Mume aliyejaribu kumuua mkewe jela miaka 19

Arusha. Mahakama ya Rufani nchini imepunguza kwa miezi sita kifungo cha Michael Mlelwa, aliyepatikana na hatia ya kujaribu kumuua aliyekuwa mke wake, Ava Kavalukutu kwa kumkata na panga mara tatu kichwani.

Mlelwa sasa atatumikia kifungo cha miaka 19 na miezi sita jela, baada ya awali kuhukumiwa miaka 20 na Mahakama Kuu ya Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea Septemba 1, 2018, katika eneo la Kiwalani, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, baada ya Ava kukataa kulala kitanda kimoja na mumewe kufuatia ugomvi baina yao.

Ava aliamua kulala kwenye sofa, lakini baadaye usiku, Mlelwa aliyekuwa kalala chumbani alitoka na kuja sebuleni alikolala Ava na kumkata kwa panga kichwani mara tatu, kitendo kilichoshuhudiwa na mtoto wao wa kiume.

Awali, Mahakama Kuu ilimuhukumu Mlelwa kifungo cha miaka 20 jela. Hata hivyo, alikata rufaa akipinga adhabu hiyo.

Mahakama ya Rufani, katika hukumu ya rufaa ya jinai ya mwaka 2023 iliyotolewa Juni 3, 2025, ilipunguza adhabu hiyo kwa kuzingatia muda wa miezi sita aliokuwa mahabusu akisubiri kesi kuanza.

Hukumu hiyo ilisomwa na jopo la majaji watatu ambao ni pamoja na Barke Sehel, Khamis Ramadhan Shaaban, na Dk Ubena Agatho na nakala ya hukumu imechapishwa kwenye tovuti ya Mahakama.

Ava ambaye ni shahidi wa pili, aliiambia Mahakama kuwa siku ya tukio walikuwa wanakula chakula cha jioni pamoja na mtoto wao.

Mlelwa alionyesha hasira baada ya kumshutumu mtoto wao kwa kuwa mkaidi. Ugomvi ulizuka, na baadaye alimshtukiza kwa kumshambulia kwa panga. Ava alinusurika baada ya majirani kuvunja mlango na kumsaidia kukimbilia nje.

Baadaye usiku, licha ya kumhakikishia balozi wa nyumba 10 kuwa hatafanya vurugu tena, Mlelwa alirudi nyumbani na kutekeleza shambulio hilo la kikatili.

Ava alipiga yowe kuomba msaada na majirani walimsaidia kumfikisha hospitali. Alipoteza fahamu kutokana na majeraha na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoka Amana kwa matibabu zaidi.

Shahidi wa kwanza ambaye ni  mtoto wao, Ezekiel Michael alithibitisha kuona baba yake akimkata mama yake kwa panga baada ya kuamshwa na kelele. Ezekiel ndiye aliyewafungulia mlango majirani waliokuja kutoa msaada.

Shahidi wa tatu, balozi wa nyumba 10 Mohamed Mbanga, alithibitisha simulizi ya Ava na kueleza jinsi alivyomsindikiza hospitali na kuripoti tukio hilo polisi.

Shahidi wa nne, Michael Aloyce ambaye ni kaka wa Ava, aliieleza Mahakama jinsi alivyompata Mlelwa mwaka mmoja baadaye akiwa Pugu Machinjioni na kusaidia kukamatwa kwake Agosti 31, 2019.

Shahidi wa tano, Sajenti Benard wa Kituo cha Polisi Buguruni, alithibitisha kupokea maelezo ya onyo kutoka kwa Mlelwa ambaye alikiri kutenda kosa hilo.

Naye shahidi wa sita, Dk Anjela Lameck wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, aliieleza Mahakama kuwa Ava alipokewa akiwa amepoteza fahamu kutokana na jeraha kubwa alilokuwa nalo kichwani.

Dk Lameck alisema CT Scan ilionyesha aliumia ubongo na kuvunjika fuvu. Alifanyiwa upasuaji wa dharura MOI kuondoa damu iliyoganda kwenye ubongo na kurekebisha fuvu lililokandamiza ubongo.

Katika utetezi wake, mrufani huyo aliiambia Mahakama kuwa alikuwa akifanya kazi katika Machinjio ya Mazizini, Gongo la Mboto na awali alikuwa akifanya kazi katika Machinjio ya Vingunguti, kati ya 2009 na 2018.

