Wanaume wasiotaka kuzeeka dawa ya bure hii hapa

Wanaume ambao wameoa huwa hawazeeki haraka ikilinganishwa na wale ambao ni makapera, utafiti umebaini.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la International Social Work,  uliangazia umuhimu wa ndoa kwa wanaume na wanawake na mchango wake katika safari yao ya kuzeeka.

Hata hivyo, kwa wanawake haikubainika iwapo maisha ya ndoa yanapunguzia uzee.

Kwenye utafiti huo uliochukua miaka 20, wanaume ambao wana umri wa kati ya miaka 45-85 walishirikishwa na maisha yao kuangaziwa.

Mwonekano wao, afya ya kiakili, uhusiano wao na jamii na umri ni kati ya vigezo ambavyo viliangaziwa.

Kwa ujumla utafiti huo ulionyesha kuwa wanaume ambao walikuwa kwenye ndoa, walikuwa na siha njema, hawakuonekana kutatizika kiakili  licha ya kuwa umri wao ulikuwa umesonga, wengi bado walionekana kuwa vijana.

Wale ambao walikuwa na utulivu kwenye ndoa zao, walionekana wachanga ikilinganishwa na umri wao kutokana na kujitunza vizuri na mahitaji yao kukidhiwa na wake wao.

Ilibainika ndoa tulivu huimarisha afya ya kiakili ya wanaume huku wale ambao ni makapera wakiandamwa na matatizo mbalimbali ya kiakili.

Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 79 ya makapera wapo katika hatari ya kuandamwa na msongo wa mawazo ikilinganishwa na wale ambao wameoa.

Hata hivyo, talaka, mume na mke kutengana, kifo cha mke au mume, huwa na mchango hasi kwenye afya ya mume au mke na husababisha wao kutinga uzeeni haraka kuliko umri wao.

Kwa wanawake, uthabiti wa ndoa si hoja sana kwenye afya yao ya kiakili,  kwa sababu wengi wao hawaithamini na wapo radhi kuishi hata bila ya kuwa katika taasisi hiyo muhimu katika jamii.

Related Posts