NIKWAMBIE MAMA: Kura iwe ya moto au baridi…

Enzi zile tulipokuwa shuleni tulikuwa tukichanganywa na malumbano ya hoja. Kwa ufundi mkubwa, waandaaji walitoa mada iliyokuwa na majibu sawa. Kilichokuwa kikisikilizwa si majibu, bali ni ufundi wa mwanafunzi kutetea hoja zake. Kwa mfano: “Maisha bora ni ya kijijini au mjini?” Aliyejibu ni ya mjini alikuwa sawa kwa utetezi kuwa mjini kuna miundombinu ya kisasa iliyoweza kumrahisishia mtu elimu, matibabu na huduma bora za kijamii. Lakini pia aliyesema maisha ya kijijini ni bora naye alikuwa sahihi kwa kuzingatia uhalisia. Chakula cha asili na utamaduni ni nguzo muhimu kwenye maisha ya mwanadamu, hivyo kuepuka mabaya yanayozalishwa na shughuli za binadamu.

Suala la iwapo Tanzania inahitaji uchaguzi huru na wa haki si swali katika jamii yetu. Watanzania wanataka amani kwenye maisha yao, wanataka kutumia haki yao kujipatia viongozi walio matarajio yao. Pande zote zinazopingana katika uchaguzi huu zitakwambia kuwa uchaguzi huru na wa haki ndio msingi wa demokrasia na maendeleo, na hauna budi kufuatwa na kutimizwa kwa gharama yoyote ile.

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba 2025 unachukuliwa kuwa tukio muhimu katika historia ya kisiasa ya taifa. Katika kipindi hiki, Watanzania wanatarajiwa kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaowaongoza katika miaka ijayo. Hata hivyo, mafanikio ya uchaguzi huu yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa amani, utulivu, na ushiriki wa wadau wote katika kuhakikisha mchakato huru na wa haki.

Uchaguzi huu ni fursa ya Watanzania kuimarisha misingi ya utaifa wao na kudhihirisha uwezo wa taifa kushughulikia tofauti za kisiasa kwa njia ya amani. Ili kufanikisha hili, ni muhimu kwa wadau wote kushirikiana kwa dhati katika kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unakuwa huru, wa haki, na wa amani. Kwa kufanya hivyo, Tanzania itaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

Katika hali ya kawaida kabisa, binadamu hujifunza kutokana na makosa yake pamoja na ya wengine. Lakini wakati huohuo, binadamu huyuhuyu huingiwa na wasiwasi kuwa makosa mengine hutengenezwa ili kumtia ugumu. Makosa haya yanapoonekana kujirudia humwaminisha kuwa mfumo wa kidemokrasia umeondolewa bila taarifa, hivyo hana nafasi ya kutumia haki yake kwenye yale anayoyataka. Hapa vurugu zinaweza kuzuka wakati wowote.

Mgogoro ulio tishio zaidi kwenye uchaguzi ujao ni baina ya kambi zinazopingana. Kila kambi inadai kufuata utawala wa haki na sheria huku upande mmoja ukilalamika kugandamizwa. Mwezi Aprili mwaka huu, vyama vya siasa vilitakiwa kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi. Hatua hii ililenga kuhakikisha kampeni zinazoendeshwa ni za amani, zenye kuheshimu haki za binadamu, na kuzuia lugha za chuki au uchochezi.

Pamoja na juhudi hizi, kuna changamoto kadhaa zilizoelekea kuhatarisha amani ya uchaguzi. Mojawapo ni hatua ya kuenguliwa kwa chama kikuu cha upinzani, kushiriki katika uchaguzi baada ya kiongozi wake kushtakiwa kwa kosa la uhaini kufuatia wito wake wa mageuzi ya uchaguzi. Tukio hili limeibua wasiwasi kuhusu usawa wa kisiasa na haki ya vyama vyote kushiriki katika mchakato wa uchaguzi.

Kwa maoni yangu, wasiwasi ni akili kwa kila mmoja. Wasiwasi ni sawa na uvimbe katika mwili, hivyo ni lazima uondolewe ili usiendelee kuleta madhara au kumtisha mwenye mwili wake. Hivyo tatizo lolote linalotajwa kwenye Uchaguzi Mkuu ni lazima litatuliwe bila kujali linatatiza kwenye kambi ipi. Kila mmoja anapaswa kuridhika na mchakato kwani wananchi ni wengi kuliko wanachama wa vyama vyote na wapiga kura kwa ujumla wao.

Vilevile, matokeo ya uchaguzi huu yanaakisi kila kona ya ulimwengu. Kitendo cha baadhi ya wachambuzi kuelezea hofu kuhusu mazingira ya kisiasa ya Tanzania ni lazima kitazamwe. Vinginevyo kinaweza kubomoa imani ya watu katika mchakato wa kidemokrasia na kusababisha mvutano wa kisiasa. Ile sura ya “Watanzania wote ni ndugu” inaweza kupoteza nuru yake.

Lazima tuunge mkono kampeni za kuhamasisha amani na mshikamano miongoni mwa wananchi. Hizi ni miongoni mwa jitihada zinazohamasisha uwepo wa amani katika kipindi hiki kigumu na muhimu. Pia ni namna bora zaidi ya kuisaidia Serikali kwa sababu kupitia jitihada hizi, Serikali itajifunza kile ambacho watu wake wanataka.

Si ajabu maswali ya majibu yao yote yatapatikana humo badala ya majibu waliyojiandikia kwenye makaratasi. Uchaguzi huja na kupita ukiwakuta na kuwaacha Watanzania ikiendelea na maisha yao. Na tukumbuke kila jambo linalofanyika katika muda mfupi lina athari ya muda mrefu na kwenye wakati wote unaofuatia jambo hilo. Ni tahadhari kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo.

Ni wajibu wa Serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini, na wananchi kwa ujumla kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani. Amani ni tunu isiyoweza kutengenezwa kwa siku moja, lakini huweza kutoweka ndani ya nukta moja na isirudi asilani. Tujifunze kutokana na makosa yetu ya chaguzi zilizopita, lakini pia tujifunze kwa wenzetu wanaokesha kuomba amani iliyotoweka baada ya makosa ya uchaguzi.

Related Posts