Unguja. Katika kupunguza na kuondosha changamoto za migogoro ya ardhi, Serikali kupitia kamisheni ya ardhi imeshapima na kutoa hati za matumizi ya ardhi maeneo 6,416 kwa kipindi cha miaka mitano.
Kati ya maeneo hayo, Unguja ni maeneo 3,914 na Pemba ni 2,502 ambayo yamepimwa tangu mwaka 2021 hadi mwaka huu kwa ajili ya matumizi ya makazi, wawekezaji, taasisi za Serikali na binafsi ikiwa ni zaidi ya mafanikio ya asilimia 80.
Hayo yamebainishwa leo Juni 4, 2025 na Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Salha Mohamed Mwinjuma wakati akijibu maswali ya wawakilishi barazani.
Amesema kiwango hicho ni kikubwa ikilinganishwa na ardhi iliyopimwa na kutolewa hati mwaka 2015 hadi 2020 ambapo walipima maeneo 1,709.
Katika swali la msingi, mwakilishi wa Wawi, Bakar Hamad Bakar alitaka kujua ni kwa kiasi gani Serikali imefanikiwa katika upimaji na umilikishaji wa ardhi kwani sio tu ardhi iliyopimwa inaondoa changamoto za migogoro, lakini pia inasaidia kwa kiasi kikubwa kuipandisha hadhi.
“Serikali imefanikiwa kufanya utambuzi wa maeneo mbalimbali ambapo jumla ya maeneo 3,611 yamesajiliwa, kati ya hayo 2,496 kwa Unguja na mengine 1,115 Pemba na kuwapatia wananchi hati, hali hiyo imesababisha kuipandisha hadhi ardhi yetu, kuwa na umiliki kisheria na kuweka ardhi kama dhamana ya mikopo,” amesema.
Naibu Waziri huyo amesema Serikali inaendelea na juhudi kuhakikisha inapanga maeneo yote ya Zanzibar ili kuweka mipango mizuri ya matumizi ya ardhi inayofuata mpango mkuu wa matumizi ya ardhi nchini.
Miongoni mwa hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuiwezesha kamisheni ya ardhi kuajiri wataalamu 44 kwa njia ya mkataba pamoja na kuimarisha upatikanaji wa vitendea kazi.