Mwanza. Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) inatarajia kufanya utafiti wa maji ya Ziwa Victoria ili kujua ubora wake yanayotegemewa na watu milioni 45 kwa nchi za Afrika Mashariki.
Utafiti huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), utaanza hivi karibuni baada ya wataalamu kupewa mafunzo ya siku tatu ya namna ya kuufanya kuanzia leo Juni 4 hadi 6, 2025 kisha kuanza utafiti wa sampuli ya maji ya ziwa hilo upande wa Tanzania.
Akizungumza jijini Mwanza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 4, 2025 Naibu Katibu Mtendaji wa LVBC, Coletha Ruhamya amesema kuna hisia kwamba yapo mambo yasiyo ya kawaida yanayosababisha athari ikiwamo magugu maji ziwani humo.
Hivyo, Ruhamya amesema utafiti huo utaleta majibu yatakayosaidia utunzwaji wa bioanuwai na ikolojia ya bonde la ziwa hilo.
“Sio kwamba tumeona kitu, ila tunahisi kuna mambo ambayo siyo ya kawaida, ukiangalia kwa jicho la kawaida muonekano wa ziwa, namna watu wanavyoongelea magugu maji pia hata ukiangalia shughuli za kibinadamu zinazofanyika kando ya Ziwa Victoria, ukiona maji ni meupe au hayana rangi sio kwamba ni masafi, ndio maana tukasema ngoja tufanye huu utafiti,” amesema naibu katibu mtendaji huyo.
Ruhamya amesema hayo baada ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wa utaalamu, wale watakaofanya utafiti huo.
Amesema licha ya kufahamu ubora wa maji, wanataka kujua hali ya usafi na uchafuzi ndani ya ziwa hilo ili kubuni miradi itakayopunguza kadhia hiyo endapo itabainika.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), Dk Renatus Shinhu amesema utafiti huo utashirikisha nchi za Afrika Mashariki zinazozungukwa na bonde la Ziwa Victoria ikiwamo Tanzania, Kenya na Uganda na kila nchi itapeleka sampuli maabara kwa ajili ya kupimwa.
“Tunaanza na mafunzo kwanza ili watu wajue namna gani tunachukua sampuli za maji kwenye Ziwa Victoria, tunatumia vifaa vipi kwa ajili ya kuchukua hizo sampuli, baada ya mafunzo,” amesema Dk Shinhu.
Amesema baada ya utafiti huo kufanyika, takwimu zitakazopatikana zitasaidia nchi wanachama kuja na miradi itakayotumika kwenye kuboresha na kuimarisha vyanzo vya maji hasa Ziwa Victoria sambamba na kufahamu ubora wa maji yake.

Naibu Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Coletha Ruhamya akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya namna ya kufanya utafiti wa maji ya Ziwa Victoria utakaofanyika nchi ya Tanzania, Kenya na Uganda.
“Kama jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki tunaweza kuja na miradi ipi itakayosaidia kwenye kutunza mazingira ya Ziwa Victoria. Lakini pia inaweza ikasaidia kwenye uboreshaji wa sera kati ya nchi wanachama,” ameeleza.
Akizungumzia hali ya ziwa hilo hususan upande wa Tanzania, amesema kulingana na upimaji wa kila siku unaofanywa na bonde hilo, ni nzuri licha ya pembezoni mwa ziwa kuonekana kama kuna uchafuzi.
Hata hivyo, amesema kadri wanapokielekea kina cha maji kati ya mita 50 hadi 100 kutokea kwenye kingo za maji, ubora unazidi kuimarika, lakini kulingana na shughuli za kibinadamu zinazoendelea zinatishia uhai wa ziwa hilo.
Mshauri wa ufundi kutoka GIZ, Omary Myanza amesema wameamua kufadhili mradi huo ili kupata takwimu na taarifa zitakazosaidia jumuiya hiyo kutatua changamoto zinazolikumba ziwa hilo.
“Tunafadhili kwa sababu takwimu na taarifa zitakazopatikana zitasaidia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na bonde la Ziwa Victoria kuweka mikakati thabiti ya kudhibiti mazingira ya ziwa hilo, tumeona kuna vitu vingi vinajitokeza ikiwamo suala la magugu maji,” amesema.