Wadau wapinga mamlaka, kufungiwa mtandao wa X

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikithibitisha kuzuia mitandao inayoenda kinyume na maadili ya nchi, wadau wa mawasiliano wamekosoa uamuzi huo, wakipendekeza mamlaka ijikite kudhibiti maudhui yasiyofaa na sio kuuzima mtandao husika.

Kwa mujibu wa wadau hao, kuzima mtandao kunavunja haki ya kikatiba ya wananchi kupata na kutoa taarifa, jambo linalowanyima uhuru wa kufanya uamuzi sahihi.

Maoni hayo ya wadau yanakuja siku moja baada ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa kuweka wazi kuwa iwapo mwananchi anashindwa kupata mtandao fulani ajue kuwa Serikali imefanya namna kumlinda Mtanzania.

“Kama umeona kuna baadhi ya mtandao sio lazima uwe X  wowote hata YouTube kuna kitu unatafuta hukipati ujue ni kazi inayofanywa na Serikali kuhakikisha inamlinda mlaji na kuhakikisha watu wote wanaoendesha huduma kwenye anga la Taifa letu wanafuata sheria,” amesema.

Silaa katika mahojiano yake na Kituo cha Luninga cha Wasafi, amesema Kifungu cha 16 cha Kanuni ya Maudhui ya Mtandao ya mwaka 2000, kinaeleza aina ya maudhui yanayopaswa kuchapishwa katika mtandao husika.

Amesema kanuni hizo zinalenga kumlinda mtumiaji Mtanzania na ikifanywa kinyume Serikali inafanya namna kuhakikisha mtumiaji analindwa.

“Baada ya X kununuliwa na baadaye Mei 2024 mtandao huo ulibadili sera yao ya faragha inayokwenda kinyume na kanuni hiyo ya Tanzania.

“Ukienda X unaweza kukuta picha za ngono, mambo ambayo yanakwenda kinyume na sheria, tamaduni, mila na desturi zetu,” amesema.

Kutokana na kauli hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Afrika inayoendelea majukwaa ya mitandao ya Jamii Forum, Maxcence Mello amesema kufungia mtandao wa kijamii ni uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na wasimamizi wa mitandao husika.

Amesema kufanya hivyo, kunavunja haki ya kikatiba ya watu kutoa maoni akifafanua, “wanafanya kwa kutumia visingizio vya kisiasa na hata visivyo vya kisiasa, visivyo na mashiko, eti kuna watu wanaitumia mitandao vibaya.”

Kwa mujibu wa Mello, kama kuna wanaoitumia mitandao vibaya kuna taratibu za kufuatwa kuhakikisha maudhui wanayoweka yanaondolewa.

“Kuna madai kuwa mitandao hii inaonyesha picha za ngono, kwa ukweli mitandao haifanyi kazi kwa mtindo huo, mitandao yote inayoonyesha picha za ngono, ina utaratibu wa kufuata kabla mtu hajaziona,” amesema.

Ili ufikie kuangalia maudhui ya utupu, amesema mtandao husika unamtaka muangaliaji athibitishe kuwa na umri zaidi ya miaka 18.

Mello amesema visingizio vinavyotumika vinawanyima watu haki ya kupata taarifa kwa kuwa sio kila mtu anatumia mitandao kuangalia maudhui yasiyostahili.

“Kitendo cha kuzuia upatikanaji wa mitandao ya kijamii ni uvunjwaji wa haki za binadamu na sio jambo la kuchekea, nashauri wadau wa sekta ya habari wapigie kelele,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema sio mtandao wa X pekee ndio wenye maudhui ya ngono, yanapatikana Instagram na kwingineko, akihoji ina maana mamlaka itakwenda kuifungia yote.

“Kuchagua baadhi ya mitandao ya kuifungia ni kutukosea, kutumia madaraka vibaya na nguvu walizonazo kama vyombo vya dola au mitandao husika. Nadhani ni vizuri kabla ya kufanya haya washirikishe wadau wapate maoni ili wananchi wenyewe waseme,” amesema.

Amesema kufungia mitandao hakupunguzi tatizo kwa namna yoyote zaidi ya kuongeza chuki ya wananchi dhidi ya mamlaka, ni vema nchi ikatoka kwenye mwenendo huo.

Mello amewataka wananchi kuwakataa viongozi au mamlaka yoyote inayosema itafungia mtandao, kuhakikisha siasa zinaacha kutumika kuinyima jamii haki ya taarifa.

Kwa upande wa mamlaka, ameitaka kutoa elimu kwa jamii kama kuna mwenendo usiofaa wa matumizi ya kijamii kwa kushirikiana na wadau, badala ya kuwaadhibu wananchi wote.

Kwa kampuni zinazotoa huduma hizo za mitandao, amesema zinapaswa kuweka wazi iwapo zimepewa amri kutoka popote kwamba zizuie mtandao.

“Itasaidia wananchi kutambua kasoro inaanzia wapi, kuliko kuhangaika kujifunza kutafuta kasoro zinatoka wapi,” amesema.

Amevitaka vyombo vya habari vihakikishe vinashirikiana na wadau kupigania haki ya wananchi kupata taarifa hasa ukizingatia mitandao ndizo nyenzo wanazozitumia kupata taarifa.

Kwa asasi za kiraia, amesema ulimwengu wa kidijitali umetengeneza fursa kwa wabaya wasiopenda watu kupata taarifa kuzuia wananchi wasiipate haki hiyo, ni wakati wote washirikiane kupaza sauti.

Hoja zinazoshabihiana na hizo, zimetolewa pia na Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya aliyesema kufungia mtandao wa kijamii, kunasababisha kukosekana kwa moja ya njia ya kupata na kutoa habari.

“Kuna habari watu watazikosa na kuna habari watu watashindwa kuzitoa. Kwa sababu binadamu wanaamua kutokana na taarifa wanazosikia na kuziona, ukiwafungia wakashindwa kuona, watashindwa kufanya uamuzi sahihi,” amesema.

Sio wananchi pekee, amesema mtandao kama X wakati mwingine huisaidia hata Serikali kupata taarifa kuhusu jamii inayoiongoza, ukiufunga fursa hiyo itakosekana.

Kwa mtazamo wa Simbaya, ingawa watu wanapaswa kuitumia mitandao kwa adabu, wachache wanaokwenda kinyume wasisababishe athari kwa jamii yote.

“Serikali ilipaswa kuwa na njia ya kuwabaini wanaotenda makosa katika mtandao husika na waadhibiwe wenyewe kwa makosa yao, badala ya kuwaadhibu wananchi kwa ujumla wao,” amesema.

Kwa mujibu wa Simbaya, suala la mawasiliano ni haki ya kikatiba na inapaswa kuheshimiwa, hivyo kama kuna wachache wanaoenenda sivyo waadhibiwe na sio kuwaathiri wengine wote.

Related Posts