Dodoma. Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Fedha ya Sh20.3 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26, huku Sh14.21 trilioni zimetengwa mahsusi kwa ajili ya kulipia deni la Serikali linalotarajiwa kuiva ndani ya mwaka huo wa fedha.
Mbali na hayo, Mbunge wa Ole (CCM), Juma Hamad Omari, amelalamikia malipo madogo ya pensheni kwa wastaafu waliotumika katika Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, hali inayosababishwa na mishahara midogo waliokuwa wakilipwa wakati huo.
Kati ya fedha hizo Sh20.1 trilioni zilizoidhinishwa na Bunge, Sh769.89 bilioni ni kwa ajili ya matumzi ya maendeleo huku kati ya hizo Sh122.5 bilioni zikienda katika Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26, leo Jumatano Juni 4, 2025 Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba amevitaja vipaumbele vitano ambavyo fedha hizo zinaelekezwa.
Vipaumbele hivyo ni kutafuta na kukusanya mapato ya jumla ya Sh50.17 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali.
“Kuhudumia kwa wakati deni la Serikali linalotarajiwa kuiva la jumla ya Sh14.22 trilioni na kujenga mfumo wa pamoja wa kutoa ankara za malipo ya Serikali ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato,” amesema.
Ametaja vipaumbele vingine ni kuboresha, kuunganisha na kuimarisha usalama wa mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa fedha na mali za umma na kuandaa Sera ya Usimamizi wa Mali za Umma.
Dk Mwigulu amesema katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili 2025, Serikali imelipa jumla ya Sh996.5 bilioni.
Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo Sh918.8 bilioni za makandarasi, wazabuni Sh38.4 bilioni na watumishi wa umma Sh38.8 bilioni.
Kwa upande wa huduma za mafao ya kustaafu, pensheni na mirathi, Dk Mwigulu amesema hadi kufikia Aprili 2025, wizara imelipa kwa wakati Sh315.08 bilioni kama mafao ya kiinua mgongo.
Amesema malipo hayo yamefanyika baada ya kupokea nyaraka kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kuhusu malipo ya deni la Taifa, Dk Mwigulu amesema hadi Aprili 2025, jumla ya Sh10.19 trilioni zimelipwa kwa notisi za madai ya deni lililoiva, sawa na asilimia 84.8 ya lengo la mwaka.
Amesema kati ya kiasi hicho, malipo ya deni la ndani ni Sh6.01 trilioni, riba ni Sh2.48 trilioni na mtaji Sh3.53 trilioni na deni la nje ni Sh4.18 trilioni, riba ikiwa ni Sh1.62 trilioni na mtaji Sh2.56 trilioni.
Walalamikia pensheni ndogo
Mbunge wa Ole (CCM), Juma Hamad Omary amesema kutokana na mishahara midogo katika kipindi cha utawala wa Rais Julius Nyerere na Rais Ali Hassan Mwinyi pensheni kwa wastaafu wa wakati huo zimekuwa ni ndogo.
Amesema mwaka 1987 alipeleka bungeni azimio la kupandisha mshahara wa Rais wakati huo ulikuwa ukiletwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa.
Omary amesema mshahara wa Rais ulikuwa ni kati ya Sh30,000 na Sh50,000 huku wengine wa chini walikuwa wakilipwa Sh20,000.
“Pensheni ilikuwa ikitegemea mshahara wa mwisho na iwapo mshahara wa mwisho ni mdogo na pensheni yako inakuwa ni ndogo. Sasa kilichotokea baada ya kustaafu, (yeye) alipokuja Mkapa (Rais Benjamin Mkapa), mshahara ikaanza kupanda,”amesema Omary.
Hata hivyo, watu waliokuwa wakifanya kazi katika Serikali hizo mbili pensheni yao ni kima cha chini na kuwa yeye ni miongoni mwa watu hao ambaye anaenda kuchukua pensheni ya kila mwezi ya Sh140,000.
“Kuna wanajeshi makanali walipopigana vita, wanapata chini ya Sh120,000 sasa mtu anayetoka Makunduchi kuja kuchukua pensheni ya 120,000 nadhani hiyo ni nauli yake tu,”amesema Omary.
“Lakini mawaziri waliongia baada ya kipindi cha Mkapa (Rais mstaafu Benjamin Mkapa) wanapata. Nashauri hapa nchini pensheni inatolewe kutokana na hali ya maisha na mfumko wa bei unapobadilika na pensheni irekebishwe. Kwa vyovyote isiwe chini ya kima cha chini,”amesema Omary.
Kwa mara ya mwisho Serikali ilitangaza kupandisha kima cha chini cha mshahara kutoka Sh100,000 hadi Sh150,000 Januari mwaka 2025.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Twaha Mpembenwe amesema kamati hiyo inashauri Serikali kufanya mabadiliko kwenye Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ili Mfumo wa malipo kwa njia ya kielektroniki (Cashlite) uanze kutekelezwa.
