Ukiacha vikumbo vya ubunge katika mikoa mingine, Dar es Salaam inabeba vita ya pekee katika mbio za kuisaka nafasi hiyo, huku wanasiasa, wafanyabiashara na wanahabari wakiwa ndani ya kinyang’anyiro hicho.
Jiji hilo linaloundwa na majimbo 12 ya uchaguzi, imekuwa kiu ya watu wengi kuusaka ubunge kupitia majimbo hayo hasa Kawe, Kinondoni, Chamazi na Kigamboni.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mwaka 2022 Dar es Salaam ilikuwa na wakazi milioni 5.4 na ni mkoa unaokua kwa kasi zaidi nchini kwa asilimia 5.6 kwa mwaka. Jiji hilo linakadiriwa kuwa na zaidi ya asilimia 12 ya wapiga kura wote nchini.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Dar es Salaam ilikuwa na wapiga kura zaidi ya 2.2 milioni, sawa na takribani asilimia 13 ya wapiga kura wote kitaifa kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) mwaka 2020.
Hii inaifanya Dar es Salaam, kuwa ngome muhimu kwa vyama vyote vikuu nchini ikiwemo CCM, Chadema na ACT-Wazalendo, hasa ikizingatiwa takriban kila jimbo lina watu wenye mwamko wa kisiasa na idadi kubwa ya wapiga kura vijana.
Hayo yanatokea katika kipindi ambacho tayari, vyama vya siasa vimefungua pazia la makada wao kutangaza nia na vingine kuchukua fomu za ubunge, urais na udiwani, kuelekea uchaguzi wa baadaye mwaka huu.
Kivumbi zaidi kinatarajiwa kushuhudiwa katika Chama cha Mapinduzi (CCM), kinachotajwa kuwa na wagombea wengi zaidi.
Wakati hayo yakiendelea, wananchi wa majimbo mbalimbali katika Jiji hilo, wanasema kiu yao ni kuwapata viongozi watakaokuwa na dhamira ya dhati ya kuwawakilisha na sio kujaza matumbo yao.
Ukiacha majimbo mengine ambayo angalau yanatabirika, katika Jimbo la Kawe hali ni tofauti. Ndilo eneo linalotajwa kuwa na mizania sawa kwa kila mshindani, kwa kuwa hadi sasa limekosa mwenyewe.
Katika uchaguzi wa 2020, Jimbo la Kawe lilikuwa na wapiga kura waliojiandikisha 125,000. Mbunge wa sasa, Askofu Josephat Gwajima, alishinda kwa kura 61,791 akimpiku Halima Mdee wa Chadema, aliyepata kura 34,533. Asilimia 12 ya wapiga kura hawakujitokeza.
Kwa kuwa Askofu Gwajima hakushinda kwa zaidi ya asilimia 55, hii inaonesha kuwa, Kawe ni moja ya majimbo yenye ushindani mkali zaidi jijini. Hii ndiyo sababu wanasiasa na wafanyabiashara wenye ushawishi mkubwa wamevutiwa na jimbo hilo kwa uchaguzi ujao.
Askofu Gwajima anatajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa wanaojipanga kutwaa ubunge huo, ikiwa ni kipindi cha pili baada ya kuongoza kwa miaka mitano.
Lakini, mbio za Askofu Gwajima katika kinyang’anyiro hicho zinatajwa kuishia sakafuni kwa kile kinachoelezwa kuwa, nguvu ya ushawishi aliyonayo imezidiwa maili zaidi na mshindani wake katika kura za maoni mwaka 2020, Furaha Dominick.
Katika kura za maoni ndani ya CCM, mwaka 2020, Dominick aliongoza kwa kupata kura 101, huku Askofu Gwajima akishika nafasi ya tatu kwa kura 79, lakini ilivipendeza vikao vya juu vya chama hicho kumteuwa agombee nafasi hiyo.
Hata hivyo, kwa sasa, Askofu Gwajima ana nafasi finyu ya kupenya kwenye vikao hivyo, baada ya kauli zake za karibuni za kukemea vitendo vya utekaji, kuonekana kuwa harakati za upinzani ndani ya chama hicho.
