Tuweni makini na maduka ya wauza roho

Kwa wanaofuatilia masuala ya dini, watakubaliana nasi kuwa imezuka biashara chafu ambayo ni karibu ya wizi na ujambazi japo tofauti ni kwamba imehalalishwa na serikali zetu.

Hii si nyingine, bali uanzishwaji wa madhehebu ya dini na makanisa yenye lengo la kutengeneza fedha na si vinginevyo.

Siku hizi biashara ya dini inalipa karibu sawa na ya dawa za kulevya. Anayeshuku hili aangalie utitiri wa madhehebu na makanisa na utajiri wa viongozi wake tena wa ghafla bin vuu, bila maelezo yanayoingia akilini.

Mwenyekiti Mao Zedong aliwahi kusema kuwa bila utafiti, hakuna haja ya kutoa madai. Pia, sheria inasema atoaye madai, atoe ushahidi.  Hivyo, katika andiko langu ninatoa ushahidi kama ifuatavyo;

Mosi, kama tulivyosema hapo juu, ukitaka kujua ukweli wa dhehebu la dini au kanisa, waangalia wale wanaojiita viongozi wake.

Angalia aina ya maisha wanayoishi na mahubiri wanayohubiri. Wengi wa wahubiri na viogozi wa kujipachika vyeo kama vile mchungaji, askofu, mtume, nabii na vingine, hawafanyi kazi zozote za kuwapatia kipato.

Ni matapeli wanaowaibia na kuwanyonya waumini wao wavivu wa kung’amua vitu rahisi ima tokana na ujinga au kukata tamaa.

Je huu utajiri wanaupata wapi kama siyo kuwaibia wafuasi wao ima waliokata tamaa au wajinga tu?

Wapo wanaojihusisha na biashara nyingine hata bila kulipia kodi na hivyo kuiibia serikali na kujiingizia fedha nyingi kinyume cha sheria. Kwa nini mamlaka hazijiulizi swali hili rahisi, kinachofanyika hakina tofauti na ujambazi wa kawaida ambao jambazi hulala maskini na kuamka tajiri bila kutoa maelezo? Kwanini mamlaka hazitaki kuuliza au kuna namna

Pili, kujua mbivu na mbichi, angalia mhusika amepata uongozi au ukuu wa dhehebu husika namna gani. kama amejipachika kama wengi tunaowaona hata wakijiingiza kwenye siasa, anachofanya mhusika ni biashara ya kusaka tonge na fedha kwa mgongo wa neno la Mungu ambalo siku hizi limegeuka biashara kubwa duniani ambapo matapeli na waroho wengi wa utajiri hujipatia utajiri na ujiko.

Tatu, angalia namna kanisa au dhehebu husika linavyopitisha madaraka inapotokea kiongozi kafa.

Utaratibu tuliozea kwa dini za kweli ni kwamba akifa kiongozi wake, hufanyika uchaguzi na kumpata mtu anayefaa ambaye mara nyingi huwa ameandaliwa hata kabla ya kiongozi kufa japo si kwa din izote.

Mfano, makanisa maarufu kama vile la Kiroma, Kianglikana, Kilutheri na mengine yanayoheshimika, huwa na utaratibu wa kuteua au kufanya uchaguzi wa mrithi wa kiongozi anapostaafu au kufariki dunia.

Hata Uislam una utaratibu huu. Mfano, anapokuwa shehe mkuu, hufanyika uchaguzi wa shehe mkuu mwingine ambaye mara nyingi hana uhusiano wa damu na anayemrithi.

Hata Papa anapokufa au askofu wa baadhi ya madhehebu yanayoheshimika, hali ni hii. Hakuna kurithishana madaraka kama tulivyoshuhudia hivi karibuni hapa nchini, alifariki dunia mmojawapo wa waliojipachika madaraka ambaye kanisa lake, kwa vile lilikuwa duka lake lililopachikwa jina la kanisa, alirthishwa binti yake.

Je kweli Kanisa la Mungu laweza kurithishwa au kutafutiwa mtumishi? Je makanisa haya yanayorithishwa kwa kufuata damu ni makanisa au maduka tu? Utarithije kanisa au msikiti wa Mungu?

Mfano mwingine wa hivi karibuni ni pale alipokufa kiongozi mwingine wa kanisa kule Nigeria. Baada ya kifo cha ghafla cha kiongozi huyo, ulizuka mgogoro katika urithi wa kanisa, mkewe alirithi kanisa la mme wake.

Wakati wenzake wakimpa urithi mke huyo, walitoa sababu hafifu na mbovu kuwa mmewe alizaliwa mtume na mkewe aligeuka mtume kupitia ndoa hasa ikizingatiwa kuwa mume na mke ni mwili mmoja!

Je kwa huyu wa kwetu dhana hii chafu inasimama au tutaambiwa kuwa kwa vile binti yake ni damu ya mama basi nao ni kitu kimoja?

Nne, kujua kuwa dhehebu au kanisa husika ni duka la kuchuuza neno na roho, angalia namna wakubwa wake wanavyosaka umaarufu na matumizi makubwa ya vyombo vya habari au kujiingiza kwenye siasa.

Nchini Uganda, marehemu Padri Simon Lokodo alifukuzwa upadri na Papa mstaafu Bendict XVI baada ya kujiunga kwenye mbio za kugombea jimbo la Dodoth ambalo alifanikiwa kushinda na kuliongoza hadi mauti yanamfika Januari 29, 2022.

Tano, kujua kama dhehebu au kanisa husika ni la kitapeli au duka la kiroho ni kuangalia aina ya mahubiri ya viongozi au wenye duka husika wanavyohubiri.

Wengi wa matapeli hawa wakiroho uhubiri mambo makuu matatu, yaani utabiri, utajiri na kufanya miujiza ya urongo.

Rejea mfano, yupo aliyeahidi kumfufua marehemu Amina Chifupa. Mbali na huyo, aliicha dunia hoi alipotabiri kuwa Hilary Clinton angeshinda urais wa Marekani akaishia kubwagwa na Donald Trump jambo ambalo lilifichua utapeli na ubabaishaji wa tapeli huyu.

Leo sitaandika mengi zaidi ya kuwasihi wale wanaoibiwa kila uchao kutokana na imani zao, wawe makini.

Wachunguze mambo matano niliyodurusu hapo juu kujua kama wanachojiunga nacho ni duka la kiroho au dini.

Wengi wanaibiwa na kuaminishwa kuwa kuna siku watabarikiwa na kuwa matajiri wakati hao wanaowaibia wanazidi kuwasikinisha, kuwadanganya na kuwapotezea muda.

Nadhani huu ni wakati wa serikali kuchunguza utajiri na taasisi za viongozi wa kujipachika madaraka umefika.

Vinginevyo, serikali haiwasaidii wananchi wake. Pia, ifahamike, imani katika miujiza ni chanzo cha uvivu na uuaji wa maarifa.

Hivyo, licha ya kuathiri hali na uchumi wa waathirika, inaathiri uchumi wa taifa ukiachia mbali kuvunja sheria kwa kuhubiri uongo.

Related Posts