“Kwa muda mrefu Kamati imekuwa ikiishauri Serikali kuhusu kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kutumia mifumo ya kielektroniki katika kufanya malipo ili kuzuia upotevu wa mapato yatokanayo na kodi,”amesema.
Amesema malipo ya kielektroniki ni miamala inayofanyika kupitia kadi za malipo, simu za mkononi na malipo ya papo kwa papo.
“Lengo ni kurahisisha miamala na kupunguza utegemezi wa fedha taslimu,”amesema.
Aidha, Mpembenwe ameshauri pamoja na kwamba kuna Sheria mbalimbali za kodi nchini, Tanzania haina sera ya kodi moja inayotoa muongozo wa masuala mbalimbali.
“Kukosekana kwa sera hiyo kunasababisha nchi yetu kutokuwa na viwango vya kodi vinavyotabirika pamoja na kuongeza vitendo vya ukwepaji wa kodi. Hivyo, Kamati inaona kwamba kuna umuhimu wa kuandaa sera ya kodi ili kutoa mwongozo wa masuala yote ya kodi,”amesema.
Mbunge wa Kalembo (CCM), Josephat Kandege amesema watu wengi hawapendi kutumia malipo kwa njia ya kieletroniki kwa sababu gharama ni kubwa.
“Pale ambako unafanya miamala ukaja ukafuatilia gharama zinazotozwa ni kubwa sana kwa hiyo naiomba Serikali wahakikishe wanafanya mapitio kuhakikisha gharama za kulipa kwa kutumia njia mitandao zinashuka,” amesema.
Amesema utaratibu huo unasaidia kupunguza wizi kwa kuzuia watu kukwepa kodi, rushwa, kutakatisha na kuibiwa fedha na kuitaka Serikali kushusha gharama ili kuhamasisha matumizi ya miamala ya kieletroniki kwenye ununuzi.
Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni amesema Wizara ya Fedha ina kazi kubwa ya kufanya kuzuia ukwepaji wa kodi ambao amedai unafanywa na baadhi ya wafanyabiashara kutoka Bara la Asia.
“Ukimwambia alete akaunti atakushawishi hadi ulipe ‘cash’ (taslimu), unapomuomba risiti anakupa hadi elimu kwa nini akupe na asikupe risiti…Sasa hii elimu ya ujasiri ya kukwepa kodi Watanzania hatukuwa nayo, tunaanza kupandikizwa ujasiri wa kukwepa kodi,” amesema Mageni.
Pia, amesema ili kuondoka katika changamoto hiyo ni lazima kubadili utaratibu wa kulipa fedha taslimu badala yake kulipa kwa njia ya kieletroniki pamoja na kupunguza makato ya kutumia utaratibu huo.
Pia, ameshauri kuongeza ufanisi katika mifumo ya malipo ambayo wakati mwingine mtu anapotaka kuitumia anashindwa hivyo kwa kuwa inagoma.
Akihitimisha hoja hiyo, Dk Mwigulu amesema Serikali haikopi zaidi ya kilichopitishiwa na Bunge na haikopi kwenda kupeleka kwenye matumizi yasiyo ya maendeleo.
“Kitachofanyika mnakusanya mnapeleka kwenye miradi ya maendeleo, tafsiri yake ni kwamba mradi ambao unaweza kuujenga kwa kwa miaka mitano kwa kuchukua fedha kubwa mathalani dola za Marekani bilioni tatu kama wa reli ya kisasa ungeamua kuujenga kwa ‘cash’ bajeti kwa makusanyo ya kila mwezi ungejenga kwa miaka 40,”amesema Dk Mwigulu.
Amesema Serikali ndio inafanya hivyo kwenye deni la Taifa, asilimia 67 ya mikopo ni ya miradi na ni mikopo ya midogo kutoka taasisi za kifedha za kimataifa ambayo kipindi chake cha kurejesha ni miaka 30 hadi 40.
“Ndio maana nikiwa waziri hapa nimeshuhudia ulipwaji wa mikopo ya Serikali ya awamu ya kwanza na ya pili. Ni mikopo ya muda mrefu. Mradi ambao ulianzishwa na Serikali ya awamu ya kwanza tungeamua kulipa kwa mapato ya mwezi ndio ingetakiwa sasa hivi mradi mmoja uwe unamalizika,”amesema.
Hata hivyo, amesema kwa zaidi ya asilimia 72 ya de ni ile mikopo ya muda mrefu ambayo riba yake ni ya chini na takribani asilimia 23-24 ndio ambayo inaangukia kwenye mikopo ya kibiashara na yenyewe inakuwa kwenye maeneo mahususi sana.