Moshi. Vilio na simanzi vimetawala katika mazishi ya wanandoa Geofrey Motta (60) na Blandina Ngowi (53) waliouawa kikatili nyumbani kwao Msufuni, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro usiku wa Mei 29, 2025.
Geofrey alikatwa shingo na Blandina alinyongwa, kisha miili yao kutelekezwa ndani ya nyumba waliyoishi kwa kupanga.
Mazishi yao yamefanyika Juni 4, 2025, katika makaburi ya familia eneo la Kariwa Chini, Kata ya Rau, baada ya ibada iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Msaranga Mandaka, na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji.

Majeneza yenye miili ya wanandoa Geofrey Mota (60) na Blandina Ngowi (53) yakiwa katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Msaranga Mandaka, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Akihubiri kwenye ibada hiyo, Mchungaji Israel Moshi amesisitiza kuachana na chuki na visasi, vitendo alivyosema huzaa laana na madhara kwa jamii.
“Jamii yetu imejaa visasi, tumegeuka kushindana na ubaya. Huu ni msiba wa majonzi makubwa. Mungu hadhihakiwi,” amesema Mchungaji Moshi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Msufuni, Elieth Mshana, ameeleza kuwa tukio hilo ni la kutisha na halijawahi kutokea katika historia ya mtaa huo.

Jeneza lenye mwili wa Blandina Ngowi (53) likiingizwa kaburini
Mwakilishi wa Kwaya ya Tumaini Kipimo, ambako marehemu Blandina alikuwa mwimbaji, amesema wamepoteza mtu muhimu mwenye moyo wa kujituma na kwamba kifo chake kimewaacha katika majonzi makubwa.
Diwani wa Kata ya Bomambuzi, Juma Raibu, ameahidi zawadi kwa yeyote atakayesaidia kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa, akisisitiza ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi.
“Tumeona vifo vingi, lakini mume na mke kuuawa kwa wakati mmoja kwa ukatili huu ni jambo la kusikitisha sana. Tunatoa donge nono kwa atakayesaidia kumfikisha mhusika kwenye vyombo vya sheria,” alisema Raibu.

Baadhi ya watoto wa marehemu, Geofrey Motta (60) na Blandina Ngowi(53) wakiaga miili ya wazazi wao katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Usharika wa Msaranga Mandaka, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi huku jamii ikihimizwa kushirikiana ili kuhakikisha haki inapatikana.