichoweka kwa ajili ya uchukuaji wa fomu nafasi ya urais, uwakilishi na udiwani.

Amesema Tume ilipokea malalamiko na ushauri uliokuwa ukitolewa na wanaharakati wa kutetea haki za wanawake, hivyo ZEC kupitia kanuni yake ya uchaguzi ya mwaka huu imetoa punguzo hilo ikiwa chama kitasimamisha mgombea mwanamke.

“Hatua hii itawapa fursa wanawake kufikia malengo yao ya kugombea katika majimbo kwa uchaguzi mkuu unaokuja,” amesema Faina

Hata hivyo, amesema, ZEC itawahamasisha wanawake wengi kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kutokana na punguzo hilo.

Kwa upande wake, Asma Ali Makame kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Vijana Mikunguni (MYDO), amesema kuna idadi kubwa ya wanawake wapiga kura, kama wangeungana mkono wakapata nafasi nyingi.

Anasema wanawake mara nyingi hujitokeza kwa wingi kwenye kupiga kura pekee, lakini si watu ambao huingia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Hivyo, ameiomba ZEC kuchukua takwimu kwa ajili ya kufanya maboresho yatakauosaidia kuwahamasisha wajitokeze kwa wingi.

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa – Zanzibar), Dk Mzuri Issa amesema wanafarijika kuona ZEC sasa ikichukua hatua chanya za kuwasaidia wanawake.

Dk Mzuri amesema hicho ni kilio walichokuwa nacho wanawake kwa muda mrefu sasa.

“Kwa muktadha huo, uamuzi wa ZEC wa kupunguza nusu gharama katika uchaguzi wa mwaka huu ni hatua itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kuwahamasisha wanawake kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema Dk Mzuri.

Amesema Tamwa ZNZ inawahamasisha wanawake wote walio na sifa za kugombea kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo muhimu na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu ujao.

Related Posts