Hilo linathibitishwa na kilichoelezwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika Mei 30, mwaka huu, alipotaka wagombea watakaoteuliwa kutoka CCM, wawe sahihi na wasifanye kile alichokiita kugwajimanize chama hicho.
“Tukipitisha wanaotafuta tu na mie niwemo ndio tunapata wale wanaokwenda huko, chama kinakuwa Gwajimanized, kwa hiyo kwa vyovyote vile tusigwajimanize chama chetu magwajima tuyaache nje, hamna kuoneana aibu wala haya,” alisema.
Kwa inavyoonekana bado Askofu Gwajima anautaka ubunge katika jimbo hilo, hivyo anaweza kuwa miongoni mwa wagombea, ingawa haijajulikana iwapo atatumia jukwaa la CCM au kwingineko.
Hilo linathibitishwa na kauli ya Dominick katika mahojiano yake na moja ya chombo cha habari nchini, akisema “(Askofu Gwajima) akatae kama hajaniomba nimuachie miaka mitano mingine.
“Ameniomba tukiwa Dodoma Mkutano Mkuu Maalum, akatae kama hakuniomba nimuachie uchaguzi,” alisema Dominick huku akisisitiza alimwambia kuwa hatamwachia.
Ukiacha wanasiasa hao wanaotajwa zaidi jimboni humo, Mbunge wa zamani wa eneo hilo kwa tiketi ya Chadema, Halima Mdee, hayuko mbali, anaonyesha kiu ya kuutaka ubunge kupitia jimbo hilo, ingawa naye haijajulikana iwapo atatumia chama gani.
Kiu ya Mdee, inapata mashiko zaidi pale aliposema katika moja ya mahojiano yake kuwa, yeye si muumini wa kususia uchaguzi, msimamo ambao ndio unaotekelezwa na chama chake cha Chadema, kwamba kitazuia uchaguzi iwapo mabadiliko hayatafanyika.
Mkazi wa Kawe, Dennis Mgacha anasema kiu yake ni kupatikana kiongozi atakayekuwa na nia ya dhati ya kuwawakilisha, badala ya wale wanaotaka ubunge kutimiza malengo yao binafsi.
“Wanavyoshindana inatia mashaka kwamba kuna maslahi wanapambania, sisi tunataka mtu atakayetanguliza maslahi yetu. Binafsi nimeshafuatwa na kusikia wengi wanataka ubunge Kwe, tunasubiri kuona nani atafaa,” amesema Dennis Mgacha.
Mchuano unaokaribiana na ule wa Kawe, unashuhudiwa katika Jimbo la Kigamboni ambalo hadi sasa halina mwenyewe, hasa baada ya Mbunge wake kwa tiketi ya CCM, Dk Faustine Ndugulile kufariki dunia.
Kwa mujibu wa INEC mwaka 2020, Kigamboni ilikuwa na wapiga kura 92,308. Hayati Dk Ndugulile aliyefariki dunia mwaka huu alishinda kwa kura 49,194 sawa na asilimia 53.3 ya kura zote halali.
Kifo chake kimeacha pengo lililovutia majina mapya kama Rais wa Klabu ya Soka ya Yanga, Hersi Said na Mwanahabari Nguli, Habib Mchange.
Katika utafiti mdogo uliofanywa na Taasisi ya Twaweza mwaka 2023, asilimia 47 ya wakazi wa Kigamboni walionyesha kuwa wako tayari kupigia kura mtu wanayemfahamu binafsi au kwa kazi zake za kijamii, tofauti na miaka ya nyuma ambapo chama kilikuwa ni kipimo kikuu.
Pia, Kigamboni ni moja ya maeneo yanayokua kwa kasi kwa miundombinu na uhamiaji mpya umesababisha idadi ya wapiga kura kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 20 tangu uchaguzi wa 2020, kwa mujibu wa NBS mwaka 2023.
Hii ina maana kuwa kuna wapiga kura wapya zaidi ya 18,000 wanaotarajiwa kujiandikisha kwa uchaguzi ujao.
Katika Jimbo hilo, watu mashuhuri kutoka sekta mbalimbali wanatajwa kulinyapia akiwemo Hersi, ingawa pia amewahi kuhusishwa na jimbo la Kongwa, aliko Spika wa Bunge wa zamani, Job Ndugai.
