Dar es Salaam. Kampuni ya Mamba Minerals Limited inayowekeza kwenye mradi wa madini adimu imeweka wazi mpango wake wa kujenga kiwanda cha kusafisha na kuongeza thamani madini adimu kijijini, Ngwala mkoani Songwe, badala ya kuyasafirisha yakiwa ghafi.
Hayo yamesemwa leo Juni 4, 2025 Kijijini Ngwala, Songwe wakati wa uzinduzi wa ulipwaji fidia kwa wananchi 192 waguswa wa mradi huo.
Akitoa maelezo ya awali mbele ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mamba Minerals Ltd, Ismail Diwani amesema ulipaji wa fidia utagharimu Sh5.3 bilioni ukihusisha wananchi 192 na mpaka sasa wananchi 116 wamepokea malipo yao tayari.

“Hatua hizi ni za awali kuelekea kwenye utekelezaji wa mradi ambapo shughuli rasmi za ujenzi zitaanza Desemba 2025 sambamba na ujenzi wa kiwanda cha kusafisha madini adimu na ujenzi wa mtambo wa kufua umeme utakaozalisha megawati 12,” amesema Ismail.
Wakati wa uzinduzi huo Waziri Mavunde ameipongeza kampuni hiyo kwa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha madini hayo hapa nchini, ikiwa ni uongezaji wa thamani wa kabla ya kusafirishwa ikiwa ni sehemu ya kuitikia wito uliotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan juu ya uongezaji thamani madini nchini.