DC Siha alaani tabia ya kupuuza utunzwaji wa miti iliyopandwa

Siha. Mkuu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Dk Christopher Timbuka ameeleza kutoridhishwa na tabia ya baadhi ya wananchi na taasisi za Serikali kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, kisha kuiacha bila kuitunza.

Dk Timbuka ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 5, 2025, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ngazi ya wilaya, yaliyofanyika katika viwanja vya Zahanati ya Lawate.

Akizungumza baada ya kupanda miche ya miti ya aina mbalimbali ikiwamo ya matunda, mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa tabia ya kupuuza utunzaji wa miti ni kikwazo kikubwa kwa juhudi za Serikali za kutaka kufikia malengo ya upandaji miti kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.

“Kwa kweli si jambo jema tunapopanda miti halafu baadaye tunakuta haipo tena. Huo ni upotevu wa muda na rasilimali za Serikali,” amesema Dk Timbuka.

Amesema changamoto kubwa si kupanda miti pekee, bali ni kuhakikisha miti hiyo inatunzwa na kustawi.

Alitoa mfano wa jitihada za awali alizoshiriki tangu alipowasili Siha, anasema walipanda miti katika kituo cha Polisi Sanya Juu, lakini baadaye akaambiwa ilikufa yote, jambo ambalo alithibitisha baada ya kwenda kujionea mwenyewe.

“Tulipanda pia maeneo ya Someli na Dachcona hadi karibu na Hashu, lakini miti iliyoota ni michache sana. Hii siyo hali nzuri, tunajidanganya wenyewe,” amesema.

Amesisitiza kuwa jambo la msingi ni kuhakikisha miti inapandwa na kutunzwa kwa bidii hadi ikue, akieleza kuwa hilo ndilo lengo kuu la wilaya katika kulinda na kuboresha mazingira.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Dancani Urasa amesema wamekuwa wakitekeleza wito wa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa lengo la kuimarisha mazingira.

“Ni kweli miti imesambazwa kwa kiwango kikubwa. TFS (Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania), wamefanya kazi nzuri mwaka huu kwa kusambaza zaidi ya miche 170,000 katika taasisi mbalimbali za Serikali. Tunapaswa kuzingatia wito wa mkuu wa wilaya kuhusu kuitunza miti hiyo ili ikue,” amesema Urasa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Haji Mnasi amesema kuna umuhimu wa kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo: Tuwajibike Sasa.”

Amewahimiza wananchi na viongozi wote wa taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali na kupunguza matumizi ya plastiki.

Aidha, Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Msikiti wa Sanya Juu na Mwenyekiti wa Jumuia ya Maridhiano na Amani Tanzania, Hamisi Idd amepongeza shughuli hiyo ya upandaji miti huku akitoa wito kwa wananchi kuhakikisha amani inadumishwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Related Posts