Nguvu ya Hersi katika jimbo hilo, inanasibishwa na ukaribu wake na vigogo lukuki wa CCM, hivyo anatajwa kuwa na njia nyeupe zaidi.
Ukiacha Hersi, mtu mwingine maarufu anayehusishwa na mbio za ubunge katika jimbo hilo ni mwanahabari mkongwe, Habib Mchange.
Mchange naye anakaribiana mizania ya ushindani kwa muktadha wa ukaribu na vigogo wa CCM, kama ilivyo kwa Hersi. Wote hao wanatajwa kuwania kwa tiketi ya CCM.
Mbali na wawili hao, ubunge wa Kigamboni upo katika rada za wafanyabiashara pia, ambao ni Ali Aboubakar maarufu kwa jina la Boka na Dotto Rwekiza maarufu Togabe Super Sembe.
Mkazi wa Kigamboni, Hellen Malenda anaona pilika zinazoendelea kutoka kwa watu hao ni ishara kwamba kila mmoja anajiona na nafasi ya kushinda.
“Mwisho wa siku sisi ndio tutakaoamua nani awe mshindi, tutakachoangalia ni mtu mwenye sifa zinazotupendeza ndiyo tumpe nafasi,” anaeleza Hellen.
Jimbo la Chamazi ni miongoni mwa majimbo mapya yaliyoanzishwa kufuatia mabadiliko ya mipaka ya uchaguzi yaliyofanywa na INEC.
Takriban kata saba kutoka Jimbo la Mbagala zimeunganishwa kuunda Chamazi, zikiwa na wakazi zaidi ya 180,000.
Kata kama Buza, Chamazi na Azimio zina wastani wa watu 25,000 kila moja na zaidi ya asilimia 60 ya wakazi hao ni vijana wa umri wa kati ya miaka 18 hadi 35, kundi linaloonekana kuwa na ushawishi mkubwa kisiasa kwa mujibu wa NBS mwaka 2023.
Chaurembo aliyekuwa Mbunge wa Mbagala alishinda ubunge kwa kura 68,343 mwaka 2020, huku akitajwa na wengi kuwa na mafanikio katika ufuatiliaji wa miradi ya maji na barabara.
Vikumbo ubunge majimbo ya Dar es Salaam
Hata hivyo, Mtinika anaungwa mkono na mtandao mkubwa wa madiwani, hasa kutoka Kata ya Azimio na Chamazi yenyewe, alikopata ushindi wa zaidi ya asilimia 70 katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2019.
Turufu aliyonayo Chaurembo ni nguvu ya ubunge, uzoefu kwa kuwa ameshahudumu katika nafasi hiyo na angalau utendaji wake unajulikana na wananchi.
Kwa upande wa Mtinika nguvu yake inatokana na utumishi wake akiwa Meya wa Temeke, pia yuko karibu na wajumbe, hivyo wote wana nguvu zinazowiana.
Kihistoria, Kinondoni ni jimbo lisilotabirika, kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya wabunge karibu kila baada ya miaka mitano.
Katika uchaguzi wa 2020, Abbas Tarimba alishinda kwa kura 47,788, sawa na asilimia 52.4 ya kura zote. Wapinzani wake walikuwa na wastani wa asilimia 44 kwa pamoja, hali inayoonesha kuwa jimbo lina ushindani mkubwa.
Katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019, chama alichonacho Tarimba, kilipata madiwani 11 kati ya 15 wa kata zinazounda jimbo hilo, lakini baadaye baadhi yao walihamia vyama pinzani.
Katika Jimbo la Kinondoni linaloshikiliwa sasa na Tarimba, linatajwa kuwa kwenye rada za wanasiasa wengi, akiwemo Idd Azzan aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka mitano.
Nguvu ya Azzan inatokana na ukaribu wake na viongozi wa CCM, lakini naye ni sehemu ya sekretarieti inayounda uongozi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam.
Pamoja na Azzan, Tarimba naye anatajwa kuonyesha nia ya kutetea nafasi yake, huku katikati yao anaibuka Diwani wa Hananasif, Wilfred Nyamwija.
Nyamwija naye ni mwanasiasa anayetajwa kuwa karibu na wadhifa huo na turufu aliyonayo ni umaarufu na ushawishi kutoka kwa wananchi wa jimbo hilo.