Aidha, alithibitisha kuishi na mkewe na mtoto wao katika eneo la Kiwalani na kuwa, anakumbua Agosti 31,2018 alimtuma mtoto huyo kununua dawa ya meno na samaki duka la jirani, lakini alirudi mikono mitupu kwa madai kuwa mama yake alimkataza kwenda.

Alidai kuwa alipomuuliza mkewe, alimdharau hivyo akakasirika na akaamua kumpiga.

“Baada ya hapo aliamua kwenda kuripoti kwa shahidi wa tatu ambaye alikuja naye nyumbani wakiwa wameongozana na mgambo. “Lengo lilikuwa kusuluhisha tofauti zetu, lakini mke wangu alikataa kulala na mimi kitanda kimoja,” alieleza mrufani.

Alieleza kuwa usiku wa manane, aliamka akawasha taa na kujiandaa kwa ajili ya kazi, alichuka panga lake, visu na kuweka kwenye mabuti na aliamini mkewe amelala hivyo akaacha fedha mezani za matumizi.

Alidai alipokuwa anatoka, mke wake alimshika kwa nyuma akimwambia fedha alizotoa hazitoshi kwa matumizi ya familia.

Alidai kuwa mke huyo alirudi ndani akajifungia huku akimtukana na kulalamika kuwa ameumizwa na panga alilokuwa nalo.

Alidai aliamua kwenda kazini ila hatua chache mbele aligundua kuwa hata yeye panga lilikuwa limemkata, hivyo alienda kupata huduma ya kwanza katika duka la dawa na kwenda kazini.

Alidai siku hiyo saa nne usiku, alipigiwa simu na shahidi wa nne akimtuhumu kuwa amemkata mkewe na panga, huku akidai mtu mwingine alimtahadharisha kuwa anawindwa auawe.

Alieleza kuwa vitisho hivyo vilimtia hofu ya kumtembelea mke wake Hospitali ya Muhimbili na alikamatwa tangu mwaka 2019, amekaa mahabusu kwa miezi sita.

“Mheshimiwa sikumtembelea mke wangu alipolazwa hospitalini kwa sababu ya vitisho vya shahidi wa nne na nilikuwa napigiwa simu na watu wasiojulikana mara kwa mara wakinionya kuhusu kulipiza kisasi kwa mke wangu,” alisimulia.

Alidai kovu la fuvu la kichwa la mkewe hakulisababisha yeye, na kama ingekuwa hivyo,  mkewe asingeweza kuishi hata kwa siku moja kutokana na ukali wa panga lake.

Baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili, ilihitimisha kuwa upande wa mashitaka umethibitisha kosa hilo bila kuacha shaka na kumuhukumu adhabu hiyo.

Katika rufaa hiyo, mrufani aliwasilisha sababu tisa za kupinga hukumu, ikiwamo madai ya kuwapo kwa utofauti kati ya shitaka na ushahidi uliotolewa mahakamani, kutotambuliwa eneo la tukio, kushindwa kwa upande wa mashitaka kuthibitisha kesi dhidi yake kwa kiwango kinachohitajika kisheria, pamoja na hukumu ya adhabu kali iliyotolewa kwa kuzingatia kanuni isiyo sahihi.

Katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, Michael alitetewa na mawakili wawili wakiongozwa na Jeremia Mtobesya, huku upande wa mjibu rufaa ukiwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Brenda Massawe.

Baada ya jopo la majaji kusoma kumbukumbu za rufaa na kusikiliza hoja kutoka kwa pande zote mbili, walieleza kuwa wamezingatia sababu zote zilizotolewa, ikiwamo iwapo kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila kuacha shaka na kama adhabu iliyotolewa ilikuwa ya kupita kiasi.

Jaji alieleza kuwa kwa kuwa rufaa hiyo ni ya kwanza, Mahakama hiyo ina wajibu wa kuchunguza upya, kutathmini na kuchambua ushahidi uliopo kwenye rekodi.

Baada ya kufanya hivyo, Mahakama ilijiridhisha kuwa upande wa mashitaka ulithibitisha kosa la kujaribu kuua bila kuacha shaka.

Hivyo, majaji walikataa rufaa hiyo kwa kuwa haikuwa na msingi wa kisheria, isipokuwa walipunguza adhabu kutoka kifungo cha miaka 20 jela hadi miaka 19 na miezi sita, wakikata miezi sita aliyokaa chini ya ulinzi akisubiri kesi kusikilizwa.

Related Posts