Watalii sasa wanaweza kuomba viza kwa mtandao

Dodoma. Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji imeanzisha mfumo wa maombi ya viza kwa njia ya mtandao (e-Visa) unaowawezesha watalii kuomba viza popote walipo duniani bila kulazimika kufika ubalozini, hivyo kurahisisha upatikanaji wake.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Juni 4, 2025 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula alipokuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa Manyoni Magharibi (CCM), Dk Pius Chaya.

Dk Chaya amehoji ni jitihada gani zimefanyika kurahisisha upatikanaji wa viza kwa watalii wenye uraia tofauti wanaokuja nchini kwa mwitikio wa Royal Tour.

Akijibu swali hilo, Kitandula amesema Serikali imeendelea kuboresha utaratibu wa utoaji wa viza nchini ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

“Mathalan, Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji imeanzisha mfumo wa maombi ya viza kwa njia ya mtandao (e-Visa) unaowawezesha watalii kuomba viza popote walipo duniani, bila kulazimika kufika ubalozini,” amesema.

Amesema Serikali imeboresha Kanuni za Uhamiaji za mwaka 2023 (GN 428) ambapo kwa sasa watalii wanaotumia Visitors Pass wanaruhusiwa kutembelea Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kurejea Tanzania bila hitaji la kuomba upya pasi ya kuingia nchini, alimradi pasi aliyopewa iwe haijaisha muda wake.

Amesema  Serikali imeendelea kuingia makubaliano na nchi mbalimbali ili kurahisisha utaratibu wa viza ambapo kwa sasa raia wa nchi 71 hawahitaji viza wanapoingia nchini.

Aidha, amesema kwa sasa watalii kutoka mataifa mengi zaidi duniani wanaruhusiwa kupata viza wanapowasili (visa on arrival) kwenye viwanja vya ndege vya kimataifa kama Julius Nyerere (Dar es Salaam), Kilimanjaro na Zanzibar.

Amesema vilevile, Serikali imefanya mapitio ya nchi zilizo kwenye kundi la viza rejea kwa lengo la kufanya maboresho.

Katika swali la nyongeza, Dk Chaya amehoji nini mkakati wa kuhamasisha utalii wa utamaduni wa asili wa mikoa ya Dodoma na Singida.

“Manyoni katika tarafa ya Kilimatinde ilikuwa ni njia ya watumwa je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha tunaboresha malikale ya Kilimantinde ili iweze kutumika katika utalii,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Kitandula amesema Serikali imekuwa ikifanya mikakati ya kushirikiana na mikoa tofauti kukutana na wadau katika eneo hilo kwa kuainisha maeneo ambayo yanaweza kuwa vivutio kwa watalii,  na aina ya vyakula vinavyoweza kutumika kutangaza utalii kwenye maeneo yao.

“Hivi tunavyozungumza kuna matamasha yanaendelea utalii wa asili Dodoma ambayo yanahusisha pia kutembelea mashamba ya zabibu na kuangalia vikundi vya utamaduni, lakini kupata fursa ya kuona mila na utamaduni wa mkoa wa Dodoma,” amesema.

Amesema kwa Mkoa wa Singida wanafanya mawasiliano kuainisha vivutio vya utalii ili wanapofanya kongamano kubwa vionyeshwe.

Aidha, Kitandula amesema timu ya wizara hiyo imeshakwenda mkoani humo ikiwemo Wilaya ya Manyoni ambapo kuna maeneo waliyoyabaini ni vivutio yakiwemo yanayomilikiwa na Kanisa la Anglikana.

Kitandula ametaja maeneo mengine ni bomba la kale la Mjerumani na njia ya kati ya watumwa iliyopo Kilimatinde mkoani Singida.

“Mpango ni kukaa na wadau ili kuona yale ambayo wanayamiliki tuweze kutangaza kwa pamoja na yake ambayo wapo tayari kuyaachia ili Serikali iyasimamie tutafanya hivyo,”amesema.

Related Posts