Majaliwa ataka TBS iende viwanda kudhibiti ubora

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelielekeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuanza kudhibiti ubora wa bidhaa moja kwa moja viwandani badala ya kusubiri bidhaa kukamilika kwa ajili ya ukaguzi.

Akizungumza leo, Juni 4, 2025, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la jengo jipya la TBS jijini Dodoma, Majaliwa amesema hatua hiyo itasaidia kuzuia uingizaji wa bidhaa hafifu sokoni na kumlinda mwekezaji dhidi ya hasara.

“Badala ya kusubiri bidhaa zizalishwe ndipo mkaanze kuzikagua, nendeni viwandani mkadhibiti huko huko. Ili pia hata mwekezaji asipate hasara kwa kuzalisha bidhaa isiyokuwa na ubora. Muanze kumjulisha mapema kama bidhaa yake ni bora au la, ili aendelee au asiendelee kuzalisha,” amesema Majaliwa.

Amesisitiza kuwa Serikali haitaki Tanzania iwe shimo la bidhaa hafifu, bali inataka soko la ndani liwe na mvuto kwa watumiaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema jengo linalojengwa lina viwango vya kisasa na litakuwa na maabara kubwa itakayosaidia kupunguza usumbufu wa kusafirisha sampuli za bidhaa kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo.

“Jukumu kubwa la TBS ni kuhakikisha Tanzania inaheshimika katika masuala ya viwango,” amesema Dk Jafo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ashura Katunzi amesema ujenzi wa jengo hilo unagharimu Sh25.3 bilioni na hadi sasa umefikia asilimia 76 ya utekelezaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kutokubali kushiriki matendo yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi wakati wa uchaguzi, akisisitiza kuwa athari za kuvuruga amani ni kubwa na huleta majuto.

“Tunapotaka kushika nafasi kuna kushindana, nawasihi ushindani wetu uzingatie tunu ya Taifa ya amani na utulivu. Kumekuwa na dalili za kuvuruga usalama kila tunapokaribia uchaguzi. Ni muhimu kila mmoja akatafakari — kwa nini haya hujitokeza kila mwaka wa uchaguzi?” amesema.

Amesema viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kuhubiri amani na kuhakikisha wagombea wanaotaka madaraka wanachujwa kwa umakini ili kuepusha vurugu na migawanyiko isiyo ya lazima.

“Nchi ni yetu sote. Tunapokaribia mwezi wa 10, kila mwaka kunaanza kujitokeza mambo ya ovyo kabisa. Watu wajitafakari, wasikubali kutumiwa vibaya,” ameonya.

Related Posts